August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ushirikina watikisa watumishi serikalini

Jumanne Sagini, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu (kulia) akifafanua jambo

Spread the love

WANACHAPWA bakora, wakiwa wamelala ndani wanajikuta wapo nje bila kujua wametokaje. Hawa ni watumishi wa umma katika Mkoa wa Simiyu, anaandika Dany Tibason.

Hatua hiyo imeonekana kumkera Jumanne Sagini, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu ambapo amesema, kitendo cha wakazi hao kuwachapa watumishi hao na na kuwalaza nje kwa njia za kishirikina, kimesababisha wengi wahame mkoa huo.

Sagini ametoa kauli hiyo mjini hapa jana katika Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alipopewa nafasi ya kueleza hali halisi ya mkoa huo kabla ya kamati kufanya mahojiano na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima.

Amesema, wakazi wa mkoa huo wamekuwa na tabia ya kuwachapa watumishi wa umma wakiwemo walimu hadharani mara wanapokiuka mila na desturi za eneo jambo ambalo ni kinyeme cha kanuni na sheria za utumishi wa umma.

Sagini ambaye, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, alifafanua kuwa mbali na watumishi kuchapwa pia wamekuwa wakijikuta wamelala nje wakati wao walikuwa wamelala ndani.

“Mimi nilipofika pale nimekuta mambo hayo ambayo ni ya ajabu sana, nimewambia kamwe watumishi hawawezi kukaa na kufanya kazi huku mtabaki nyuma wakati wote.

“…, kama walimu wanawafundishia watoto wenu wanakuwa madaktari na vyeo mbalimbali serikali leo mnawachapa fimbo hadharani, nikawambia lazima mbadilike,”amesema.

Amesema, hali hiyo imesababisha mkoa na halmasauri zake za wilaya kukosa watumishi ambao ni wataalam na hivyo kuwa katika hali mbaya kiutendaji.

Katibu tawala huyo amesema, wamefika pale lakini hakuna wataalam wa kutosha na wachache waliopo  ni wageni na kwamba, wakipelekwa watalam wanakaa mwezi, miezi mwaka mmoja na baadaye wanaondoka kutokana na tabia za wakazi wa eneo hilo.

Amesema, kukosekana kwa wataalam, kumesababisha washindwe kuandaa vitabu vya LAAC, kushindwa kujibu hoja za Mkaguzi na Mhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hivyo vitabu vilivyokuja mbele ya kamati yako ni vya hovyo kabisa wala havifai.

Hata hivyo, kamati hiyo ilishindwa kufanya mahojiano na halmashauri hiyo, kwa madai kuwa imejaa madudu, ubadhirifu hivyo kamati haiko tayari kuwahoji na kuishia kutoa maagizo.

Sagini aliomba nafasi ili atumie uzoefu alionao kwa kufanya kazi muda mrefu TAMISEMI, kushirikiana na watendaji waliopo ili waweze kuandaa upya vitabu vya LAAC, kujibu hoja za CAG na kuziwasilisha kwa CAG kwa ukaguzi na ndipo warejee tena kwenye kamati hiyo kwa mahojiano.

“Mheshimiwa mwenyekiti, nimeona nizungumze hali halisi iliyopo kwa utangulizi ili kamati yako ijue ni wapi pa kuanzia na kuishia, binafsi nimepitia vitabu hivyo sijaridhika kabisa, licha ya kuwa watendaji wanaweza kuwa wanajiamini na kuwa tayari kuhojiwa ila mimi nasema hakuna kitu hapa,”amesisitiza.

Kwa upande wake Daudi Nyalamu, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amekiri kuwepo kwa vitendo hivyo katika eneo hilo ambapo ameahidi kukaa na wenzake na kubadili tabia hiyo na kuikomesha kabisa.

“Ni kweli kabisa kama alivyosema, RAS hali halisi ndivyo ilivyo, watendaji hawakai wanahama mara kwa mara hivyo utendaji kuwa mgumu, haya ambayo kamati mmetuagiza, tutakwenda kushirikiana na kuyafanyaia kazi,” amesema.

error: Content is protected !!