Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Upya wa CCM na matendo ya kale  
Makala & Uchambuzi

Upya wa CCM na matendo ya kale  

Spread the love

UKIWAKUTA walevi wanasifiana unaweza ukashangaa ni jinsi gani wamehitimu katika sanaa ya kupeana ujiko. Ni kama mashindano ya nani anaweza kutoa sifa zaidi kwa mlevi mwingine. Anaandika M. M. Mwanakijiji … (endelea).

Na katika kujua wanavyojua kupeana sifa, walevi huja na nyimbo zenye kuburudisha klabu na kumfanya kila mmoja hata mpita njia ajisikie hamu ya kucheza.

Nyimbo zao zenye vibwagizo vifupi vifupi vyenye kurudia rudia maneno hadi yanakukaa mifupani huimbwa kwa sauti kali zikisindikizwa na shangwe.

Ukiwa ni timamu kati ya walevi wenye kusifiana namna hii, unaweza ukapata burudani ya kutosha na kukufanya kusahau matatizo yako kwa muda.

Nilikuwa naangalia matendo ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na nikirejea mkutano wake mkuu na jinsi ambavyo wanachama wa chama hicho wanavyoonesha furaha yao kwa serikali yao, nathibitisha kile ambacho nilikiandika miaka takribani mitano iliyopita, kwamba chama hiki “kimelewa ugimbi wa madaraka.”

Kwamba kwa kila kipimo na kwa haki kabisa, CCM na wanachama wake wako madarakani na zaidi ya kuwa madarakani, wameshikilia makreti yaliyojaa kilevi cha madaraka.

Lakini nani atawalaumu? Hakuna. Ni kwa sababu, hawawezi kuishi nje ya kuwa serikalini. Hawawezi.

Ukifuatilia yanayotendeka ndani ya serikali utaona mambo kadhaa nchini.

Kwanza, CCM haitambui kuwa kuna tatizo la ufisadi nchini na tatizo hilo ni kubwa. Pili, chama hiki hakina sera mahususi inayoeleweka ya kushughulikia na kumaliza ufisadi huo.

Ninafahamu kuna watu (wakiwemo viongozi wa juu wa CCM), ambao hawaamini kuwa ufisadi ni tishio kubwa zaidi la maendeleo, uhuru na utu wetu kuliko magonjwa, ujinga na umaskini.

Nafahamu kuwa wapo baadhi ya watu wanaweza kusema, serikali ya Rais Magufuli imeanza kupambana na ufisadi.

Lakini kwangu mimi, ninapozungumzia ufisadi nalenga mfumo unaotengenezwa, kulea, kudumisha na kuendeleza vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, undugunization, na kubebana katika kutawala pasipo kujali uwezo wa mtu.

Ufisadi kwangu mimi ni mfumo mbovu wa kutawala wenye kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma; kulimbikiza utajiri na njia za kupata utajiri mikononi mwa kikundi cha watu wachache  na utawala wenye misingi ya kuleta hofu kwa kile anayeonekana kuupinga.

Miongoni mwa haya yamejidhihirisha katika utawala huu wa sasa. Ndani ya kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais John Magufuli, kuna mabilioni ya shilingi yamepotea; na au hazijulikani matumizi yake.

Ndani ya miaka miwili kumeibuka madai ya matumizi mabaya ya madaraka. Kupeleka fedha maeneo nje ya maelekezo ya Bunge, CCM kufanyia vikao Ikulu. Mifano ni mingi.

Ndani ya miaka miwili, kumeibuka madai ya baadhi ya viongozi serikalini, kujilimbikizia utajiri kwa njia haramu. Haya hayajaweza kushughulikiwa vizuri na utawala uliyopo na zilizopita.

Ufisadi unatishia maisha yetu zaidi kwa sababu unaongeza gharama za maisha, unavujisha uchumi wetu na kutengeneza mfumo bandia wa kiuchumi ambao hauwezi kuelezeka kisayansi.

Jiulize kwa mfano, licha ya matumizi makubwa ya Dola za Kimarekani nchini, kwa nini bado mfumo wa bei uko chini? Jiulize inakuwaje fedha zitolewe toka sehemu moja ya uchumi na kupelekwa kwingine katikati ya bajeti na kusitokee matatizo yoyote yale ya kiuchumi.

Ufisadi unafanya watu waishi kwa kuingia gharama ambazo vinginevyo wasingeziingia. Mathalani, imefika mahali katika shughuli zetu za kila siku tunaanza kubajeti gharama za ufisadi katika kutafuta huduma na bidhaa mbalimbali.

Mtu anaenda kwenye ofisi fulani ya umma ambapo anajua kuwa anayotakiwa kulipa ni Sh. 15,000 (elfu kumi na tano), lakini inabidi aongeze na Sh. 5,000 juu yake ili apate huduma haraka.

Hii shilingi 5000 ya ziada ni “gharama ya ufisadi” ambayo mfumo wetu umeingiza akilini mwetu.  Huu ni mfano mdogo tu.

Nenda katika kutafuta ajira, bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ununuzi wa vitu mbalimbali au ajira, mwananchi analazimika kutumia fedha au kujuana kupata anachokitafuta. Vinginevyo, hakuna atakayekusikiliza.

Lakini zaidi ni katika kiwango cha juu cha utendaji. Miaka hii 17 ya utawala wa CCM tumeshuhudia jinsi gani kampuni kubwa ambazo zimekuwa makuwadi wa ufisadi yakijipenyeza katika shughuli mbalimbali ambazo zinaitwa “uwekezaji.”

Wengine tena kwa kuwafuata sisi wenyewe na kuwabembeleza. Kampuni hizi zingine zimeweza kuingia kwa namna ambayo zisingeweza kufanya kwenye nchi zao.

Lakini zaidi na la kutisha, ni jinsi kampuni hewa za kifisadi zilivyoundwa kuweza kuchota utajiri wetu.

Yote yametokea mbele na usoni mwa utawala wa Chama Cha Mapinduzi. Kampuni kama Tangold Limited, Meremeta, Deep Green, Richmond Development Company (RDC), Dowans Copration Limited na wizi katika akauti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).

Yote haya yameweza kusababisha upotevu wa zaidi ya shilingi trilioni 10. Kwa maneno yake mwenyewe aliyekuwa Rais wa Jamhuri, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwamba, serikali yake inapoteza asilimia 30 ya fedha za bajeti kila mwaka kwa mikono ya kifisadi.

Mpaka sasa, pamoja na kwamba serikali haijaeleza inapoteza kiasi gani kila mwaka, lakini hakuna shaka kuwa bado asilimia kubwa ya fedha zake, zinaangukikia kwenye ufisadi.

Nilitarajia CCM angalau wangeonesha kuwa wanatambua kuwapo kwa tatizo kubwa la ufisadi nchini.

Mungu awaonee huruma kwani hawalioni, hawataki kuliona na hata likiwakodolea macho kama bundi aliyekosa tawi mchana, bado hawana uwezo wa kuona na kisha wakatenda. Wataishia kwenye maigizo.

Hii ni kwa sababu, hawana uwezo wa kushughulikia ufisadi. Hawawezi kushughulikia ufisadi wala kuuondoa.

Hawawezi kuvunja mtandao mkubwa wa kihalifu (organized crime ring) ambao umejikita nchini na sasa unajihusisha na madawa ya kuleva ambapo vijana wetu wanaangamia kila kukicha, usafirishaji silaha haramu na uhamishaji wa fedha kwa njia haramu (money laundering).

Mtandao huu hauwezi kuhusisha watu wadogo isipokuwa wanasiasa, watumishi wa serikali. Mtandao huu umeweza kujipenyeza hadi kwenye chama chenyewe.

Labda hii ndiyo sababu CCM haiwezi kufanya vita dhidi ya ufisadi kuwa ni ajenda yake kuu ya kila mwaka.

Hawawezi kwa sababu hawatambui na hawana uwezo wa kutambua ufisadi ni sumu mbaya zaidi yenye kurudisha maendeleo nyuma kuliko tatizo jingine lolote.

Watajipitisha pitisha wakiahidi barabara, hospitali, shule na vyuo vingine vya kale. Vyote hivi ni geresha kwani tatizo kubwa zaidi na lenye kuhitaji ujasiri zaidi ni la ufisadi.

Wanaishia kuhubiri kuwa wanapambana na ufisadi, lakini papo hapo wanatumia mabilioni ya shilingi bila idhini ya Bunge.

Lakini hatuna budi kujiuliza watakapojikuta ndio wahusika wakuu, itakuwaje kama baadhi yao ndio wanufaika wakubwa wa mfumo wa utawala wa kifisadi?

Itakuwaje kuwa ni ufisadi ndio unawafanya wadumu madarakani? Itakuwaje kuwa ufisadi ukibomolewa na wao vile vile watazibuka kutoka katika ulevi wanaopeana kama kwa kupokezana kibuyu cha ulanzi?

Ndugu zangu, tuna uamuzi katika taifa hili. CCM wameshaamua kufanya vita dhidi ya ufisadi kuwa mchezo wa walevi. Wamechagua kulindana na kubebana, wamechagua kukumbatiana na kupepeana.

Huu ndio uamuzi wao. Ndio uamuzi wa taasisi zinazonufaika chama hiki na watu wake. Huu ni uamuzi wa wana CCM wote nchini. Ni uamuzi watu wasiozidi milioni nne.

Taifa hili linahitaji uongozi utakaochukua maamuzi sahihi na magumu zaidi. Yaani, maamuzi ya kupambana na kuuvunja vunja mfumo wa utawala wa kifisadi.

Tunahitaji viongozi ambao wako tayari kuwavua kinga ya uongozi, viongozi walioruhusu wizi wa rasilimali zetu na kuwatia pingu na kuwafikisha mahakamani na kuhakikisha kwa haraka sheria inafuata mkondo.

Uamuzi wa kuhakikisha kuwa wabadhirifu wa fedha za umma wanahukumiwa kunyongwa au kifungo cha miasha na adhabu ya chini inayoendana na kutaifishwa kwa mali za wanaokutwa na hatia ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 50 jela.

Ni vema wananchi wasidang’anyike na usanii wa CCM katika mapambano dhidi ya ufisadi. Suala la ufisadi – kama nilivyolieleza – siyo moja la matatizo ambayo chama hiki inaliona lipo nchini.

Hata hiki kinachoitwa, “mabadiliko ya kiuongozi” yanaoendelea ndani ya chama hicho, bado hayawezi kutoa nuru kuwa sasa CCM inajirekebisha.

Mabadiliko haya yataishia kuwafunua viongozi wake na kuwaonesha jinsi wasivyokuwa na maono na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu na kuthibitisha kuwa kwa kile kipimo siyo viongozi bora na hata siyo bora viongozi!

Ndio maana huwezi kusikia wapiganaji walioko CCM wakijadili kwa mapana mabadiliko yanayohubiriwa kuwa yanafanyika kwa kuwa siyo mabadiliko ya sera au katiba.

Hutasikia wanachama hao wakilalamika juu ya serikali yao kuuza uhondo wa Loliondo kwa wageni huku wakiwakana raia wao na kuwaita Wakenya!

Huwezi kusikia wakizungumzia matatizo ndani ya chama ila utaona kila mmoja anaelezea kuwa “CCM ni safi, ufisadi ni wa mtu mmoja mmoja.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!