August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Usafiri Mafia aibu tupu

Spread the love

MAZINGIRA ya usafirishaji abirika kupitia Bandari ya Nyamisati iliyopo Rufiji kwenda Mafia, ni aibu tupu, anaandika Faki Sosi.

Wananchi na watumiaji wa bandari hiyo wanateseka kwa muda mrefu na hata kueleza kutoona umuhimu wa Uhuru uliopatikana miaka 55 iliyopita.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, wananchi na watumiaji wa bandari hiyo  wameeleza kwamba, hawapo salama kutokana na mashaka tele yanayotokana na mazingira mabovu ya bandari hiyo.

Wananchi hao wamemweleza mwandishi wa habari hii alipokutana nao eneo la bandari hiyo juzi na kwamba, maisha yao yamewekwa reheni na serikali yao kutokana na kutojali usafiri ambao unatumiwa na wengi.

Mwajuma Ismail, mmoja wa wasafiri hao aliyekuwa bandarini hapo ameeleza kuwa, amefika hapo mchana na kwamba, anasubiri usafiri (boti) iliyotarajiwa kuondoka saa tisa usiku jambo ambalo linaonesha tatizo la safari kwenye kisiwa hicho.

Amesema kuwa, vyombo vinavyotumika kusafirishia abiria baharini ni duni na kwamba, boti hizo hazina usalama wakutosha kutokana na kutokuwa na jaketi za uokoaji .

“Ufike muda wowote lakini kuondoka ni usiku tena usiku wenye hatari, linapowafika jambo mkiwa baharini, ni vigumu kupata msaada kwa kuwa, muda huo wahusika wanakuwa wanakoroma,” amesema.

Mwajuma Shaha amesema kuwa, mtu akisafiri kwenda Mafia kupitia bandari hiyo, hulazimika kuweka kambi bandarini hapo (Nyamisati).

Na kwamba, eneo hilo si rafiki kwa usalama na afya za wasafiri kutokana na mbu wengi, baridi lakini pia hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali.

“Kwa kweli watu wa Mafia tunateseka katika usafiri kwa muda mrefu, kila siku tunasikia viongozi wa kisiasa wakileta porojo.

“Angalia jinsi hawa watoto wanavyoteseka (anawaonesha). Kwa kweli hii ni aibu, tangu tupate Uhuru hatujawahi kusafiri kwa raha,” amesema Shaha.

Mwananchi Mohammedi Omari amesema kuwa, watu wa Mafia wameshoshwa na majivuno ya wanasiasa majukwaani na kutofanya mambo kwa vitendo kwani jamii inateseka kwa muda mrefu katika usafari.

Ahamadi Mbonde, Diwani wa Kata ya Kilindoni Mafia amesema kuwa, ingawa yeye ni miongoni mwa watumiaji usafiri huo lakini hali si salama.

“Kwanza boti zinaondoka katika wakati mbaya yaani nyakati za usiku, mathalani  kumetokea ajali wakati huo ni ngumu kupata msaada,” amesema mbonde.

Shaibu Mnunduma, Mkuu wa Wilaya ya Mafia akizungumzwa na mwandishi amesema, eneo la Bandari ya Nyamisati linahusiana na Wilaya ya Rufiji.

Na kwamba, kutokana na watu wanaotumia bandari hiyo kuwa ni watu wa wilaya yake, alizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji ili kushughulikia matatizo hayo.

 

error: Content is protected !!