IMEELEZWA kuwa Serikali ya Urusi imepanga upya uongozi wa operesheni zake za kivita nchini Ukraine na kumteua Jenerali mpya mwenye uzoefu wa mapambano ya kivita nchini Syria kusimamia vita hiyo ya Ukraine.
Kwa mujibu wa BBC mmoja wa maofisa wa Jeshi la Urusi amebainisha kuwa Kamanda wa wilaya ya kijeshi ya kusini mwa Urusi, Jenerali Alexander Dvornikov sasa ndiye anayeoongoza uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
“Kamanda huyo ana uzoefu mkubwa wa operesheni za Urusi nchini Syria. Kwa hiyo tunatarajia uongozi na udhibiti utaimarika,” kilisema chanzo hicho.
Uteuzi mpya ulifanyika katika jaribio la kuimarisha uratibu baina ya vikosi mbalimbali, kwani makundi ya Urusi yamekuwa yakipangwa na kuongozwa na wakuu tofauti, alisema afisa.
Urusi hadi sasa inahangaika kufikia malengo yake ya kivita, ikishindwa kuichukua miji muhimu kama vile Kyiv kabla ya hatimaye kuelekeza macho yake katika jimbo la Donbas mashariki.
Ofisa huyo alisema mbinu za Urusi zimekuwa zikiwafanya warudishwe nyuma na vikosi vyenye askari wachache wa Ukraine wanaopigana kwa akili zaidi na kwa kushtukiza-licha ya Urusi kufikiriwa kuwa na kikosi kikubwa chenye bataliani 100 zenye wanajeshi wenye ujuzi.
“Bila kubadili mbinu zake ni vigumu sana kwa Urusi kufanikiwa kwa malengo yao waliyojiwekea wenyewe,” alisema afisa huyo.
Leave a comment