January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ushauri kutoka Rich Dad, Poor Dad

Waziri wa Fedha, Saada Mkuywa akifafanua jambo kuhusu bajeti

Spread the love

ROBERT T. Kiyosaki na mwenzake Sharon L. Lechter katika kitabu chao cha Rich Dad, Poor Dad wana ujumbe mzito kwa Watanzania.

Wanasema, “Kukua kwa deni la taifa kwa kiasi kikubwa kunatokana na viongozi wetu, wanasiasa na maofisa wa serikali wafanya maamuzi wakiwa ni wale ambao hawakusomea wala kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya fedha.”

Wachumi hao wanasema hata waliosoma, wanasiasa wengi ni waliohitimu masomo yasiyo na uhusiano na fedha. Baadhi wanajua kusoma na kuandika tu na wasomi wachache wa masuala ya fedha hutoa maamuzi ya kisiasa ili kufurahisha genge lao (chama chao) badala ya mwelekeo wa uchumi.

Ni kweli. Bajeti ya Fedha ya Serikali nchini huandaliwa na wataalamu lakini hupelekwa kujadiliwa na wabunge wasio na utaalamu ila ushabiki tu. Mbunge hufuata maelekezo ya chama katika upitishaji bajeti na siyo uelewa wake mpana juu ya kilichowasilishwa na serikali.

Wabunge hawa, ndio wakipewa fursa ya kuchangia bajeti husema “naunga mkono bajeti kwa asilimia 100” halafu anaanza kulalamika Jimbo lake kutengwa, kutotekelezewa maombi, kutopangiwa miradi ya maendeleo au miradi iliyopangwa kukosa fedha.

Hawa ndio wakiulizwa sasa fedha zitoke wapi hawawezi kuchangia kwani hawajui. Hawa ndio katikati ya mjadala wa Bajeti ya Fedha wanauliza njiwa anataga mayai mangapi.

Wabunge hawa vilaza ndio hukimbilia kumshambulia mwanasiasa makini au mbunge wa upinzani kwa mambo binafsi (kama vile kuwa na kimada).

Katikati ya mjadala wa bajeti, wabunge vilaza hukimbilia kubadili hoja eti katika uchaguzi ujao ‘nitamng’oa’ fulani jimboni kwake.

 

Hawa ndio, badala ya kutoa maoni ya kuboresha bajeti iliyopo wanajikita katika mambo mepesi ambayo kuyasema na kutoyasema hakuongezi wala kupunguza kitu.

Katika Bajeti ndiko Mbunge anapewa fursa ya kuhoji matumizi mabovu ya fedha au fedha iliyotumika bila kuidhinishwa na Bunge.

Kwa mfano, katika Bunge la Bajeti, Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe alihoji zilikotoka fedha kwa ajili ya mchakato wa Katiba wakati Bunge halikuidhinisha ni sahihi. Hakujibiwa.

Mwaka 2007 Mbunge wa Nzega (CCM) Lucas Seleli nusura aiangushe serikali bungeni alipohoji sababu za serikali kuanza kutumia fedha kabla ya kuidhinishwa na Bunge. Ilichukua zaidi ya wiki kwa serikali kutoa majibu tena ya uongo. Tangu siku hiyo alianza kufanyiwa mizengwe na hatimaye aliondolewa katika kinyang’anyiro cha ubunge nafasi yake ikachukuliwa na Dk. Hamis Kigwangala.

Tatizo la kila jambo kufanywa la kisiasa, Mbunge wa CCM akisema haungi mkono bajeti wenzake hukaa kimya, lakini mpinzani akisema haungi mkono CCM wote huzomea.

Hata katika Bunge Maalum la Katiba, wamejazwa watu ambao uwezo wao ni kusoma na kuandika tu. Baadhi yao hata kuandika ni shida. Kazi yao kubwa ni kusema hewala kama ahsante kwa kuingizwa, lakini hawana uwezo wa kutoa hoja kipi kiingizwe ndani ya katiba na kwa nini.

Tukumbuke, Kiyosaki na Lechter ambaye ana C.P.A wanasema, “Kukua kwa deni la taifa kwa kiasi kikubwa kunatokana na viongozi wetu, wanasiasa na maofisa wa serikali kufanya maamuzi wakiwa ni wale ambao hawakusomea wala kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya fedha.”

error: Content is protected !!