May 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Utafiti: darasa la saba wengi ‘Mbumbumbu’

Spread the love

UTAFITI uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza, ili kupima hali ya elimu hapa nchini kwa mwaka 2015, umeonyesha kuwa wanafunzi wengi wa darasa la saba hawana uwezo wa kusoma wala kujibu maswali ya darasa la pili, anaandika Charles William.

Ripoti ya matokeo ya utafiti huo, imehusisha jumla ya wanafunzi 32,694 kutoka kaya 16,013, katika shule za msingi 1,309 imetolewa na taasisi ya Twaweza.

Wanafunzi wanne kati ya kumi wa darasa la saba (40%), hawawezi kusoma hadithi za kingereza za darasa la pili, huku 16% ya darasa la saba, wakiwa hawawezi kusoma hadithi za darasa la pili na 23% ya darasa la saba, hawawezi kufanya hesabu za kujumlisha za darasa la pili.

Mbali na kupima uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi hususani wa darasa la saba katika shule za serikali, utafiti huo pia umepima utoro wa walimu katika shule za serikali pamoja na uwiano wa upatikanaji wa vitabu kulingana na idadi ya wanafunzi.

Katika mkoa wa Singida, kiwango cha utoro wa walimu ni 58% wakati katika mkoa wa Ruvuma na Manyara utoro wa walimu ni 17% pekee. Uwiano wa wanafunzi kwa mwalimu mmoja kwa mkoa wa Mara ni wanafunzi 126 ilihali katika mkoa wa Pwani ni wanafunzi 56 kwa mwanafunzi mmoja.

“Takwimu za tafiti zetu, zinalenga kutoa fursa kwa watunga sera kufahamu ni wapi pa kuanzia na pia kutoa picha halisi ya nini tunachovuna kutokana na uwekezaji mkubwa tunaofanya katika sekta ya elimu,” amesema Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza.

Wakati utafiti ukionyesha baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba, hawawezi kusoma na kujibu maswali ya darasa la pili. Hali ni mbaya zaidi kwa darasa la tatu waliopewa majaribio ya darasa ka pili.

46% ya wanafunzi hao wa darasa la tatu, hawawezi kusoma hadithi za Kiswahili za darasa la pili, 81% hawawezi kusoma hadithi za kingereza za darasa la pili na 65% hawawezi kufanya hesabu za za darasa la pili.

Ripoti hiyo imeonyesha kutokuwepo kwa uwiano wa vifaa vya kitaaluma, walimu pamoja na mazingira ya wanafunzi kusoma katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Huku mazingira hayo yakichangia matokeo mabaya kwa kiasi kikubwa.

Kitaifa, 65% ya wanafunzi hawajaandikishwa katika shule za awali, hata hivyo 84% kati yao ni wale wanaoishi vijijini. Wakati kitabu kimoja kikitumiwa na wanafunzi 26 mkoani Tabora, katika mikoa ya Kilimanjaro, Ruvuma na Njombe kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi watatu.

error: Content is protected !!