September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Urusi yashambulia hospitali tatu, Rais Ukraine alaani

Spread the love

VITA kati ya Ukraine ba Urusi imezidi kupamba moto baada ya ndege za Urusi kudaiwa kuzishambulia hospitali tatu usiku wa kuamkia leo tarehe 10 Machi, 2022.

Ndege hizo zimeshambulia hospitali zilizopo magharibi mwa mji mkuu, Kyiv na kwenye mji wa bandari wa Mariupol, huku juhudi za uokozi zikiendelea.

Mashambulizi hayo yamekuja kukiwa na matumaini ya kuwahamisha raia kutoka miji kadhaa iliyozingirwa, ukiwemo Mariupol, ambao hauna chakula, maji, wala umeme kwa siku kadhaa sasa.

Mji huo umezingirwa na majeshi ya Urusi kwa siku tisa sasa, huku maofisa wa mji wakisema kuwa wakazi wake 1,200 wameshauawa na wafanyakazi wa kujitolea wameanza kuzika maiti kwenye makaburi ya baada ya maeneo ya makaburi kujaa.

Mkuu wa mkoa wa Kyiv, Oleksiy Kuleba amesema kupitia televisheni kwamba jeshi la Urusi limeyageuza maisha kuwa jehanamu, ambapo watu wanajificha chini ya mahandaki mchana na usiku wakiwa hawana chakula, maji wala umeme.

Mji mwengine ulioshambuliwa vikali kwa mabomu ni Zhytomyr wenye wakaazi 260,000 na ulio magharibi mwa mji mkuu, Kyiv.

Meya wa mji huo, Serhii Sukholym amesema kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba hospitali mbili zimeshambuliwa, mojawapo ikiwa ya watoto.

Katika mji wa pili kwa ukubwa, Kharkiv, makombora ya Urusi yaliharibu makao makuu ya polisi, na kuwaua watu wanne na kuwajeruhi wengine 15.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa ofisi ya mwendesha mashitaka, Serhii Bolvinov, aliongeza kuwa tangu uvamizi kuanza wiki mbili zilizopita, wakazi 282 wa mji huo wameshauawa, sita kati yao wakiwa watoto wadogo.

Aidha, kufuatia mashambulizi, Rais wa Ukraine Volodymr Zelenskyy kupitia akaunti yake ya Twitter amelaani mashambulizi hayo na kuendelea kuomba msaada kwa mataifa ya magharibi.

Rais Zelenskyy aliyataka mataifa ya Magharibi kuzidisha vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi, baada ya mashambulizi ya anga dhidi ya hospitali ya wazazi kwenye mji wa Mariupol usiku wa kuamkia leo, ambapo watu 17 walijeruhiwa, wakiwemo wajawazito.

Kwa mara nyengine, Zelenskyy aliyataka mataifa ya Magharibi kuweka marufuku ya ndege kuruka kwenye anga la Ukraine, ombi ambalo wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO wamelikataa mara kadhaa kwa hofu kwamba hatua hiyo itasababisha vita vya moja kwa moja na Urusi, ambavyo wanavikwepa.

Kwa kushindikana hilo, Zelenskyy aliomba ndege zaidi za kivita kwa ajili ya nchi yake, pendekezo ambalo pia lilikataliwa na wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, hapo jana Jumaatano.

Awali, Poland ilisema ingelikabidhi ndege zake chapa MiG-29 kwa NATO kwa ajili ya kulisaidia jeshi la Ukraine, lakini msemaji wa Pentagon, John Kirby, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Waziri wa Ulinzi, Lloyd Austin alizungumza na mwenzake wa Poland na kumueleza kuwa hatua hiyo ni ya hatari na pia haitabadilisha chochote kwenye uwezo wa jeshi la anga la Ukraine.

error: Content is protected !!