KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeibuka na kero saba za Muungano kwamba, mpaka sasa bado zinatikisa. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Ratifa Chande, Mbunge wa Viti Maalum akiwasilisha taarifa ya kambi hiyo bungeni leo tarehe 16 Aprili 2019 anesema, licha ya maelezo ya masuala ya muungano kuelezwa vizuri katika Ibara ya (4)(3), bado kuna malalamiko.
Kambi hiyo imeeleza kwamba, zipo hoja ambazo kwa miaka yote zimekuwa zikilalamikiwa, lakini licha ya kuundwa tume kadhaa, malalamiko hayo bado hazijapatiwa ufumbuzi.
Kwenye taarifa yake Chande amezitaja kero hizo kwamba ni pamoja na; Mafuta na Gesi Asilia, Mambo ya Muungano, Ajira za Wazanzibari katika Taasisi za Muungano, Uwezo wa Zanzibar kukopa nje.
Pia Gawio la Zanzibar katika Mali za Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB), Mfuko wa Pamoja wa Fedha, Utozwaji Kodi mara mbili kwa Wafanyabiashara wa Zanzibar.
Chande ameeleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) peke yake ama kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano, zimechukua hatua kadhaa za kutafuta ufumbuzi wa kero za muungano.
Na kwamba, upande wa SMZ, miongoni mwa hatua ilizochukua na ambazo zinajulikana ni pamoja na kuunda kamati mbalimbali.
Amezitaja baadhi ya kamati zilizoundwa na SMZ kushughulikia kero za muungano kati ya mwaka 1990 na 2003 ni pamoja na;- Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992, Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamhuna, 1997), Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Kisanga (Kamati ya Salim Juma), Kamati ya Rais ya Kuandaa Mapendekezo ya SMZ juu ya Kero za Muungano, (Kamati ya Ramia, 2000).
Kamati zingine alizotoja ni Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLM) juu ya Sera ya Mambo ya Nje, Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano (2001).
Pia ametaja Kamati ya BLM ya Jamuiya ya Afrika Mashariki, Kamati ya Mafuta, Kamati ya Madeni baina ya SMZ na SMT, Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ), Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu, Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu – (1996 – 1999).
Pamoja na juhudi hizo amesema, SMZ imewahi kuajiri mtaalamu wa mambo ya fedha, Dk. Courtrey Blackman na mtaalam wa masuala ya mafuta katika kutafuta suluhu ya mambo hayo yanayoyumbisha muungano, lakini kamati zote hizo hazikuzaa matunda.
Amesema, kambi hio inaamini tatizo kubwa liko kwenye muundo wa muungano na kwamba, suluhu yake ni kubadilisha muundo ili muungano uimarike zaidi na kuwa wenye manufaa kwa pande zote washirika.
“Mheshimiwa Spika, Mbali na baadhi ya kamati hizo za SMZ peke yake, SMT na SMZ zimeunda Tume, Kamati na Kuajiri Wataalamu mbali mbali ili kutafuta suluhisho la Kero mbali mbali za Muungano.
“Miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni kama zifuatazo, Kamati ya Mtei, Tume ya Nyalali, Kamati ya Shellukindo, Kamati ya Bomani, Kamati ya Shellukindo 2, ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT,” amesema.
Na kwamba, kamati nyingine ni Kamati ya Harmonisation, Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila).
Hata hivyo, SMZ na SMT zimefanya vikao vya pamoja visivyopungua 80 katika ngazi mbalimbali ili kuzungumzia kero za muungano.
“Aidha, serikali hizi mbili mwaka 1994 ziliomba msaada wa IMF ili kuzishauri kuhusiana na Benki Kuu, mgawano wa misaada na uhusiano wa kifedha (intergovernmental fiscal relationship).
“Mbali ya juhudi zote hizo, tarehe 14 Novemba, 2000 wakati Rais Benjamin Mkapa alipokuwa akizundua Bunge, aliahidi kuzipatia ufumbuzi kero za muungano ndani ya siku 60!! Tokea ahadi ilipotolewa hadi leo ni ni miaka 19 imepita.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, serikali zinazoongoza ni ile ile ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kuchelewa huko kutatua kero hizo, kunaonesha dhahiri kwamba, Serikali ya CCM hazijatoa kipaumbele kwa muungano huu kuendelea kuwepo.
Leave a comment