Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Urais wa Magufuli, wamponza Membe, hatarini kufukuzwa 
Habari za SiasaTangulizi

Urais wa Magufuli, wamponza Membe, hatarini kufukuzwa 

Spread the love
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeelekeza wanachama wake watatu, makatibu wastaafu, Yusuf Makamba na Abdulrahaman Kinana, kuhojiwa na kamati yake ya Ulinzi, Usalama  na Maadili. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Kinana na Makamba, wanapaswa kuhojiwa na kamati hiyo, kufuatia madai kuwa wamekidhalilisha chama hicho na kiongozi wake mkuu, Rais John Pombe Magufuli.

Mwanachama mwingine anayepaswa kuhojiwa na Kamati ya Maadili, ni aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Benard Membe.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Halmashauri Kuu ya taifa, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, imeeleza kuwa viongozi hao wandamizi, wataitwa mbele ya kamati hiyo, kujibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili.

Kuibuka kwa “sakata” hili kumekuja kufuatia kuvuja kwa mazungumzo yao kwa njia ya simu, wakimtuhumu Rais Magufuli, kumkumbatia mtu anayejiita, “mwanaharakati huru,” Cyprian Musiba.

Kinana na Makamba, walifika mbali zaidi, baada ya kuamua kuandika barua kwa Katibu wa Kamati ya Wazee ya chama hicho, Pius Msekwa, kulalamikia vitendo hivyo.

Naye Membe alikiri kudukuliwa sauti yake, ingawa yeye hakuwasilisha malalamiko yoyote kwa chama chake, badala yake aliamua kumfungulia mashitaka Musiba.

Taarifa ya chama hicho imesema: “NEC imepitisha na kuelekeza kwa kauli moja, wanachama hao waitwe na kamati ya usalama na maadili, ili wajibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili. Kwa mujibu wa katiba ya chama na kanuni ya maadili na uongozi.”

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, kuibuka kwa tuhuma hizi, kunamlenga moja kwa Membe.

Mwanadipromasia huyo mashuhuri nchini, amekuwa akitajwa kwa kasi katika siku za hivi karibuni, kufuatia madai kuwa amepanga kujitosa katika mbio za urais mwaka 2020 kupitia chama hicho.

Pamoja na kwamba Membe mwenyewe hajaweka wazi jambo hilo, lakini watu waliokaribu naye wanasema, “liwe jua au inyeshe mvua,” ni lazima atajitosa katika kinyanganyiro hicho.

Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanasema, ukimya wa Membe kuhusu urais wa 2020, ndiyo chanzo kikuu cha kushambuliwa kwake na makundi mbalimbali yanayojinasibu kuwa “watetezi wa Rais Magufuli.”

Katika hatua nyingine, NEC imeridhia msamaha uliotolewa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli, dhidi ya mbunge wa Bumbuli, January Makamba; mbunge wa Ntama, Nape Nnauye na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Polepole anasema, “NEC imepokea, kujadili na kuridhia kwa kauli moja taarifa ya Kamati ya Usalama na Maadili juu ya uamuzi wa mwenyekiti wetu, kuwasamehe wanachama walioomba radhi kwake.

“Baada ya kukiri mbele yake, kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma.”

Hata hivyo, baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM, wamejitokeza kuwapinga viongozi hao wandamizi kwa madai kuwa “ukitengeneza utaratibu, ujue utakugeukia.”

Miongoni mwa wanaotetea Musiba na kuwashambulia Kinana na Makamba, ni pamoja na Livistone Lusinde, mbunge wa Mtera; mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma; mbunge wa Nzega, Hussein Bashe; mbunge wa Simanjiro, James Millya na mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!