September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Urais Chadema: Kesi za Lissu si hoja

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeeleza kwamba hakitakwama kumpitisha Tundu Lissu kwa sababu ya kuhofia kesi zake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Na kwamba, iwapo kura zake zitatosha na Baraza Kuu litaona umuhimu wa kumpitisha Lissu kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, basi chama hicho kitasimama naye.

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara akizungumza jana tarehe 2 Agosti 2020 na gazeti moja nchini amesema, chama hicho kinatambua kwamba Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ana kesi kadhaa mahakamani.  

“Tunajua kuwa Lissu ana kesi kadhaa mahakamani, lakini zile ni tuhuma ambazo si kikwazo kwa yeye kugomea urais,” amesema Kigaila.

Amesisitiza kwamba, kesi za Lissu haziwezi kumzuia kupanda kwenye majukwaa na kuomba kura wananchi kwa kuwa, kesi hizo haziitishwi mahamani kila siku.

“Sio kila siku kuna kesi, siku ambazo atahitajika kwenda mahakamani atakwenda, siku ambazo hatohitajika ataendelea na kampeni zake.

“Kwa vyovyote vile inabidi hakimu au jaji aelewe kuna mtu anagombea urais au ubunge ikiwezekana kesi isimame ili akimaliza kampeni ziendelee,” amesema.

Tayari jina la Lissu limepenya katika hatua ya Kamati Kuu iliyoketi jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Mliman City. Majina mengine yaliyopenya kati ya matano ya awali ni Lazaro Nyalandu na Dk. Myrose Majinge.

Leo Baraza Kuu la Chadema linaendelea na vikao vyake ili kupitisha jina la mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Visiwani Zanzibar.

error: Content is protected !!