August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Upinzani: Serikali inanyima jeshi fedha

Spread the love

SERIKALI imeweka rekodi mbaya ya kutoa fedha chini ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge kwa miradi ya maendeleo katika wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na katika mafungu mengine fedha hazikutolewa kabisa katika mwaka wa fedha 2015/16, anaandika Pendo Omary.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni na Juma Hamad Omar, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Omar amesema kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Bunge liliidhinisha jumla ya Sh. 220.14 Bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2016 fedha iliyokuwa imeshatolewa na hazina ilikuwa ni Sh. 40 Bilioni sawa na asilimia 18 tu ya bajeti iliyoidhinishwa.

“Kitendo cha kutotekelezwa kikamilifu kimewaathiri sana wananchi. Kwa mfano mradi mmojawapo ulikuwa ni upimaji na ulipaji wa fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na jeshi. Mradi huu ulitengewa takribani Sh. 7.4 Bilioni, lakini fedha iliyotolewa hadi kufikia Machi, 2016 ni Sh. 277.1 Milioni sawa na asilimia 3.7 tu ya bajeti iliyoidhinishwa,” amesema Omar.

Aidha, Omar amesema “jambo la ajabu kabisa kuwahi kutokea ni kitendo cha kutopeleka fedha yoyote kutekeleza miradi ya maendeleo katika fungu 38 (Ngome). Fungu hili lilitengewa jumla ya Sh. 8 Bilioni lakini hadi kufikia Machi 2016, hakuna hata senti moja iliyotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wowote wa maendeleo uliopangwa.”

Ameitaja miradi ilipasawa kutekelezwa kuwa ni ujenzi wa uwanja wa ndege Tanga, utafiti na ulinzi wa anga, ujenzi wa maghala ya mlipuko, ukarabati wa zana za ulinzi wa anga na ujenzi wa gati.

“Kitendo cha Serikali kutotekeleza bajeti ya maendeleo ya wizara hii, sio tu kunalifedhehesha Jeshi letu, lakini pia kinawaweka wananchi katika hali ya hatari kubwa,” amesema Omar.

Ametolea mfano matukio ya milipuko ya silaha katika maghala ya silaha za milipuko Mbagala na Gongo la Mboto – Dar es Salaam, yalivyosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa makazi ya wananchi.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali iliahidi kujenga na kukarabati maghala hayo ili kudhibiti ajali za milipuko.  Lakini Bunge liliidhinisha bajeti lakini Serikali haikutekeleza.

“Safari hii, katika fedha za maendeleo  Serikali inaomba kuidhinishiwa Sh. 10 Bilioni katika fungu 38 (Ngome) na Sh. 8 Bilioni katika fungu 39 (JKT). Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji; kuna haja gani ya bunge kuidhinisha fedha hizi ikiwa fedha zilizoidhinishwa mwaka wa fedha 2015/16 hazikutumika kabisa?, amehoji Omar.

error: Content is protected !!