July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Utalii wa faru weupe kuanzishwa hifadhi za Burigi-Chato, Mikumi

Faru

Spread the love

WAZIRI wa Mali Asili na Utalii, Dk. Pindi Chana amesema katika kupanua wigo wa utalii na mapato, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) litaanzisha utalii wa faru weupe katika hifadhi za Taifa Burigi – Chato na Mikumi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Aidha, amesema Shirika litawezesha kuanza rasmi kwa uwekezaji katika maeneo ya utalii maalum katika Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Dk. Chana ameyasema hayo leo Ijumaa tarehe 3 Juni, 2022 bungeni jijini Dodoma akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23 yenye jumla ya Sh 624 bilioni kwaajili ya matumizi ya maendeleo na kawaida.

Mbali na hilo Dk. Chana amesema, Shirika litashiriki maonesho ya utalii katika masoko 19 ya nchi za India, Brazil, Argentina, Qatar, Uholanzi, Ufini, Poland, Urusi, Uswisi, Ujerumani, Israel, Ubelgiji, Marekani, Uhispania, Uingereza, Ufaransa, China, Korea ya Kusini na Italia.

Katika kuboresha miundombinu ya huduma za utalii, Dk. Chana amesema Shirika litajenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 2,500 katika hifadhi za Taifa Arusha, Burigi – Chato, Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Udzungwa, Manyara, Rubondo, Rumanyika – Karagwe, Ruaha, Mikumi, Nyerere na Serengeti.

Amesema pia, Shirika litajenga njia za utalii zenye urefu wa kilomita 251 na barabara za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 342.5.

“Vilevile, Shirika litakarabati barabara zenye urefu wa kilomita 6,500; na viwanja vya ndege 17 katika hifadhi za Taifa Ruaha, Mikumi, Nyerere, Saadani, Tarangire, Mkomazi na Serengeti. Pia, Shirika litajenga nyumba 77 za makazi ya watumishi katika hifadhi za Taifa Kigosi, Mto Ugalla, Nyerere, Gombe, Serengeti na Ruaha.”

Katika kuhakikisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu unakuwa endelevu Dk. Chana amesema Shirika litaanzisha Kikosi Kazi cha Ujenzi kwa ajili ya kuhudumia miundombinu ya shirika na iliyo nje ya shirika kibiashara.

Waziri wa Mali Asili na Utalii, Dk. Pindi Chana

Mbali na hayo amesema kazi nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na ununuzi wa magari tisa (9), seti mbili (2) za mitambo ya kutengeneza barabara, boti moja (1), injini za boti tatu (3) na pikipiki nane (8).

Katika hatua nyingine, Dk Chana amesema Shirika litaanza kurusha mubashara (Live streaming) shughuli na matukio ya vivutio vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

error: Content is protected !!