RAIS John Magufuli, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ameonya wanachama wa chama hicho waliojitokeza kuwania urais Zanzibar kutochafuana na kuhakikisha wanaheshimiana na kuzingatia taratibu za chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Amesema, kazi si moja ya urais pekee bali kuna nafasi zingine ndani ya Serikali za uteuzi hivyo si lazima kuanza kuchafuana ikiwemo kupitia mitandaoni.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo leo Jumanne tarehe 30 Juni 2020, wakati anazungumza na wanachama wa chama hicho na viongozi wa CCM waliojitokeza kushuhudia akirejesha fomu za kutetea nafasi ya urais makao makuu ya chama hicho Dodoma.
Hadi leo Jumanne saa 10 jioni, mgombea aliyejitokeza kuchukua fomu upande wa urais wa Tanzania ni yeye pekee huku Zanzibar wakiwa 32.
Hata hivyo, mgombea mmoja, Hussein Ibrahim Makungu amekwisha tangaza kujitoa.
Kati ya hao 31, kuna watoto wa marais wastaafu, viongozi walioko madarakani na wastaafu wanaowania nafasi ya kuingia Ikulu.
Rais Magufuli amesema amekuwa anafuatilia kinachoendelea Zanzibar na kubaini kuna baadhi wameanza kuchafuana mitandaoni.
“Nimeona hiyo dalili kwa wagombea huko Zanzibar, wengine wanatumia mitandao wanamsema mwenzao, wengine kwenye magazeti lakini atakayechaguliwa ni mmoja tu na Mungu wetu wa mbinguni anamfahamu,” amesema Rais Magufuli.
Mwenyekiti huyo wa CCM amesema “sisi tulikuwa 42 (watia nia kugombea urais wa Tanzania mwaka 2015). Kwa hiyo niwaombe sana hasa wagombea wa CCM Urais wa Zanzibar wakawe waangalifu katika kunadi sera zao. Wasiumizane tunawapa nafasi washindani wetu.”
Rais Magufuli amewataka wanachama 32 waliojitosa katika kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Ali Mohamed Shein, anayemaliza muda wake, kuacha kugombana, kwa kuwa kitendo hicho kitaleta mpasuko na kuvipa nguvu vyama vya siasa vya upinzani.

Amesema, kuna nafasi nyingi za kufanya si lazima urais na chama kitakaposhinda kunakuwa na nafasi Zanzibar na Tanzania hivyo umoja kwa wagombea urais, ubunge, uwakilishi au udiwani ndiyo mafanikio ya chama.
“Katika kipindi hiki cha kampeni, tusikitumie kama kipindi cha kuharibu CCM, sababu tutaenda kule tutaanza kubomoana. Wakati utakapofika wa uchaguzi kugombana na vyama vingine tutakuwa tumeshajiumiza. tukawe wavumilivu,” amesema Rais Magufuli
Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa rai kwa wanachama wa CCM watakaojitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani, kutanguliza maslahi ya chama hicho, badala ya kuweka tamaa ya madaraka mbele.

Rais Magufuli amewataka watia nia hao, kuvumiliana katika mchuano huo, huku akiwahimiza kuwaunga mkono wanachama wa CCM watakaofanikiwa kuteuliwa kugombea katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.
“Niwaombe kwenye majimbo maana nimeambiwa kuna majimbo yana watia nia 25, mtarogana bure, mtaumiza bure, atakayechaguliwa Mungu anamjua, niwaombe wanachama wa CCM kamwe tusivunje umoja wetu,” amesema
“Tukigombana sana wakati wa kampeni zitatupotezea mwelekeo, tuvumiliane, baada ya uchaguzi atakayechaguliwa tumbebe kwa nguvu zote,” amesema Rais Magufuli.
Waliojitokeza kuwania urais Zanzibar ni;
- Mbwana Bakari Juma
- Balozi Ali Abeid Karume
- Mbwana Yahya Mwinyi :
- Omar Sheha Mussa
- Dk. Hussein Ali Mwinyi
- Shamsi Vuai Nahodha
- Mohammed Jaffar Jumanne
- Mohammed Hijja Mohammed
- Issa Suleiman Nassor
- Profesa Makame Mabarawa
- Mwatum Mussa Sultan
- Haji Rashid Pandu
- Abdulhalim Mohammed Ali
- Jecha Salum Jecha
- Dk. Khalid Salum Mohammed
- Rashid Ali Juma
- Khamis Mussa Omar
- Mmanga Mjengo Mjawiri
- Hamad Yussuf Masauni
- Mohammed Aboud Mohammed
- Bakari Rashid Bakari
- Ayoub Mohammed Mahmoud
- Hashim Salum Hashim
- Hasna Atai Masound
- Fatma Kombo Masound
- Iddi Hamadi Iddi
- Pereira Ame Silima
- Shaame Simai Mcha
- Mussa Aboud Jumbe
- Mgeni Hassan Juma
- Maudline Cyrus Castico
Leave a comment