Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Upinzani wajibu vijembe vya Serikali
Habari za SiasaTangulizi

Upinzani wajibu vijembe vya Serikali

Mbunge wa Malinndi, Unguja, Ally Salehe
Spread the love

MBUNGE wa Malindi, kisiwani Unguja, Ally Salehe, ameituhumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kupunja mapato ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), yanayopitia Mfuko Mkuu wa Hazina. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, leo Jumatatu wakati wa kuchangia bajeti kuu ya Serikali, mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari amesema, “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, haijawahi kupewa hata shilingi kutoka kwenye akaunti ya pamoja ya fedha za Muungano.”

Anasema, kwa mujibu wa Katiba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, imepewa mamlaka ya kutunza akaunti maalum ya pamoja inayoundwa na serikali mbili – Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – ambayo itakuwa sehemu ya mfuko mkuu wa hazina.

Amesema, kwa mujibu wa katiba hiyo, fedha zote za serikalizitakazochangwa na serikali zote mbili, zitagawanwa kwa jinsi watakavyokubaliana.

Mbunge huyo amesema, “hakuna fedha yeyote itayotumiwa katika kabla ya Tume ya Pamoja ya Fedha kuchambua mapato na matumizi ya shughuli za Muungano na kutoa mapendekezo yake kwa vyombo vinavyohusika juu ya mgawanyo wa matumizi hayo.”

Amesema, “Katiba inaelekeza kuwa Serikali ya Zanzibar, ni sharti iyakubali mapendekezo hayo na mgawanyo wake.

Salehe ameonya kuwa kutokana na vitendo vya Serikali ya Muungano kuikandamiza Zanzibar, “Muungano uliyopo unaendelea kuchukiwa na wananchi, hata kama Muungano huo, utaendelea kuwapo.”

“Tangu mwaka 1977, Zanzibar haijwahi kupewa mgawo wake wa fedha kutoka Akaunti ya Pamoja zinazotokana na mambo ya Muungano. Hii maana yake ni kwamba, mgawo wa fedha za Zanzibar umekuwa ukitumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya Tanzania Bara, ambayo haimo katika mambo ya Muungano.

“Kwa miaka 42, kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kinyume na Katiba ya Zanzibar, pamoja na serikali zote mbili kutambua uwepo wa Akaunti ya Pamoja na utaratibu wa namna ya kuchangia, upo mkanganyiko kwenye uwiano wa mgawo wa fedha zilizopo kwenye akaunti hiyo,” ameeleza.

Anasema, Salehe amesema, “Katiba zote mbili ziko kimya kuhusu uwiano wa mgawo wa fedha hizo, jambo ambalo linatoa shaka kuwa pengine kuna serikali, miongoni mwa serikali hizo, na hasa ile ya Zanzibar, haipati mgawo wake kama inavyotakiwa.”

Amesema, hata fedha zinazopatikana kupitia mikopo na  misaada ya kibajeti kwa Jamhuri ya Muungano, ni miongoni mwa mambo ya Muungano. Akaitaka Serikali ya Muungano, kupeleka fedha inazopokea, ikiwamo mikopo na misaada ya kibajeti kwa Zanzibar.

Akiongea kwa uchungu, mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari na mwanasheria amesema, Ibara za 133 na 134 za Katiba ya Muungano, inaeleza kuwa fedha za namna hiyo zinatakiwa kuwekwa kwenye akaunti ya pamoja, ili zigawiwe kwa Serikali zote mbili kwa ajili ya utekelezaji wa mambo ya Muungano kupitia Tume ya Pamoja ya Fedha.

Ameongeza: “Lakini tangu mwaka 1977, Zanzibar haijawahi kupata mgawo wake wa fedha kutoka kwenye Akaunti ya Pamoja. Na kwa kuwa kwa miaka 42 iliyopita hakuna mradi wowote wa kielelezo ambao ni miongoni mwa mambo ya Muungano uliowahi kutekelezwa Zanziabar; na kwa kuwa deni la Serikali ya Muungano linaihusu pia Serikali ya Zanzibar; na kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haiwezi kukopa nje peke yake, tunaomba Zanzibar ipewe mgawo wake, haraka iwezekanavyo.”

Naye David Silinde, akiwasilisha bajeti mbadala ya upinzani bungeni amesema, uchambuzi uliofanywa na kambi hiyo, umebaini kuwa bajeti iliyowasilishwa na serikali imejikita kwenye maendeleo ya vitu na sio maendeleo ya watu.

Akatoa mfano wa Sh. 33.104 trilioni zilizotengwa, ni kiasi cha Sh. 12.5 trilioni pekee, zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo.

Hata hivyo, mchanganuo wa bajeti ya maendeleo unajumuisha fedha za ndani kiasi cha  Sh. 9.74 trilioni na fedha za nje kiasi ni Sh. 2.51 trilioni.

Alitaja mgawo wa fedha hizo, kuwa Sh. 2.48 trilioni (sawa na asilimia 20.245) ya bajeti yote ya maendeleo ni kwa ajili ya Mradi wa Ujenzi wa Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR); Sh. 1.44 trilioni (sawa na asiliia 11.755 ya bajeti yote ya maendeleo), ni kwa ajili ya Mradi wa Kufua Umeme katika  mto Rufiji 9 ( Stiegler’s Gorge Hydoro Power Project) na

Sh. 500 bilioni (sawa na asilimia 4.081 ya bajeti yote ya maendeleo), ni kwa ajili ya kumalizia malipo kwa ajili ya ununuzi wa Ndege za Serikali.

Amesema, “miradi hiyo mitatu, imechukua Sh. 4.42 trilioni, ambayo ni sawa na asilimia 36.081 ya fedha zote za maendeleo. Hii miradi ipo kwenye wizara mbili tu, wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano pamoja na wizara ya Nishati.

“Pamoja na miradi hiyo michache kuchukua sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo; bado miradi hiyo haina faida za moja kwa moja katika uchumi wa nchi yetu na wake. Hii inatokana na ukweli kwamba malighafi inayotumika kujenga SGR (Chuma na Cement) karibu zote zinatoka nje ya nchi na hivyo fedha zinaondoka katika mzunguko wa ndani na kupelekwa nje kwa ajili ya ununuzi wa malighafi hizo.

“Hata ajira zinazozalishwa, haziingizi chochote kwenye bajeti yetu kama kodi ya mshahara (PAYE) kwa kuwa wengi walioajiriwa katika mradi huo, ni vibarua (casual laborers) ambao hawapo kwenye mfumo wa kodi. Kwa maneno mengine, hii ni miradi ambayo inanyonya uchumi wetu kwa kutoa fedha ndani na kuzipeleka nje; lakini pili haina multiplier effect katika kuchechemua sekta nyingine za kiuchumi kama vile biashara na ajira.”

Amesema, kutokana na bajeti hii kuweka kipaumbele katika maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu; sekta nyingine zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja zimepata mgawo mdogo sana wa fedha za maendeleo jambo linaloashiria kwamba Serikali hii haina mpango na maendeleo na ustawi wa watu.

 Amesema, miradi na sekta ambazo Serikali inasema ndiyo vipaumbele vyake, nayo imepata mgawo mdogo jambo ambalo linaleta mkanganyiko kuhusu vipaumbele vya Serikali.

Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ndiyo kipaumbele cha kwanza katika bajeti ya Serikali, imetengewa Sh. 51. 5 bilioni. Anasema, kiasi hicho cha fedha, ni sawa na asilimia 0.42 tu ya bajeti nzima ya maendeleo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Wazanzibar watarajia makubwa kutoka NMB Pesa Akaunti

Spread the loveWateja wapya wa Benki ya NMB wa Zanzibar wanatarajia neema...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kinana aungana na Tale kugawa mitungi ya gesi 800

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda amjibu Mwenyekiti UWT, “wananipa nguvu ya kuwapiga spana”

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemshukia Mwenyekiti wa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Madeni ya bilioni 219 yalipwa, wadai wengine waitwa

Spread the loveSERIKALI imesema kuanzia Mei mwaka 2021 hadi sasa imelipa madai...

error: Content is protected !!