Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Ushauri mzito kwa Makonda, atakiwa kuomba radhi
Makala & UchambuziTangulizi

Ushauri mzito kwa Makonda, atakiwa kuomba radhi

Paul Makonda
Spread the love

 

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda, ameshauriwa kuwaomba radhi hadharani viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, wafanyabiashara na baadhi ya wananchi na makundi aliowakosea akiwa madarakani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ushauri huo umekuja siku chache baada ya Makonda kulalamika mitandaoni, kwamba kuna makundi matano ya watu yamepanga kummaliza na kuangamiza maisha yake.

Malalamiko ya Makonda yamekuja kipindi ambacho kuna taarifa kwamba yuko hatarini kufikishwa mahakamani na Jamhuri akituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Vyanzo vya kuaminika kutoka serikalini kwa nyakati tofauti vimeidokeza MwanaHALISI Online, kwamba uchunguzi dhidi yake unaendelea, ikiwamo kuhojiwa na mamlaka husika na kinachosubiriwa ni taratibu.

Wiki iliyopita katika ukurasa wake wa Instagram, Makonda aliandika maelezo marefu ya mkakati aliodai unaratibiwa na makundi matano, yenye lengo la kuangamiza maisha yake.

Alitaja makundi hayo ni wauza dawa za kulevya, wanufaika na dawa za kulevya, wapenzi wa jinsia moja, wanaokesha usiku kucha kutafuta kulipa kisasi kwa wasaidizi wa Dk. John Magufuli na waliowahi kuwa sehemu yake.

Askofu wa Kanisa la Pentekoste, William Mwamalanga ni mmoja wa watu waliojitosa kutoa ushauri kwa Makonda, akimtaka amrudie Mungu ili moyo wake ufufuke na Yesu Kristo.

Askofu Mwamalanga alisema kwa kifupi, Makonda anayedaiwa kuumiza watu wengi wakati wa utawala wake, akubali makosa kwamba ndiyo yaliyomfikisha hapo, badala ya kueleza kuna makundi yanataka kumwua.

“Makonda amtafute Mungu wake, amsamehe na Mungu atamwonesha njia ya kufikia aliowakosea. Alijawa kiburi, amesababisha watu wafikishwe mahakamani, ameharibu heshima na utu wao, hivyo awaombe radhi, atubu,” alioshauri Mwamalanga.

Mwingine aliyempa ushauri Makonda ni William Malecela ‘Lemutuz’, mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu, Samuel Malecela, ambaye aliandika waraka mrefu mitandaoni kuhusu Makonda.

Lemutuz ambaye alikuwa moja wa watu wa karibu sana na Makonda, alisema katika waraka huo, kwamba kiongozi huyo wa zamani, asihangaike na maadui wa nje bali aanze na adui namba moja wa ndani ya moyo wake, na ndiye aliyekuwa akitesa watu.

“Ndugu yangu, mimi sina tatizo na wewe, lakini ninakutana kila siku na viongozi na wananchi wa kawaida wenye matatizo na wewe. Inasikitisha sana wakianza kuongea mambo ya hovyo uliyowafanyia.

“Kuna viongozi uliwakosea na kuna wananchi uliwakosea. Simama juu uhesabiwe, waombe radhi na hasa mwombe Mungu wako akusamehe mambo mengi ambayo yanakutesa leo, bila wewe kujua sababu,” alisema Lemutuz.

Mtoto huyo wa Malecela, alimsisitiza Makonda asiendelee kukaa gizani na kujidanganya kwamba anachukiwa, bali chuki nyingi zinazomtesa leo, alijitakia.

Kwa mujibu wa waraka huo wa Lemutuz, Makonda alikosea adabu baadhi ya viongozi wakubwa katika Taifa, kwa sababu ya ukaribu wake na Rais Magufuli.

Alitaja baadhi ya viongozi aliowakosea adabu kuwa ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati huo akiwa Waziri wa Fedha.

William Malecela ‘Lemutuz’

Makonda na Dk Mpango waliingia kwenye mzozo baada ya kuingiza nchini kontena bila kulipia kodi akidai kuwa ni samani kwa ajili ya walimu, huku Dk. Mpango akisisitiza kuwa lazima zilipiwe kodi.

“Kwa mfano vita vyako na Makamu wa Rais, Dk. Mpango. Mwishoni mwa vile vita mimi niligundua, kwamba ulikuwa na makosa kwa sababu hata Rais Magufuli aliniambia kwa simu akiwa Chato, kwamba ni Waziri wa Fedha pekee ndiye mwenye mamlaka ya kukusamehe kodi.

“Nikaamua kumwandikia Waziri Mpango waraka wa kukuombea radhi hadharani, matokeo yake ulinikasirikia na hata sherehe ya uzinduzi wa kitabu changu, uligoma kuhudhuria kwa hasira,” alisema Lemutuz.

Alimtaja kiongozi mwingine anayepaswa kuombwa radhi, kuwa ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kwamba naye alimkosea sana akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alikusaidia sana katika maisha yako ya siasa mpaka akakupa ukuu wa wilaya Kinondoni, lakini kumbuka uliyomlipa kwa kumtangaza mtoto wake Ridhiwani, kuwa ni ‘mwuza unga’

“Ndugu yangu hawa wote wanahitaji kuombwa msamaha wa dhati kutoka moyoni. Nimeamua kuvunja ukimya baada ya kuona unaanza kutoka nje ya mstari,” alisema.

Alisema tabia ya Makonda ilianza kubadilika baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwani hakuna kiongozi mwingine aliyemsikia na kumheshimu zaidi ya Rais Magufuli.

“Hivi ni wewe peke yako ndiye uliyekuwa karibu na Rais Magufuli? Kwani Waziri Mkuu hakufanya kazi karibu na Magufuli? Kwani Rais wa sasa, Mama Samia hakufanya kazi karibu na Magufuli? Mbona hakuna makundi yanayopanga kuwamaliza isipokuwa ni wewe tu?

Mshauri mwingine kwa Makonda ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, aliyemtaka kama ana madai ya kutaka kuuawa basi akatoe taarifa kituo chochote cha Polisi kilicho karibu.

Kamanda Muliro alimhakikishia Makonda kuwa teknolojia ilivyo hivi sasa ni rahisi kufanya uchunguzi na kubaini au kuthibitisha kuwapo kwa hila kama hizo.

Tuhuma za Makonda

Makonda, anadaiwa kujimilikisha kimabavu kiwanja namba 60 Title no.186153/60 kilichoko Regent Estate Kinondoni, mali ya Ghalib Said Mohamed (GSM).

GSM alipewa kibali cha ujenzi wa eneo hilo Oktoba 16, 2017 chenye namba 00020032.

GSM aliilipa malipo ya awali kampuni ya Ujenzi wa Group Six International Januari 31, 2018, Sh milioni 51.92 ambayo yanathibitishwa kupitia kwenye mifumo ya kodi Mamlaka ya Mapato (TRA). Sakata hili halijulikani limeishia wapi.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Hamduni aliieleza Raia Mwema hivi karibuni, kwamba makachero wake wamekuwa na kazi nzito ya kukusanya taarifa za kiintelijensia kabla ya kuvaa wahusika.

“Uchunguzi una hatua zake. Tangu sakata hili lianze tumekuwa tukikusanya taarifa na kufanya uchunguzi wa awali, kuangalia ilipo jinai.

“Tulishatoa maelekezo ya kufanya uchunguzi wa kina kwanza kabla ya kukamata au kuhoji watuhumiwa. Hii ni kwa sababu hatutaki kukaa na kesi muda mrefu. Kabla ya kukamata, tunakuwa tumepata taarifa zote muhimu, ili haki itendeke kwa uhakika,” alisema Hamduni.

Makonda akiwa Mkuu wa Mkoa, yeye na mkewe walipigwa marufuku na Marekani, kuingia nchini humo wakimtuhumu kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kutishia uhai wa wananchi.

Taarifa ya Marekani ilieleza wangekuwa tayari kuthibitisha ukiukwaji huo mkubwa wa haki za binadamu alioufanya kama wangepewa fursa hiyo. Hata hivyo, hadi sasa Serikali haikupata kuzungumzia zuio hilo la Makonda.

Alichoandika Makonda

Wiki iliyopita katika ukurasa wake wa Instagram, Makonda aliandika maelezo marefu ya mkakati huo aliodai unaratibiwa na makundi matano yenye lengo la kuangamiza maisha yake.

Alitaja makundi hayo kuwa ni wauza dawa za kulevya, wanufaika na dawa za kulevya, wapenzi wa jinsia moja, wanaokesha usiku kucha kutafuta kulipa kisasi kwa wasaidizi wa Dk Magufuli na waliowahi kuwa sehemu yake.

“Nafahamu pia juu ya mbinu zinazoandaliwa, ili kuniua kwa faida ya familia zao na kutengeneza mashahidi wa uongo ili mnipe kesi ya uhujumu uchumi,” aliandika Makonda.

Katika andiko hilo, Makonda alisema: “Mambo mawili najiuliza. Pamoja na kazi zote nzuri nilizozifanya kwa chama changu (CCM), Serikali yangu na wananchi wa Dar es Salaam, haya ndiyo malipo yake?

“Mtu aliyejenga hospitali, aliyejenga ofisi za CCM, magari ya Polisi, ofisi za walimu, vituo vya Polisi, shule za sekondari mpaka na msingi, kutibu wagonjwa mpaka meli kuja Tanzania, kuhudumia makundi mpaka kuiunganisha Serikali na viongozi wa dini. Leo hii naonekana eti natakiwa kunyongwa,” alilalamika.

Akihitimisha andiko lake, Makonda alisema: “Pamoja na kwamba lipo kundi kwenye mitandao linalolipwa ili kuandaa Watanzania watakaponikamata ionekane ni sawa, hakika ipo siku walemavu, yatima, wajane na waliotamani watoto wao wasife kwa dawa za kulevya, sauti zao zitasikika. Ukiona maji yametulia, jua kina ni kirefu.”

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Bunge lalia msongamano wa mizigo bandari Dar es Salaam

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wanaokwamisha mradi Liganga na Mchuchuma kitanzani

Spread the love  NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, watu wanaokwamisha utekelezaji...

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

error: Content is protected !!