July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Usiri wa kamati za Bunge, wawavuruga Wabunge

Spread the love

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amekuwa gumzo miongoni mwa wabunge, kufuatia hatua yake ya kufanya siri katika uteuzi wa wabunge wanaounda kamati za kudumu za bunge. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Hali hiyo ilibainika jana, baada ya wabunge kuwasili mjini Dodoma na kuanza kujisajili, tayari kwa kukutana leo ambapo ndipo kila mmoja wao atatangaziwa na Spika mwenyewe, amechaguliwa kuunda kamati gani.

Utafiti uliyofanywa na MwanaHALISI Online kwa siku nzima ya jana, ulibaini hakukuwa na wabunge waliokuwa na taarifa kuhusu wameteuliwa kuunda kamati gani.

Mmoja wa wabunge vijana kutoka Nyanda za Juu Kusini, kwa sharti la kutotajwa jina lake, amesema wabunge wanaowania uenyekiti na makamu mwenyekiti wa kamati mbalimbali ni wengi, lakini mbali na kujipitisha kwa wenzao kuomba kuchaguliwa, walikumbana na kigingi cha kutofahamu watateuliwa kuwa kwenye kamati gani.

Amesema wengi wa wabunge hao walikuwa wakijipitisha kueleza nia yao hiyo, ni waliokuwa bungeni kwa muda mrefu. Alipongeza uongozi kwa usiri uliyowekwa akisema hapati picha hali ingekuwaje endapo wabunge hao wangekuwa wanafahamu kamati walizoteuliwa na wajumbe wa kamati hizo.

Ally Kessy (Nkasi-CCM) ambaye ni awamu ya pili kuwa bungeni, amesema kasi ya wenye nia ya kugombea uongozi wa kamati imepungua ikilinganishwa na bunge lililopita.

Naye alipongeza usiri uliyowekwa na Spika wa Bunge katika uteuzi wa kuunda kamati hizo, akisema itasaidia kupata viongozi wenye nia ya kutumikia wananchi bila kuendekeza maslahi binafsi.

“Wabunge wote tupo sawa, tunawakilisha na kutumikia wananchi. Uongozi wa kamati ni sehemu ya utumishi, iweje mtu autafute kwa kutumia hata hongo? Naona wamefanya vizuri sana,” alieleza Kessy

Naye Magdalena Sakaya (Tabora), ambaye pia ni Katibu wa Chama Cha Wananchi CUF-Taifa, amesema kambi ya upinzani bungeni imedhamiria kuhakikisha haitoi mwanya kwa ‘mamluki’ kuongoza kamati mbili, ambazo huongozwa kwa mujibu wa kanuni huongozwa na upinzani.

Kamati hizo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (RAC), ilielezwa na Sakaya kwamba, pamoja na kuwepo wabunge miongoni mwao ambao wanaotamani kuziongoza, wanafahamu kuwepo uwezekano wa watu wasiokuwa waadilifu, kupandikiza wagombea wanaoweza kurubuniwa na hatimaye kuhujumu umma.

Dk. Prudensiana Kikwembe, amesema ingawa wameshangazwa na usiri ambao ulisababisha mpaka jana jioni kutokuwepo mbunge aliyefahamu kamati aliyopangwa, wengi wanafurahia kwakuwa ilisaidia kupunguza kasi ya ushawishi, watu kujipenyeza kwenye kamati kwa maslahi binafsi.

error: Content is protected !!