Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko URU wanyweshwa maji yenye matope, mradi uligharimu bilioni 2
Habari Mchanganyiko

URU wanyweshwa maji yenye matope, mradi uligharimu bilioni 2

Spread the love

OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imethibitisha kuwa Mradi wa Maji wa Mang’ana uliotekelezwa kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi wa vijiji vya Kata ya Uru Kaskazini katika Halmashauri ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, unatoa maji machafu yenye matope na yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

 

Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), Mhandisi Kija Limbe

Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 2.15, ulianza kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), mwezi Disemba 2016 na kumalizika Disemba 2018 kwa kutumia njia ya manunuzi ya “Force Account”.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya mwaka 2020/2021 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma jana tarehe 12 Aprili, 2022 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, imebainisha kuwa mabomba yaliyotumika katika mradi huo yalifukuliwa miradi ya enzi za ukoloni hivyo kushindwa kutatua shida ya maji wilayani humo.

Kutokana na hali hiyo Kichere amependekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) ihakikishe waliohusika wanachukuliwa hatua stahiki kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ya kuhakikisha kuwa mfumo wa kuchuja maji umejengwa.

“Pia Mamlaka ifanye usanifu na kujenga mfumo wa kuchuja matope (filtration system) kwenye Mradi wa Mang’ana na katika siku zijazo, Mamlaka izingatie usanifu bora wa mradi kulingana na mahitaji halisi ya miundombinu na eneo husika ili kuondokana na changamoto zinazotokana na usanifu duni,” amesema.

Aidha, akifafanua kwa kina kuhusu ukaguzi maalumu alioufanya kutokana na malalamiko ya wananchi wa Moshi kuhusu mradi huo, Kichere amesema mradi uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.15 bila kujumuisha gharama za mabomba ya chuma yaliyofukuliwa kutoka kwenye mifumo ya zamani ya maji ya Shiri na Nsere na kutumika kwenye mradi wa maji wa Mang’ana yaliyokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 441.

Amesema kutokana na mahojiano aliyoyafanya na baadhi ya watumishi wa MUWSA, alibaini maji yanayotoka kwenye Mradi wa Maji wa Mang’ana ni machafu hasa kipindi cha mvua.

“Vilevile, nilitembelea Mradi wa Mang’ana ambapo wananchi wa eneo hilo walikiri kuwa wakati wa mvua maji huwa machafu.

“Pia, vipimo vya ubora wa maji vilivyofanywa na Mamlaka vilionyesha kuwa, wakati wa mvua, maji katika Mradi wa Mang’ana huwa na kiwango kikubwa cha chembechembe za matope kwa kiwango cha NTU 8-8.17 (Nephelometric Turbidity Units) ambapo ni zaidi ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani cha NTU 5, na hivyo kuyafanya maji hayo yasiwe salama kwa matumizi ya binadamu,” amesema.

Amesema uchafu huo wa maji ulisababishwa na kutokuwekwa kwa mfumo wa chujio katika chanzo na bomba kuu.

Aidha, amesema mabomba yaliyotumika kwenye Mradi wa Mang’ana yalikuwa chakavu na yalifukuliwa kutoka kwenye mifumo ya maji ya zamani tangu ezi za ukoloni.

Waziri wa Maji, Juma Aweso

Amesema alipowahoji wafanyakazi wa MUWSA alibaini mabomba hayo ya chuma yenye kipenyo cha inchi 10 yalifukuliwa kutoka kwenye mifumo ya zamani ya maji ya Shiri na Nsere katika Manispaa ya Moshi.

“Katika mahojiano hayo, watumishi walishindwa kutaja hasa ni lini mifumo hiyo ya Shiri na Nsere ilifungwa japo walikadiria kuwa mifumo hiyo ilifungwa tangu enzi za ukoloni ikimaanisha kuwa mifumo hiyo ni ya zamani,” amesema.

Amesema alishindwa kubaini vigezo vilivyotumiwa na Mamlaka katika maamuzi ya kutumia mabomba hayo ya chuma ya zamani kwenye Mradi wa Mang’ana hasa ikizingatiwa kuwa ubora wa vifaa hupungua kulingana na muda unavyoongezeka.

“Kwa kuwa ubora wa mabomba ya chuma ya zamani haukuweza kuthibitishwa kabla ya kutumika, ni dhahiri kuwa kuendelea kutumika kwake kunabaki kuwa na mashaka, hali ambayo inaweza kuigharimu Mamlaka siku zijazo,” amesema.

Amsema kwa kuzingatia maelezo hayo, ni wazi kuwa tuhuma zilizowasilishwa na wananchi wa Wilaya ya Moshi kuwa mabomba yaliyotumika ni ya zamani yalikuwa ya kweli.

“Ninapendekeza MUWSA ifanye upimaji na tathmini ya kitalaamu kwenye mabomba ya chuma ya zamani yenye kipenyo cha inchi kumi yaliyotumika katika Mradi wa Maji wa Mang’ana ili kujua ubora wake na kujiridhisha kuhusu uendelevu wake.

“Pia MUWSA ihakikishe waliohusika wachukuliwe hatua stahiki kwa kushindwa kutimiza wajibu na majukumu yao ama kwa kuruhusu au kushauri kutumika kwa mabomba ya chuma ya zamani yaliyofukuliwa kutoka eneo lingine na kuwekwa kwenye mradi mpya bila kufanyiwa uchunguzi wa kitalaamu kuhusu ubora wake,” amesema.

Vibarua wakiwa na mafundi wa MUWSA mradi huo ulipokuwa unajengwa

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

error: Content is protected !!