KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, imekosoa marekebisho yanayokusudiwa kufanywa katika Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, Sura ya 3 kuwa haina tija kwa Taifa na unawalenga watu fulani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Hayo yamesemwa leo Jumatano tarehe 10 Juni 2020 na Msemaji MKuu wa Kambi hiyo katika Wizara ya Katiba na Sheria, Salome Makamba wakati akiwasilisha maoni juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2020.
Katika muswada huo uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi ukipendekeza kufanyika marekebisho ya sheria 13.
Profesa Kilangi amesema, Muswada unalenga kufanya marekebisho katika Kifungu cha 4 ili kuweka masharti yatakayotaka mtu yoyote anayekusudia kufungua shauri lolote la kikatiba chini ya Ibara za 12-29 zinazohusu haki za msingi kuidhihirishia mahakama ni kwa kiasi gani mlalamikaji ameathiriwa na ukiukwaji wa haki anayolalamikia.
Amesema, marekebisho katika kifungu hiko yanapendekeza mashauri yote ya madai dhidi ya viongozi wakuu wa nchi yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Lengo la marekebisho haya ni kukidhi maudhui ya dhana ya kinga ya mashtaka dhidi ya viongozi hao.
Hata hivyo, upinzani kupitia kwa Makamba umepinga marekebisho hayo akisema, “Ni muhimu Bunge hili tukufu liweze kutofautisha kati ya uvunjifu wa Ibara ya Katiba na uvunjifu wa haki za msingi za Kikatiba.”
“Uvunjifu wa ibara ya Katiba unaweza kupingwa na kila mtu kwa kuwa unahusu ulinzi wa Katiba na uvunjifu wa haki za msingi unaweza kupinganiwa na mtu ambaye haki zake za msingi zimekiukwa,” amesema
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Chadema amesema, “mabadiliko ya vifungu hivyo yanakiuka ibara za 26(2) ambayo inasema ‘kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sharia za nchi” sasa kwa kuwa Katiba haisemi mtu huyo lazima awe ameathirika na jambo hilo.”
“Ikiwa Bunge hili tukufu litapitisha mabadiliko ya vifungu hivyo, ni dhahiri kwamba vifungu hivyo vya sharia vitakuwa batili kwa kukinzana na Katiba, kwa sababu Kifungu cha 4(2) kinachopendekezwa kipo kinyume na Katiba na kinakinzana na Ibara za 26(2),” amesema
Makamba amesema, kila kiongozi wa umma anapoingia madarakani anaapa kuilinda Katiba pamoja na sharia.
“Kiujumla, marekebisho haya yanapoka uhuru wa wananchi kufungua mashauri ya Katiba, mashauri yanayohusu haki za binadamu na hivyo kufunga milango ya mahakama kwa wananchi kudai haki zao za msingi,” amesema
Makamba amesema, marekebisho hayo yanapendekeza madai dhidi ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Jaji Mkuu na Naibu Spika yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Marekebisho haya ni kinyume na msingi ya mgawanyo wa mamlaka baina ya mihimili mbalimbali katika nchi lakini tayari kuna maamuzi mbalimbali ya Mahakama ambayo yameshaamua kuwa Rais pamoja na viongozi wengine nao wanaweza kushtakiwa ikiwa watavunja Katiba,” amesema
Akisisitiza, Makamba amesema, “ni muhimu kwa wadaiwa kuhusishwa wao wenyewe na si kutenda makosa halafu akashtakiwa mtu mwingine ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”
“Pia, kwa kuweka kipingele hiki, inaondoa dhana nzima ya uwajibikaji na kiapo cha mhusika aliyeapa lazima awajibike kwa matendo yake,” ameongeza.
Leave a comment