December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Urasimu unavyokwamisha biashara ya magogo

Magogo yakiandaliwa tayari kwa kuuzwa

Spread the love

SHERIA kandamizi na urasimu katika nchi yoyote huwa kikwazo dhidi ya ukuaji wa uchumi kwa sababu mazingira hayo husababisha biashara halali kufanywa katika mazingira haramu, nje ya mfumo rasmi wa kisheria. Anaandika  Jimmy Mfuru … (endelea).

Hali hiyo imeikumba sekta ya biashara ya magogo na mbao hapa nchini Tanzania, ambapo biashara hii ni halali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kutokana na urasimu uliopo hapa nchini sasa wafanyabiashara wa magogo na mbao wanafikiria kuifanya kwa njia uharamu. Uharamu huu utaigharimu serikali kiuchumi.

Baada ya kuliona tatizo hilo, baadhi ya wafanyabiashara wa  mbao na magogo mkoani Lindi na Tanga ambao ni waadilifu wameiomba serikali kupunguza ukiritimba. Wanapinga utitiri wa kodi katika biashara hii. Wanataka kunusuru hali.

Wakifafanua ukubwa wa tatizo hili, wafanyabiashara hao wamesema kuwa, kwa sasa kuna vituo vingi vya ukaguzi barabarani ambavyo vimejenga mazingira ya watumishi wa serikali katika vituo hivyo kuomba rushwa.

Hivyo, wafanyabiashara hao wanasema kuwa kuna kila sababu ya kupunguza vizuizi hivyo ili kuondoa usumbufu kwao.

Hayo yalibainishwa  katika warsha ya wafanyabiashara wa mbao na magogo iliyofanyika katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na Wilaya za Mkinga na Korogwe mkoani Tanga kwa nyakati tofauti.

Warsha hizo zilishirikisha zaidi ya wafanyabiasha 40 kutoka mikoa hiyo, iliandaliwa na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) na Mfuko wa Dunia wa Kuhifadhi Mazingira (WWF) – Tanzania. 

Ally Kinunga, ambaye ni Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Mbao Lindi (UWAMBALI), akichangia katika warsha hiyo alisema, “kutokana na utitiri wa kodi katika kuvuna rasilimali za misitu, imekuwa kero na imewalazimu baadhi ya wafanyabiashara kuvuna kinyemela na kuikosesha serikali mapato.” 

Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo Kinunga amesema, serikali inapaswa kuweka viwango vyenye unafuu ili isiendelee kupoteza mapato.

Amesema kwamba, wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi kutokana na ugumu uliomo katika taratibu kupata leseni za uvunaji kutoka halmashauri na zile za Wizara ya Maliasili na Utalii. 

“Suala la kugongewa alama ya nyudo katika magogo (kuhalalisha), kazi inayofanywa na wilaya badala ya vijiji, imesababisha usumbufu na kuwakatisha tamaa ishara, ambao baadhi yao wameomba nyundo hizo zimilikiwe na vijiji ili kupunguza bughuda hiyo,” alisema Kinunga.

Na huko mkoani Tanga, Wilaya ya Korogwe, mfanyabiashara wa mbao Adamu Mussa amesema, suala hilo la biashara ya mbao liachwe kuingiliwa na wanasiasa.

Ametaka suala hilo libakie kwa wataalamu ili kupunguza adha katika zoezi la uvunaji na kuwalazimu kutoa rushwa hasa katika upatikanaji wa leseni na kugongewa nyudo ili hali na wajibu wa watendaji hao.

Kwa upande mwingine, wafanyabiashara wa mazao ya misitu wa Mkinga  na Korogwe, walisema kuwa kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo wanatamani kuachana biashara hiyo.

Wanasema wakilazimika kuendelea na biashara hiyo katika mazingira ya sasa, ni afadhali wafanye biashara isiyo halali, kwa maana ya kufanya biashara bila kukata kibali na kupitia njia za panya, kuliko kufanya biashara halali lakini wakajikuta wanapata hasara na usumbufu.

Mustafa Mfangavo ni Afisa Misitu Wilaya Kilwa mkoani Lindi. Amesema kuwa serikali inatakiwa kuwatendea haki wafanyabiashara hao na kuendelea kulinda serikali isikose mapato.

Amesema ili kunusuru hali hiyo jitihada za makusudi zinatakiwa kufanyika kuweka kiwango maalum kuliko  kuwepo na utitiri wa kodi unawakatisha tamaa. Ameongeza kuwa kiwango hicho kitawekwa wazi ili kuondoa mkanganyiko kwa  wafanyabiashara hao ili kuwepo na tija katika   ukusanyaji wa mapato.

Nae  Faustine Ninga-Mratibu wa Miradi ya Usimamizi kutoka TNRF alisema kuwa wadau hao ni sehemu ya utekelezaji mradi wa miaka mitatu wa 2014/17.

Alisema   washirika katika miradi ni  TNRF na WWF- Tanzania inayofadhiliwa na WWF-Finland na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland.

Ninga ameongeza kuwa, malengo mengine ya mafunzo ni kutoa elimu katika mambo ya uwekezaji katika misitu na ardhi nchini Tanzania na kuwafanya wananchi kufaidika na mazao ya misitu kupitia usimamizi shirikishi wa misitu.

Amesema, mafunzo hayo malengo makuu ni mbinu za kutatua migogoro inayohusu  uwekezaji katika misitu na ardhi hasa kuendesha mijadala na wadau mbalimbali na kutafuta mbinu bora za kuendesha mambo ya  uwekezaji.

Ninga katika majumuisho ya mkutano huo aliwashauri wafanyabiashara hao kuongeza thamani  ya mazao ili jamii zinazohusika na uvunaji  ziweze kuendeshwa kibiashara.

Amesema  ili waweze kufanikiwa na kuinua uchumi waungane na kujenga  viwanda vidogo  vidogo vya mbao kwa ajili ya uchakataji na hatimaye kuongeza thamani ya mazao ya mbao na magogo kuliko kuyauza yakiwa ghafi.

Mawasiliano: Mfuruj@yahoo.com 0717362692

error: Content is protected !!