December 4, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Upelelezi wakwamisha kesi ya madiwani wa Loliondo

Nyundo ya Hakimu

Spread the love

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imeahirisha kesi ya mauaji inayowakabili baadhi ya viongozi wa Loliondo, mkoani Arusha, hadi tarehe 11 Oktoba 2022, kutokana na upelelezi kutokamilika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Kesi hiyo namba 11 ya 2022, imeahirishwa na mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Herieth Mhenga,baada ya upande wa Jamhuri kuomba iahirishwe kwasababu upelelezi wake haujakamilika.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi waliutaka upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka ili hatma ya kesi hiyo ijulikane, kwani nusu ya washtakiwa wake ni viongozi wa Serikali.

Wamesema kukwama kwa kesi hiyo,  kunawakosesha wananchi wao kupata haki ya kuongozwa pamoja na kuwakilishwa kwenye miradi ya maendeleo, kwa kuwa viongozi wao wako  mahabusu.

Pia, mawakili wa utetezi waliomba upande wa Jamhuri ukamilishe upelelezi huo haraka, kwani baadhi ya washtakiwa wana matatizo ya kiafya.

Hakimu Mhenga, aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 11 Oktoba 2022, ambapo washtakiwa wamerudishwa mahabusu katika Gereza la Kisongo, jijini Arusha.

Kesi hiyo ina washtakiwa 25, akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Ngorongoro, Ndirango Olesenge Laizer; Diwani wa Kata ya Piyaya, Simon Orosokiria; Diwani viti maalum, Kijoolu Kakeya.

Wengine ni, Diwani wa Ololosokwani, Moloimet Yohana; Diwani wa Malambo, Joel Lessonu; Diwani viti maalum, Talengo Leshoko; Diwani wa Oloirien, Shengena Killel; Diwani wa Arash, Mathew Eliakimu na Diwani wa Maaloni, Damiani Laiza.

Washtakiwa hao waliwekwa mahabusu tangu tarehe 16 Juni 2022, wakikabiliwa na mashtaka mawili, la kwanza wanatuhumiwa  kupanga njama ya kuua maofisa wa Serikali na polisi , watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka katika pori tengefu la Loliondo.

Shtaka la pili ni la mauaji ya askari polisi mwenye namba G 4200, Koplo Garlus Mwita, wanalodaiwa kulitenda tarehe 10 Juni mwaka huu, maeneo ya Ololosokwan, wilayani Ngorongoro.

error: Content is protected !!