April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Usaliti Chadema watibua uchaguzi Meya

Mch. Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini

Spread the love

HOFU ya usaliti ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Iringa imekwaza kufanyika kwa uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo imetokana na Chadema kupendekeza utaratibu wa upigaji kura kwa kuweka alama zaidi ya vema kwenye karatasi ya kura. Uchaguzi huo ulitakiwa kufanyika jana tarehe 16 Oktoba 2019, umeahirishwa.

Chadema Iringa kwenye uchaguzi, iliweka utaratibu wa kuweka alama zaidi ya vema kutokana na hofu ya kusalitiwa na baadhi ya wapiga kura wake, wanaodaiwa kupokea ‘mlungula’ kutoka CCM.

Katika Halmashauri hiyo, idadi ya madiwani wa Chadema na wabunge wao ni 14 ambapo ni idadi sawa na wale wa CCM ambao ni 14.

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba, CCM imeweka mtego kwa baadhi ya wapiga kura wa Chadema, kwamba wakipata kuta hata moja kutoka upande wa pili (Chadema), itawawezesha kuwa na kura 15 huku Chadema wakibaki na kura 13 jambo litalowawezesha (CCM) kushinda uchaguzi huo.

Kumea kwa hofu hiyo, ndio kuliisukuma Chadema kuibua na mkakati wa kulinda kura kwa kuwataka wajumbe wake (wapiga kura), kuweka alama zaidi ya vema ili kuwatambua kama watasaliti kwa kuwapigia kura CCM ama kuharibu kura kwa kusudi.

Mjadala wa hoja ya Chadema ndio uliovuruga utaratibu wa uchaguzi na kusababisha Hamid Njovu, msimamizi wa uchaguzi katika halmashauri hiyo kuahirisha uchaguzi.

“Sasa naahirisha baraza hili mpaka wakati mwingine, wajumbe wote nawaomba mkasome sheria na kanuni za uchaguzi ili kukwepa kukiuka masharti,” amesema Njovu wakati akiahirisha uchaguzi huo.

Amesema, hawezi kuruhusu uchaguzi huo kufanyika kwa kuwa, madiwani ambao kisheria ndio wapigakura, waliibua mjadala kuhusu matumizi ya kanuni za upigaji kura.

“Kuna tatizo katika kuelewa kanuni,” amesema Njovu na kuongeza “manapaswa mkasome kanuni ili mzielewe vizuri.”

Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema amesema, wanataka kuwajua wasaliti kwenye uchaguzi huo na hivyo, wamependekeza namna ambayo itawawezesha kuwajua.

“Tulichokitaka sisi ni kwamba wasituwekee masharti ya namna ya mtu apige kura vipi,” amesema Mchungaji Msigwa na kuongeza “Sisi Chadema tulikubaliana wote tuweke alama itakayomuonesha kila mmoja wetu amepiga kura, ili tumjua atakayesaliti.”

Njovu ameahirisha uchaguzi huo bila kutaja tarehe ya kufanyika, baadhi ya wabunge wa CCM wamepongeza uamuzi wa kuahirisha uchaguzi huo huku wakisisitiza kura ni siri na kwamba itabaki hivyo.

error: Content is protected !!