KAMBI Rasmi ya Upinzania Bungeni imelalamikia juhudi za serikali katika kuboresha elimu kwamba, bado ni finyu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Kambi hiyo imeleeza kuwa, mitaala ya elimu inalalamikiwa kutokana na kubadilishwa mara kwa mara bila kushirikisha wadau.
Suzan Lyimo, Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknologia akiwasilisha hotuba ya kambi rasm ya upinzania kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya kwa mwaka wa fedha 2019/20 amesema, bado kuna tatizo katika uboreshaji elimu.
“Mitaala yetu imekuwa ikilalamikiwa sana, na tunapoongelea mitaala ni pamoja na vitabu – ndiyo maana Taasisi ya Elimu Tanzania; jukumu lake ni kutayarisha vitabu vya kiada na mitaala.
“Mitaala yetu imekuwa ikibadilishwa mara kwa mara bila kuwashirikisha walimu ambao ndio wadau wakubwa. Mitaala yetu haiangalii maarifa (competency) na pia haitoi ujuzi ili mwanafunzi aweze kuendeleza vipaji vyake. Mtaala umekuwa zaidi wa kuwakaririsha wanafunzi,” amesema.
Na kwamba, kutokana na mazingira walimu wamekuwa hawavutiwi kufundisha jambo ambalo linaendelea kuzoretesha elimu.
“Sambamba na kukosa ujuzi na mbinu za kufundisha, bado walimu wengi hawavutiwi na kazi ya kufundisha jambo ambalo linawafanya kutofundisha kwa bidii na hivyo kupelekea kushuka kwa ubora wa elimu.
“Utafiti ulifanywa na HakiElimu 2016 ulibaini kwamba, ni asilimia 37.8 tu ya walimu ndio waliokuwa wanaipenda kazi yao ya ualimu,’ amesema.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa, hii ina maana kwamba, zaidi ya asilimia 60 ya walimu hawaipendi kazi hiyo; na kwa maana hiyo, hawaifanyi kwa ufanisi.
“Changamoto zote hizi zimepelekea kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya kuhitimu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitachoka kuishauri serikali kuwa na mikakati mahsusi ya kuboresha mitaala.
“Pia kuwashirikisha walimu ambao ndio wafundishaji pamoja na kuwapatia mafunzo ili waweze kufundisha mitaala hiyo kwa weledi na hivyo kupandisha viwango vya ubora wa elimu nchini,” ameeleza Lyimo.
Hata hivyo, upinzani umelalamikia kushuka kwa idadi ya walimu jambo linalochangia kudumaa kwa elimu nchini.
“Kwa mujibu wa takwimu za BEST za mwaka 2016 na 2017; idadi ya walimu kwa shule za msingi imeshuka kutoka walimu 191,772 mwaka 2016 hadi kufikia 179,291 mwaka 2017 ikiwa ni anguko la asilimia 6.5 na kufanya uwiano wa mwalimu na wanafunzi kuwa 1:50,” ameeza Lymo.
Leave a comment