July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Utafiti wa Lowassa waibua utata

Waziri mkuu mstaafu na mbunge wa Jimbo la Monduli Bw.Edward Lowassa akikabidhiwa mkuki kama ishara ya kukabidhiwa majukumu ya kuwa mlezi wa Machifu Tanzania

Spread the love

UTAFITI uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Positive Thinkers Tanzania (PTT), umeelezwa “kupikwa” kwa na lengo la kumpendelea Edward Lowassa- Mbunge wa Monduli. Anaandika Pendo Omary ….. (endelea).

Mtoa taarifa wa gazeti hili amesema “Kuna kila dalili kuwa, Lowassa amefadhili utafiti huu na matokeo yake ni ya kupikwa”.

“Hii kampuni inayodaiwa kufanya utafiti iko mtaa mmoja, jengo moja na ghorofa moja na kampuni binafsi za Lowassa. Bila shaka ni watu wanaojuana,”amesema mtoa taarifa.

Baadhi ya kampuni binafsi za Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kwa kashfa ya ufisadi wa Richmond, zinazosimamiwa na mtoto wake, Frederick Lowasa ni; Alphatel, Barare Limited na Intergraded Property Investment Limited.

Anuani ya ofsi hizi ni: Ghorofa ya nne, Jengo la Mavuno, mtaa wa Maktaba, jijini Dar es Salaam.

Gazeti la MwanaHALISIOnline limemtafuta Tibatizibwa Gulayi Yabatinga- Rais wa PTT, ili kujibu madai hayo ambapo amesema, “sio kweli kwamba tumepika matokeo ili kumpendelea Lowassa”.

“Mtu yoyote kama Bernard Membe, January Makamba na Samuel Sitta wanaweza kudhani tumeyapika. Mbona maeneo kama Mbeya, Iringa na Mwanza ameongoza Dk. Wilbrod Slaa,” amesema Yabatinga.

Yabatinga amesema utafiti huo ulifanywa kwa njia ya ana kwa ana na kwa simu huku washiriki wa njia ya simu wakipatikana kupitia mtandao wa “Whatsapp”.

“Mimi nimejiunga na Whatsapp. Nimejiunga na makundi kama sita kwenye mtando huu. Nilichukua namba kwenye magroup (makundi), na kuwauliza mahali walipo na nilipojua kama wapo kwenye mikoa tuliyokuwa tunafanya utafiti, nikawahoji,” amefafanua Yabatinga.

Yabatinga alitoa majibu hayo baada gazeti hili kumuuliza ni namna gani waliwapata washiriki kwa njia ya simu na namna gani waliweza kudhibiti udanganyifu wa mshiriki kuhusu eneo analoishi.

Matokeo ya utafiti huo yalitangazwa Jumapili iliyopita, yakionesha Lowassa akikubalika zaidi miongoni mwa wanasiasa 15 wanaotajwa kuwania urais katika uchaguzi mkuuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Aidha, Dk. Slaa – Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anashika nafasi ya pili akifuatiwa na Mwigulu Nchema- Naibu Waziri wa Fedha.

Utafiti huo ulifanyika Februari mwaka huu na ulihusisha mikoa 13 na kushirikisha watu 3,298.

Matokeo ya utafiti huo unaonesha CCM imeongoza kwa kupata kura 1,144 sawa na asilimia 34.68, Chadema kura 1,117 (asilimia 33.86), Chama cha Wananchi CUF kura 360 (asilimia 10.91) na NCCR Mageuzi kura 77 (asilimia 2.33).

Washiriki katika utafiti huo walitaja kiongozi wanayemtaka lazima awe na sifa za utendaji kwa vitendo, uadilifu, uzoefu na elimu bora.

Wanasiasa wengine waliopigiwa kura ni; Prof. Ibrahimu Lipumba, John Magufuli, Zitto Kabwe, Bernard Membe, Mizengo Pinda, January Makamba, Prof. Mark Mwandosya, James Mbatia, Dk. Hussein Mwinyi, Steven Wasira, Fredrick Sumaye na Samuel Sitta.

error: Content is protected !!