October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uraia wa Kibu: Zitto amtwisha zigo Majaliwa, Simbachawene

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT Wazalendo

Spread the love

 

SAKATA la uraia wa mchezaji mpya wa Simba ya Dar es Salam, Kibu Denis limemuibua Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuingilia kati kulimaliza. Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).

Mbali na Majaliwa, Zitto amewatupia mzigo Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene na Innocent Bashungwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wanaoweza kuhitimisha suala hilo.

Kibu aliyesajiliwa na Simba akitokea Mbeya City, amejikuta katika mgogoro kuhusu suala la uraia wake kwa hati yake ya kusafiria kushikiliwa na Idara ya Uhamiaji.

Mchezaji huyo, amewahi kuvaa jezi ya timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mchezo wa kirafiki kati ya Stars na Malawi, tarehe 13 Julai 2021, uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Stars kuibuka na ushindi wa 2-0.

Kwenye mchezo huo, Kibu anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alionesha kiwango kinachoridhisha na kuwezesha ushindi huo na baadaye akizungumza na waandishi wa habari alisema “nashukuru sana kwa mara ya kwanza kuichezea timu yangu ya Stars. Wazidi kunipa moyo kwani safari bado ndefu.”

MwanaHALISI Online limemtafuta Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Masele kuhusu sakata hilo alismea, wanaendelea kulifanyia kazi na “baadaye tutalitolea ufafanuzi.”

Alipoulizwa baadaye wiki, mwezi au mwaka, Masele amesema “…hapana, wiki ijayo.”

Tovuti ya Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara inaonesha, Kibu anayevaa jezi namba 38, alijiunga na Simba tarehe 18 Agosti 2021 na mzaliwa wa Mbeya.

Katika mahojiano maalum kati ya Zitto na MwanaHALISI Online yaliyofanyika ofsini kwake, Masaki mkoani Dar es Salaam leo Ijumaa tarehe 1 Oktoba 2021 amesema, suala hilo linapaswa kuhitimishwa ili Kibu ajue hatima yake.

Chibu Denis (kushoto) akiwa katika kikosi cha Taifa Stars. Kulia ni John Bocco

“…mpaka sasa hajaruhusiwa kucheza kwa kile kinachoitwa siyo raia wa Tanzania, lakini Kibu amechezea Mbeya City, amechezea timu ya Taifa kwa kiwango kikubwa sana, lakini amesajiliwa tu Simba haya ndiyo yameibuka,” amesema.

Zitto aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini amesema, wakati sakata hilo linatokeana kocha wa Taifa stars anamhitaji Kibu “Waziri wa michezo yupo, waziri wa mambo ya ndani yupo, kamishna wa uhamiaji yupo, waziri mkuu yupo na wote wako kimya.”

Amesema, mpaka sasa hakuna nchi yoyote ambayo imejitokeza kueleza kwamba Kibu ni raia wake.

“Kuna nchi zinanunua watu kuwa raia wao, sisi tunamchezaji mwenye kiwango anayehitaji kuitumikia Stars tunasema siyo raia. Haikupaswa hata kuwa mjadala. Mpeni uraia Kibu aweze kuiwakilisha nchi, msiiangalie Simba angalieni maslahi ya nchi,” amesema Zitto

error: Content is protected !!