RAIS wa Urusi, Vladimir Putin amempa uraia kachero na mhandisi wa zamani wa Marekani, Edward Snowden, ambaye tangu mwaka 2020 amekuwa mkaazi wa kudumu nchini Urusi.
Dikrii iliyotolewa jana tarehe 26 Septemba, 2022 na Rais Putin, iliwapa uraia wa Urusi raia 72 wa kigeni.
Licha ya kwamba haifahamiki iwapo Snowden ameukana uraia wake wa Marekani, kachero huyo aliyetuhumiwa kuvujisha siri za Taifa hilo, anatakiwa nchini Marekani kukabiliana na mashtaka ya ujasusi.
Mfanyakazi huyo wa zamani wa Shirika la Usalama la Marekani aliikimbia nchi hiyo baada ya kuvujisha nyaraka za programu za ujasusi mwaka 2013.
Alikuwa ameshafanyia kazi shirika hilo tangu mwaka 2009. Mwaka 2019, Snowden alisema alikuwa tayari kurejea Marekani ikiwa angelihakikishiwa kutendewa haki kwenye kesi dhidi yake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani, Ned Price, amesema msimamo wa Marekani juu ya Snowden haujabadilika.
Leave a comment