August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Upigaji kura TLS wakamilika

Tundu Lissu akiwa na mke wake, wakipiga kura zao katika uchaguzi wa TLS jijini Arusha

Spread the love

HAKUNA marefu yasiyo na ncha. Hatimaye vuta nikuvute ya uchaguzi wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), imehitimishwa leo asubuhi kwa mawakili kupiga kura kuchagua viongozi wao, anaandika Charles William.

Ingawa kuna nafasi nyingi zinazowaniwa, lakini mvutano mkubwa zaidi ni katika nafasi ya Urais wa TLS ambapo wagombea ni wanne akiwemo Tundu Lissu, Godwin Mwapongo, Francis Stolla na Victoria Mandari.

Hapo awali wagombea wa urais walikuwa watano, lakini Lawrance Masha aliyekuwa miongoni mwa wagombea hao alitangaza kujitoa katika uchaguzi huo siku ya jana katika ukumbi wa AICC.

“Natangaza kujitoa ktika nafasi niliyokuwa nagombea, na naomba wote mliokuwa mkiniunga mkono, mpige kura zenu kwa Tundu Lissu,” alisema Masha jana usiku.

Jana usiku, wagombea wote walipewa nafasi ya kujinadi na kuulizwa maswali huku zoezi la kupiga kura likifanyika leo asubuhi.

Akizungumza kwa njia ya simu na MwanaHALISI Online, Peter Kibatala mbaye ni wakili na wakala wa mgombea Tundu Lissu amesema tayari zoezi la kupiga kura limemalizika saa tano kamili asubuhi.

“Hapa ninavyozungumza na wewe tayari zoezi la kupiga kura limemalizika, kwahiyo tunaingia ndani kwenda kuhesabu kura,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu muda ambao matokeo yatatangazwa amejibu, “Siwezi kujua, tume ya uchaguzi ndiyo inayotangaza matokeo baada ya kumalizika kwa zoezi la kuhesabu kura kumalizika. Vuteni subira kidogo.”

Mawakili 6,000 walitarajiwa kupiga kura leo asubuhi ili kuwachagua viongozi wao katika nafasi za urais, makamu wa Rais, ujumbe wa Baraza la TLS na zinginezo. Viongozi hao watakiongoza chama hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja.

error: Content is protected !!