October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Urais Z’Bar: Rais Magufuli, Dk. Shein watoa kauli nzito

Halmashauri Kuu ya Taifa NEC

Spread the love

UPIGAJI kura wa kumchagua mgombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 unaofanywa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Shughuli hiyo inafanyika leo Ijumaa tarehe 10 Julai 2020 makao makuu ya CCM jijini Dodoma huku Marais, John Pombe Magufuli wa Tanzania na Dk. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar wamesema, hawana mgombea waliomwandaa.

Majina matatu yamepitishwa kati ya 31 ambao ni; Dk. Khalid Salum Mohamed, Dk. Hussein Mwinyi na Shamsi Vuai Nahodha.

Kamati kuu ilipokea majina matano na kuyachakata na kupatikana matatu. Majina matano yalikuwa  ni;

  1. Dk. Hussein Mwinyi
  2. Profesa Makama Mbarawa
  3. Shamsi Vuai Nahodha
  4. Dk. Khalid Salum Muhamed
  5. Khamis Mussa Omar

Baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally kutangaza majina hayo matatu, Rais Magufuli alianza kuwaomba Profesa Mbarawa na Omar wazungumze kwa kifupi.

Profesa Mbarawa amesema, mchakato ulikuwa mkubwa na mwisho atakayepatikana atamuunga mkono kuhakikisha atakayeshinda anakwenda kushinda pia kwenye uchaguzi mkuu.

Pia, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Magufuli, “umenitoa mbali, umenifunza mengi. Katika maisha yangu umeandika historia kubwa name nikija kuandika historia yangu utakuwa mtu muhimu.”

“Safari hii haikuwa rahisi, tulikuwa wengi, tulipita kwenye milima na mabonde mengi, maneno mengi mazuri yalisemwa, mabaya yalisemwa lakini leo jahazi letu limefika bandarini na mmoja miongoni mwetu atapatikana,” amesema Profesa Mbarawa.

Naye Omar amekishukuru chama hicho kwa kuufanya mchakato huo kuwa huru na wa kidemokrasia na kuwatakia kila la kheri wajumbe wa mkutano huo ili wakamchague mmoja.

Kauli ya Rais Magufuli, Sheini

Akizungumza kabla ya upigaji kura kuanza, Rais Shein amesema waliwachuja wagombea 31 na kubaki na watano ambao waliwasilisha majina yao katika kikao cha kamati kuu kilichokutana jana Alhamisi jijini Dodoma.

Dk. Ali Mohamed Shein

Amesaema, waliwapima wagombea na yeye binafsi hakuwa na mgombea yoyote mfukoni kama maneno yalivyokuwa yanazungumzwa huko nje.

“Ni kazi ambayo tuliifanya kama binadamu, tunaupungufu lakini tuliifanya vizuri sana na tukiwa na akili na kufuata taratibu na kuwapata wagombea watano,” amesema.

“Tutashinda uchaguzi, wengi mnanijua, CCM ya jana siyo leo,” amesema Rais Shein na kuwataka wajumbe hao kuhakikisha wanamchagua mgombea makini bila kutumia maneno ya watu.

“Sijambeba mgombea na sitambemba, sijapata kufanya hivyo na sitafanya hivyo, kila mgombea au mwanachama anayofursa hiyo. Wapo wanaosema, Rais Magufuli wanamsema anambeba Profesa Mbarawa na mimi sitafanya hivyo, sijui kumbeba, sijafanya na sitofanya,” amesema Rais Shein.

Naye Rais Magufuli amesema, “Tumekuja kwa kazi hii, tuna wagombea watatu. Kikubwa tunapaswa kuzingatia, kuchagua hapa siyo tumemaliza kazi, tunakazi kubwa ya kwenda kushindana kule Zanzibar na vyama vingine.”

“Kila mmoja ajitafakari, anamchagua nani kati ya hawa watatu. Ushindi lazima uwepo na tunataka ushindi mkubwa na jukumu hili lipo kwenu,” amesema Rais Magufuli.

“Yawezekana mmejulishwa, mmepigiwa simu, angalieni dhamira yenu, hiki ni kikao kikubwa sana, kinakwenda kuamua mambo makubwa ya taifa hili, kinakwenda kuamua mambo makubwa ya taifa hili.”

“Rais Shein amefanya mambo makubwa sana, amenunua meli, zao la karafuu sasa ni kubwa, Shein anaheshimu demokrasia ya CCM na ndiyo maana anasema muda wake umefika mwisho,” amesema.

Rais Magufuli amesema, “kikao hiki, tunapokwenda kumchagua, dhamira yangu, huyu ninaye mchagua atakwenda kuyaendeleza bila ya kuhubiriwa, kuombwa ombwa, kila mmoja yuko huru.”

“Lakini Rais Shein amejieleza vizuri, katika kampeni hizi kila mmoja atapewa na wote watatu hawa wanafaa lakini yupo anayefaa zaidi na anayefaa zaidi ni jukumu lenu.”

Amesema, Hamisi na Profesa Mbarawa wameeleza vizuri. Nina hakika hata wale 31 wangeambiwa kuzungumza, wangezungumza vizuri.

“Wagombea wote 31, nawapongeza kuchukua fomu, lakini sasa atakayepatikana mmoja tumuunge mkono, wakati mwingine maneno yanapitishwa na upinzani na sisi tunayaunga mkono, tumchague mmoja. Nina matumaini mkubwa, kati ya hawa watatu atakuwa Rais wa Zanzibar,” amesema.

Kura zimekwisha kupigwa na uhesabuji wa kura unaendelea.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!