Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Urais Zanzibar si rahisi (2)  
Makala & Uchambuzi

Urais Zanzibar si rahisi (2)  

Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar (kushoto) walipokuwa katika mazungumzo ya muafaka na Maalim Seif Shariff Hamad
Spread the love

NDANI ya Baraza la Wawakilishi lililoanza mkutano wake wa kujadili na ikibidi kuidhinisha bajeti ya serikali ya mwaka mpya wa fedha unaoanza mwezi ujao, unamsikia mjumbe anamuombea Dk. Ali Mohamed Shein “uongozi wa kifalme.” Anaandika Jabir Idrissa…(endelea). 

Huyu mwakilishi wa wananchi anamsifia Dk. Shein kwa kiasi cha kuwa sawa na ua la waridi lisilopauka au kiongozi muadilifu wa aina yake na ambaye “ni peke yake kwa serikalini asiyevunja maadili ya uongozi na asotumia vibaya madaraka.”

Basi kwa umalaika wake huo, mwakilishi huyo mwenye nafasi adimu ya kuzungumzia shida za kimaendeleo na kimaisha za watu wa jimbo atokako, haoni aibu kusema “Dk. Shein apewe tena uongozi kwa muhula ujao.”

Lakini nje ya chombo hicho kilichoundwa mahsusi kuwa sehemu ya kuendesha serikali kwa kujali maoni na matakwa ya wananchi, Dk. Shein mwenyewe anaonya wanaosaka urais.

Urais wa Zanzibar ambao ni wa kiutendaji si wa sherehe tu, unajulikana ndio wadhifa wa juu mwisho Zanzibar. Ni wadhifa unaompa mpataji ukubwa kama wa utukufu vile. Rais wa Zanzibar ni nafasi kubwa, yenye hadhi na heshima ya aina yake.

Kwa sababu hiyo, zinaonekana jitihada za kuupa wadhifa huu hadhi zaidi; lakini sasa unajengewa mazingira ya kuchukuliwa ni wadhifa wa kawaida tu ambao mtu akiutaka “na achukuwe tu.”

Kwamba yule yeyote anayejisikia anautaka urais wa Zanzibar, hata pasina kujipima kama anao uwezo wa kuongoza, ana huruma kiasi gani kama kiongozi wakati wa shida; au anawajali vipi wananchi wanaounda nchi hii iitwayo Zanzibar, “basi na apewe tu.”

Kwa bahati mbaya, dhana hiyo ni fikra potofu mno, fikra mfu na kwa kweli ni fikra zisizostahili kuzingatiwa. Nichukuwe nafasi hii kuwaasa Wazanzibari wenzangu wamsamehe bure mwenzao yeyote anayedhani urais wa Zanzibar ni wadhifa wa mchezomchezo.

Wamsamehe mwananchi na binaadamu mwingine yeyote yule, awe ndani ya Zanzibar yenyewe, au katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; awe barani Afrika, Ulaya, Asia na Marekani, anayejipa imani kuwa hata zumbukuku (ulimwengu uko huku) aweza kuwa Rais wa Zanzibar.

Hapana. Hata kidogo. Haistahili kuchukuliwa kuwa ni wadhifa mdogo na rahisi tu namna hiyo. Zanzibar ni nchi si sawa na timu ya mpira au asasi ya kiraia inayoishi kwa uongozi wa mafaili mfukoni.

Urais wa Zanzibar ni wadhifa wa kutukuka kabisa ambao kwa yeyote anayeutaka au kufikiria anafaa, yampasa lazima atafakari mapema mara tu anapofikiria anautamani.

Huyu anayeutamani wadhifa wa urais wa Zanzibar shuruti ajue kwamba anataka kuwa kiongozi wa watu. Tena anataka kuwa kiongozi wa watu makini sio watu tu. Watu makini kwa hali zote.

Wazanzibari wanajua mahitaji yao na wanajua namna nchi yao ilivyo. Wanajua nchi yao imeruzukiwa mali na raslimali za kiasi gani na zina mchango gani kwa maendeleo ya Zanzibar yao na dunia. Wanajua.

Wazanzibari wanajua namna dunia inavokwenda. Wanajua vizuri kuwa yale yanayotokea huko yanaweza kuwa na mnasaba kwa maslahi yao katika nchi yao. Si watu wa kuishi wakizoea kuambiwa na viongozi serikalini kwamba “maisha ndivo yalivo kote huko duniani.”

Eti atoke mwenzao na kusema kwamba nchi nyenginezo huko watu wake pia hawana maisha mazuri kama tu walivyo wao ndani ya nchi yao. Huyo ajue hatastahamiliwa. Hajapata kuvumiliwa mtu kama huyo.

Zanzibar imebarikiwa mali na raslimali chekwa, zikiwemo zile ambazo ukitoka nje yake, hakuna utakokwenda ukazikuta. Ukizikuta basi hizo za huko zitakuwa za hadhi ya chini au za ubora usiotimia kiwango cha kimataifa.

Zanzibar ina rasilimali za asili sio za kuongezewa ladha (au chumvi au na rangi) kama inavotendeka kwengineko. Mfano mzuri ni karafuu. Hazishindiki duniani pamoja na utafiti mpana uliopata kufanywa ili kuzishushia hadhi yake.

Haitoshi kuwa mfano. Ni wapi utakuta nchi ya visiwa vilivyojaa watu watafutaji maisha kama Zanzibar? Ni wapi utakuta nchi kama Zanzibar, ya visiwa viwili vikubwa na vingine vidogo vinavyoishi watu, imejaa watu wenye akili zilizotulia katika kujua au kuelewa fani au stadi mbalimbali za kuwa chimbuko au njia za mipango yao ya maendeleo kama binaadamu.

Wazanzibari wanatumia vizuri mazingira ya nchi yao kujitafutia riziki lakini wale walioona ndani vipo vikwazo vya wao kujipatia maendeleo, wameondoka – na utaratibu huu wa enzi na dahari unaendelea mpaka sasa – na kutapakaa duniani kote kuhangaikia maisha.

Na yule anayedhani kuwa Wazanzibari kwa ujumla wao ni watu milioni 1.5 tu kama isemwavo, basi huyo naye ni muala ajipe muda wa kutosha wa kujifunza namna nzuri na bora zaidi ya kuijua khasa Zanzibar na watu wake.

Zanzibar ina watu mabara yote wanatafuta maisha. Tena ina watu wenye fani – achilia mbali maelfu ya wenye viwango vya kawaida vya kielimu – tangu fundi mchundo mpaka mainjinia na wanasayansi hata warusha ndege na wabunifu wa mifumo ya kiatomiki.

Ikiwa nchi yenye mandhari mazuri ya kitalii kwa kuwa na bahari kubwa iliyopambwa kwa fukwe mwanana za kumvutia yeyote anayebahatika kufika mara ya kwanza au kusimuliwa na aliyepata kufika, Zanzibar ipo kwenye eneo zuri kijiografia kiasi cha kuwavutia hata wenye roho mbaya.

Ilipo wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanasema ni eneo la kimkakati maalum kwa kuzalisha fursa ayami za kuijenga kiuchumi hata kufudhu kufananishwa na Singapore. Ndipo wale wenye akili kubwa wakazaa fikra ya kuigeuza iwe na hadhi ya kiuchumi ya kuitwa “Singapore ya Afrika.”

Hawa watu wenye roho mbaya wamekuwa tatizo kubwa kwa Zanzibar. Walijikuta wakitamka hadharani kuwa wangeweza wangeichomoa nchi hii na kuisokomeza (kama ni neno linalofaa) “huko mbali na mwambao huu wa Afrika Mashariki.”

Mpaka leo hawajahi kusema hadharani ni kwanini khasa walitamka hivo. Hata hivyo, walijua na wanajua hawana uwezo huo waliotamani. Ni hawa hiyo juzi, jana na mpaka sasa, wamebaki wachangiaji wakubwa wa mipango ya kuifisidi.

Kumbe wafanyeje wakati wanao watu wanaoshirikiana nao kujaribu kufikia malengo yao. Kwa hakika – maana hili ni suala la historia inayoendelea – hiyo kwao ndiyo njia rahisi au mbadala ya kuitumia ili kukidhi haja zao au kutimiza dhamira zao mbaya.

Hawa mola muumba anawaona. Watajitahidi kupanga mipango michafu ya kuihujumu na kuifisidi Zanzibar kiuchumi na hivyo kuisababishia madhara kisiasa, kijamii na kiutamaduni, lakini hawataimaliza yote – watashindwa tu.

Wataendelea hivyo kwa sababu bado wanaiona Zanzibar inazidi uzuri wake. Na vile wanavyoiona bado tu ingalipo na ingali na watu wanaojua wanachokitaka; wanaoijua dunia na wanaompenda na kumtii Mola aliyewaumba, yafaa wajiulize itawachukuwa miaka mingapi zaidi kuimaliza.

Zanzibar inaendelea kutajika tu duniani. Allah azidi kuikinga na waovu kwa kuwadamirisha wote wasioitakia neema.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Usiyoyajua ziara ya Rais Samia Korea Kusini

Spread the loveMWEI 31 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Local content’ inavyotajirisha Watanzania, wavuna mabilioni

Spread the loveUshirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za madini (Local Content) na...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyotumia teknolojia kuigeuza Geita kuwa ya kijani

Spread the loveSHUGHULI za uchimbaji madini hutakiwa kwenda sambamba na urejeshaji mazingira...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Rais wangu mama Samia; Wananchi wa Igoma watendewe haki

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wananchi wa eneo la Igoma Truck...

error: Content is protected !!