Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Urais Zanzibar si rahisi (3)
Makala & UchambuziTangulizi

Urais Zanzibar si rahisi (3)

Spread the love

ZANZIBAR katika maisha yake, imepigwa mapigo ya aina kwa aina. Imepigwa kwenye pande zote za kimaendeleo; pembe zote – Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi. Anaandika Jabir Idrisa … (endelea).

Ni mapigo yaliyotoa vishindo vikubwa kiasi cha kuiteteresha kila inapotaka kupiga hatua za kuyafikia matumaini ya watu wake.

Wazanzibari wanayo kumbukumbu mbaya na machungu hasa wanapofikiria namna nchi yao ilivopita katika vipindi vigumu katika maendeleo.

Nchi hii ya visiwa vikuu viwili vya Unguja na Pemba pamoja na vingine kadhaa vidogo zaidi vinavyokaa watu, imerudishwa nyuma kimaendeleo kwa kuzingatia historia yake.

Ilikuwa nchi ya mfano katika nchi za ulimwengu wa tatu zilizokuwa na maendeleo makubwa. Ilivyo na watu waliotulia akili na wenye maarifa na Wacha Mungu.

Watu wa mabara yote mengine likiwemo la Afrika ilimo, walifika Zanzibar na kuwa wakiitegemea kama sehemu ya wao kuendelea.

Historia ya maendeleo ya mwanadamu iliyoandamana na matembezi kwa njia mbalimbali, inaonesha kuwa kulikuwa na wasafiri wakati wa misimu ya biashara waliingia Zanzibar kwa harakati za biashara na utafiti.

Baadhi ya wengi ya wasafiri hao walifika Zanzibar kwa ajili ya kupeleka bidhaa za kuuza. Hawa walipokwishauza au wakati wakitafuta washtiri wa bidhaa zao, hapohapo kwa upande mwingine, wakipanga ni bidhaa gani za kuchukua ili kwenda kuziuza kule walikotoka.

Zanzibar ilikuwa lango kubwa au chimbuko maarufu la biashara kwa ukanda wa Mashariki mwa Bahari ya Hindi. Ikipokea bidhaa za aina kwa aina za chuma, fedha na shaba; bidhaa za nguo na chakula cha nafaka.

Ukiacha bidhaa za chakula, Zanzibar ikipata bidhaa mbalimbali zilizotumika kama malighafi ya kutengenezea bidhaa za viwandani.

Wakati huo yenyewe ilikuwa zaidi na viwanda vya mafuta ya nazi kutokana na asili yake ya kimaumbile ya kuwa nchi iliyojaaliwa hazina kubwa ya rutuba ya kuotesha minazi.

Baadaye ikapata karafuu, zao jingine mahsusi ambalo pamoja na nazi, ndiyo yaliibeba Zanzibar katika safari ya kuwa na uchumi mkubwa.

Zanzibar ilibahatika kuwa na ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo cha viungo. Aina mbalimbali za viungo kwa ajili ya matumizi ya kwenye mchanyato wa mapishi, mpaka sasa zinastawi kwa nguvu Zanzibar.

Asili yake ya kuwa nchi ya visiwa kwenye ukanda wa bahari, nayo ikawa na mpaka sasa inaibeba Zanzibar na kuwa nchi yenye akiba kubwa ya mazao mbalimbali ya samaki.

Lakini pia inazungukwa na fukwe nyingi ambazo maumbile yake yameifanya nchi ya kivutio kikubwa cha watalii. Mamia kwa mamia ya wageni kutoka mabara mengine wanafika kufanya ziara za matembezi Zanzibar.

Ni kwa sababu hiyo, kwa miaka kadhaa sasa, sekta ya utalii imeandaliwa na kujengewa mazingira ya kuwa chanzo kingine kikubwa cha mapato. Bali pia ni sehemu nyingine inayotoa ajira kwa watu wake.

Zanzibar nayo ikatumia fursa hiyo ya mbadilishano wa biashara, kujenga viwanda vidogo ikitumia malighafi kutoka nje kama vile ngozi, chuma, fedha na shaba.

Mpaka sasa Zanzibar inaendelea kutajika miongoni mwa nchi makao makuu ya mafundi wa vito vya samani – masonara. Hii ni biashara iliyowavuta wafanyabiashara wengi kutoka Asia.

Na hiyo ni sehemu muhimu ya kuifanya Zanzibar kuonekana leo kuwa nchi yenye mchanganyiko mkubwa wa watu wake. Na ni chimbuko la makabila yake mengi yanayoonekana.

Misafara ya majahazi ilikuwa imejenga mtandao au mfumo wa ukuzaji biashara kati ya Zanzibar na mabara mengine, hususan Asia na Ulaya.

Baadaye Zanzibar ilipata fursa ya kuwa nchi maarufu ambayo kwa kuwa na bandari nzuri kijiografia, ilitunga sheria mahsusi ya kusajili meli kimataifa.

Kwa muktadha huo, Zanzibar ilifanikiwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa hatua hiyo ya mafanikio, ikamudu kutandika mifumo imara ya kutolea huduma za kijamii kwa watu wake.

Na ni hapo Zanzibar iliingia katika kundi la nchi chache zilizokuwa na kiwango cha juu kabisa cha elimu. Ikifuatana na Misri, Ghana na Algeria.

Hiyo peke yake inathibitisha ukweli unaoishi mpaka leo kwamba Zanzibar imetoa wataalamu wengi wa fani nyingi za kimaendeleo ambao wametapakaa kwingi duniani.

Anayedhani Zanzibar ni kijinchi kidogo cha kudharauliwa maana kilivo cha watu milioni 1.5 tu, hakina watu mahiri kimaarifa kumiliki asilimia chache ya wataalamu, huyo amepotea kwa mbali. Yapasa ajue kuanzia leo kuwa Marekani, Ulaya, Asia, Australia na Afrika yenyewe ilipo, ina wataalamu wengi wa Kizanzibari.

Ni kwa sababu hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayo idara ya Diaspora katika muundo wake wa kiutumishi. Wataalamu hao kwa njia mbalimbali wamesaidia kuwepo mwamko wa wananchi wengine nao kujisikia watoke kwenda ughaibuni kutafuta maisha.

Sasa nchi yenye watu wa maarifa hayo, haiwezi kuchukuliwa kirahisi. Haiwezi kuwa nchi ya kubanwabanwa au kuwekewa vipingamizi vya kujipatia maendeleo.

Na kwa sababu hiyo hiyo, ni muhimu isemwe hapa kwamba Zanzibar haistahiki hata kidogo kuwa nchi ya kuburuzwa au kupangiwa au kuamuliwa mambo yake kwa namna yoyote ile.

Kwa hakika inahitaji kupumua na iachwe hasa ipumue. Inayo haki isiyopingika au kubishanika ya kutumia uhuru wake kupanga na kutekeleza mipango yake ya maendeleo. Lazima ishughulikie yenyewe mustakbali wake na watu wake.

Inakuaje nchi hii yenye sifa zote hizo na ambayo ilipata kiti katika Umoja wa Mataifa ijikute iliyokwama na kufungwa minyororo hadi kuwa iliyoganda kwenye tope la umasikini?

Si haki yake. Kule kuwa na watu wenye utulivu wa akili, wenye maarifa kifikra na watu wanaoipenda nchi yao, kunatosha kuifanya iwe na haki nyingine ya msingi ya kuachiwa iufaidi uhuru wake.

Zanzibar nayo inahaki ya kwenda inavotaka kwa mujibu wa matakwa ya watu wake na kulingana na utaratibu wa haki na kisheria uliowekwa na wenyewe Wazanzibari.

Wapo watu ndani yake wanaipenda Zanzibar kiuongo uongo. Sehemu kubwa ya maisha yao huitumia kupanga namna ya kuivuruga isistawi.

Wakikaa, wanajinasibu ni wazalendo wanaoitakia Zanzibar mema. Waongo na wazandiki. Ni chui walovaa ngozi ya kondoo. Hali ya Zanzibar na wake inawasuta.

Tatizo lao ni kwamba utekelezaji wa mipango yao ndio umekuwa na matokeo hayo ya kuizamisha nchi; ya kuigandisha kwenye tope la umasikini. Ni matokeo yaliyo wazi ambayo hayahitaji mwanafalsafa kuyaona.

Wazanzibari wenyewe wapo. Wenye moyo wapo. Tena wengi wa kutosha. Wanahaki ya kuchagua rafiki anayewafaa katika kupigania maendeleo yao. Wanajiamini na wako tayari kujituma ili kuijenga nchi yao kwa utashi wao.

Hili la kupewa uhuru wa kutumia au kufaidi uhuru wao, ni eneo ambalo Zanzibar imenyimwa kwa miaka mingi. Ni eneo ambalo Wazanzibari wamenyimwa wala si kwa hiyari yao.

Panahitajika meza kugeuzwa juu chini; sasa ikae vile wanavyoitaka watu wenyewe ili watumie fursa zilizomo ndani yao na ndani ya nchi yao kupata maendeleo ya kasi kama walivyo wa mataifa menzao.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Askofu Wolfang Rais mpya TEC, Padri Kitima aula tena

Spread the loveBARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetambulisha safu mpya za...

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari za SiasaTangulizi

Bashe apasua mtumbwi CCM

Spread the love  HUSSEIN Mohammed Bashe, waziri wa Kilimo, amekiweka pabaya Chama Cha...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Baba mzazi, mganga, paroko wadakwa mauaji ya mtoto mwenye ualbino

Spread the loveHATIMAYE Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa tisa wakiwa na viungo...

error: Content is protected !!