Tuesday , 18 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Upinzani watinga Mahakama ya Afrika Mashariki, kupinga sheria vya Vyama vya Siasa
Habari za SiasaTangulizi

Upinzani watinga Mahakama ya Afrika Mashariki, kupinga sheria vya Vyama vya Siasa

Spread the love

UMOJA wa vyama nane vya upinzani nchini, vimefungua shauri la madai katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), jijini Arusha, kupinga sheria mpya ya vyama vya siasa nchini. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Katika shauri hilo, wadai wanaomba Mahakama kubatilisha vifungu 10 vilivyomo kwenye sheria hiyo.

Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 1, ilipitishwa na Bunge katika mkutano uliyopita na kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Pombe Magufuli, tarehe 13 Februari mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alisema, kesi iliyofunguliwa na wadau hao, tayari imesajiliwa mahakamani na kupewa Na. 3 ya mwaka 2019.

Mbowe amesema, wamelazimika kwenda mahakamani baada ya kujiridhisha kuwa sheria hiyo, inakiuka haki za binadamu; inapingana na Katiba ya Jamhuri na inaweka hata adhabu za jinai kwenye masuala ya kisiasa.

Amesema, “tumekwenda mahakamani kutokana na kuridhika kuwa mbali na sheria hiyo, kukiuka mkataba wa EAC, baadhi ya vifungu vyake, vinakiuka Katiba ya Jamhuri na misingi ya utawala bora, pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imerdhia.”

Kwa mfano, Mbowe ametaja kifungu cha 21 E, “kinachotoa mamlaka kwa Msajili wa vyama, kusimamisha uanachama wa chama cha siasa, mwanachama yeyote na kumzuia kufanya shughuli za kisiasa.”

Amesema, “huu ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba na ni mpango wa watawala kwenda kuwasimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya vyama kutogombea na jambo hili ni hatari kwa Amani na ustawi wa nchi.”

Bunge lilipitisha muswada huo wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa (2018), katikati ya msuguano mkali kati ya wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenister Mhagama.

Baadhi ya wadau waliofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, walipinga baadhi ya vifungu, kikiwamo kifungu kinachotoa kinga ya kutoshitakiwa kwa msajili huyo wa vyama vya siasa.

Akizungumzia uamuzi wa kufungua shauri hilo, Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro amesema, “kifungu hiki kikiachwa kama kilivyo, ndio utakuwa mwisho wa upinzani nchini.”

Alitoa mfano wa mamlaka ya Msajili wa Vyama ya kumuondoa au kumsimamisha uanachama mtu yeyote “akiwamo hata mgombea urais.”

Mkutano kati ya viongozi wa vyama hivyo na waandishi wa habari, ulifanyika makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Vyama vilivyoitisha mkutano huo na waandishi wa habari, mbali na Chadema, ni National Convention for Construction and Reform (NCCR- Mageuzi); United Democraty (DP), Chama cha Ukombozi wa UMMA (CHAUMA) na Chama Cha Kijamii (CCK).

Vyama vingine, ni ACT- Wazalendo, National League for Democracy, (NLD) na United Peoples Democratic Party (UPDP).

Washitakiwa kwenye shauri hilo, ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni mshitakiwa wa kwanza na Msajili wa vyama vya Siasa, ambaye ni mshitakiwa wa pili.

Walalamikaji katika shauri hilo, wanawakilishwa na Freeman Mbowe; Maalim Seif Shariff Hamad, Zitto Kabwe na Salum Mwalimu. Wanatetewa na jopo la mawakili wanne, wakiongozwa na Fatuma Karume, Mpale Mpoki na Jebra  Kambole.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mazingira magumu ya JPM yamechangia ‘Comedy Journalism’

Spread the loveMwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

RC Chalamila: Nimeacha ubabe

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chamalila amemthibishia...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia atoa ujumbe mzito Sikukuu Eid Al Adha

Spread the loveKATIKA kusherehekea Sikukuu ya Eid Al Adha, Rais wa Tanzania,...

BiasharaHabari za Siasa

Dk. Biteko aipongeza NMB kwa kuanzisha utoaji wa bima ya mifugo

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!