July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Upasuaji wa aina yake, upandikizwaji kichwa

Dk. Sergio Canavero akiwa na uhakika wa kufanikisha upandikizaji kichwa

Spread the love

HUENDA kwa mara ya kwanza tangu Dunia iumbwe historia ya kupandikiza kichwa (head anastomosis), itaandikwa miaka miwili ijayo 2017.

Upasuaji huo utakaofanya na madaktari na wauguzi 150 utagharimu dola za kimarekani milioni 15 sawa na fedha za kitanzania bilioni 30.

Ndoto hii inatokana na wazo la Dk. Sergio Canavero wa Italia atakayefanya upasuaji huo kwa Valeri Spiridonov (30), mwenye ugonjwa wa kusinyaa kwa misuli (Werdnig-Hoffman disorder), ugonjwa uliomsababishia ulemavu na kumuweka kwenye hatari ya kupoteza maisha.

Baada Dk. Canavero kuja na wazo hili kwa miezi kadhaa, alialikwa kwenye mkutano wa madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa fahamu na mifupa huko Indianapolis, Marekani wiki iliyopita.

Dk. Canevaro alihudhuria mkutano huo akiwa na Spiridinov, mgonjwa wake kutoka nchini Urusi aliyeamua kujitoa mhanga kukatwa kichwa chake na kupandikizwa kwenye mwili mwingine.

Kabla Spiridonov hajasafiri aliviambia vyombo vya habari kuwa anaamini kuwa atasaidia kusambaza wazo hili kwenye sekta ya upasuaji na hatimaye kuweza kushawishi madaktari wengine kuhudhuria kongamano hilo na alipoulizwa atawaelezaje watu watakaomwambia asithubutu kujitoa kafara kufanyiwa operesheni hiyo alijibu “wanapaswa wajiweke katika hali yangu ya ugonjwa”.

“Tunapaswa tufanye mambo ambayo hayajawahi kufanywa na mtu yeyote, binadamu wa kwanza kwenda mwezini alikuwa na hofu, ni dhahiri hata mimi ninaogopa hata hivyo ninatambua ni lazima ifanyike, kwani tusipojaribu hatutafanikiwa”, anasema

Hata hivyo pamoja na wazo la Dk. Canavero la upasuaji huo wa aina yake ambao haujawahi kufanyika hakuweza kutoa ufafanuzi jinsi gani atashiriki kufanikisha hilo. Lakini aliweza kusema kwenye kongamano hilo wakati anatoa mada kwa saa tatu kuwa jukumu lake kubwa ni kushughulikia uunganishaji wa uti wa mgongo.

Jinsi upasuaji huo utakavyofanyika

Upasuaji huo umebatizwa na kuitwa ‘HEAVEN’ (head anastomosis venture), utafanyika kwa kutumia vifaa vya kisasa kabisa, mfano kisu cha upasuaji kinachoitwa ‘nano-blade’, chenye unene mdogo sana unene ambao unaweza usikione kwa macho ya kawaida.

Aidha,udogo wa kisu hicho utapunguza uharibifu wa mishipa ya fahamu, mishipa ya damu na viungo vingine, lakini itawezesha kupunguza ukubwa wa jeraha na hivyo kuweza kupona kirahisi na kwa haraka.

Upasuaji huo utawahusisha watu wawili Valeri Spinodov mwenye kichwa kizima na chenye akili timamu, tatizo lake ni mwili unaosinyaa wa pili ubongo wake hauna uhai hata hivyo mwili wake una afya mzuri na utatolewa na kuunganishwa na kichwa Spinodov.

Ukataji wa vichwa hivyo utafanyika kwa wakati mmoja na baada ya ukataji wa kichwa cha aliyejitolea mwili wake utaunganishwa na kichwa cha Spiridinov.

Dk. Canavero anasema watatumia gundi iitwao ‘polyethylene glycol (PEG)’ ili kuunganisha uti wa mgongo, uunganishaji utakaosaidiwa na kichocheo cha umeme, kitakacholeta hisia kwenye uti wa mgongo.

Uunganishaji utafanyika pamoja na uunganishaji wa mishipa ya damu na mishipa ya fahamu, kwa kutumia bomba maalumu ili kuunganisha pande mbili.

Baada ya hapo mgonjwa atapewa dawa ya usingizi na atakuwa kwenye usingizi mzito kwa muda wa wiki tatu mpaka nne.

Baada ya muda huo inategemewa mgonjwa atakuwa na uwezo wa kuanza kuongea kama kawaida, na sauti yake haitabadilika inakisiwa mgonjwa ataweza kuanza kutembea baada ya mwaka mmoja akisaidiwa na wataalamu wa mazoezi ya viungo.

Upasuaji huu utafanyika kwa miili kuwekwa katika hali ya ubaridi kati ya nyuzi 10-15 (hypothermic conditions),ili kuweza kuongeza uhai wa seli bila ya hewa ya oksijeni kabla ya kuunganishwa na kuruhusu damu ianze kuzunguka.

Ukosoaji wa mpango huo

Mpango huu umekosolewa na wanasayansi ikiwa ni pamoja na madaktari waliobobea kwenye taaluma ya upasuaji wa mfumo wa fahamu.

Wengi hawajaonyesha utayari wa kukubaliana na upandikizaji huu kwa kuita ni ndoto kwani haiwezekani kisayansi na kimaadili.

Dk. Raymond Dieter, aliyehudhuria kongamano hilo anapata wasiwasi na haimwingii akili na anasema upandikizaji wa kichwa hauwezekani, huku akihoji ni namna gani mzunguko wa damu utaanza tena kufanya kazi na ni jinsi gani ubongo utaanza kufanya kazi kwani ubongo unakufa endapo umekosa damu kwa dakika tano tu.

Profesa Eduardo Rodriguez ambae ni bingwa wa upandikizaji wa viungo nje ya mwili (plastic surgery), huko New York aliyewahi kufanya upandikizaji wa uso kamili kwa mara ya kwanza mwaka 2012.

Anasema pamoja na utafiti wa kutosha unaohusu ajali na matibabu ya uti wa mgongo, bado hamna matibabu yanayoweza kuunganisha uti wa mgongo.Profesa Rodriguez anamalizia kwa kusema kwa vile hamna wanasayansi waliogundua jinsi ya kuunganisha uti wa mgongo, hamna jinsi ambavyo upasuaji huo unaweza kufanikiwa.

Pengine matumaini ya hali ya juu ya Canavero na ‘kufikiria nje ya boksi’ kwa maana kuwa na mtazamo na mawazo nje ya uelewa wa kawaida inasemekana itaweza kusaidia kushawishi madaktari kujiunga katika operesheni hii hatari.

Historia ya Upandikizaji Kichwa

  • 1908-USA: Dk Charles Guthrie-aliunganisha kichwa cha Mbwa
  • 1950-Urusi: Dk. Vladimir Demikhov – aliunganisha kichwa cha mbwa kwenye mbwa mwingine na kufanya vichwa viwili-alidumu kwa siku 29
  • 1970-USA: Profesa Robert J. White aliunganisha kichwa cha Tumbili aliyeweza kunusa, kuona, na kusikia, alikufa baada ya siku 9.

Historia ya upandikizaji wa viungo vingine

  • 2012 – USA: Profesa Eduardo Rodriguez – Upandikizaji wa uso mzima kwa mara ya kwanza anaendelea vizuri.
  • 1905 – Australia: Daktati Eduard Konrad Zirm – Upandikizaji wa sehemu ya jicho la mbele (Konea) uliofanikiwa
  • 1967- Afrika ya Kusini: Daktari Christiaan Neethling Barnard-Upandikizaji wa kwanza wa Moyo , mgonjwa alidumu kwa siku 18
  • 1998 – Ufaransa: Daktari Warren C. Breidenbach III na wenzake – Upandikizaji wa Mkono, mpandikizwa alikaa nao kwa miaka 3, baadae akaomba uondolewe

Valeri Spiridonov ni nani

Spiridonov ni Mhandisi wa usanifu na programu za Kompyuta, huko Urusi, anayetengeneza programu za kompyuta zinazohusu elimu na watoto.

Kwa mujibu wa tovuti ya motherboard, Spiridonov hajawahi kutembea tangu alipokuwa mtoto wa mwaka mmoja, Spiridonov amasema kuwa hakumbuki kama aliwahi kutembea.

Spiridonov kila siku analazimika kuamka saa 9 alfajiri na huwa anasaidiwa na jirani yake kutoka kitandani, huku mama yake akimsaidia kupika na kazi nyingine. Spiridonov huwa hapendi sana kuangalia TV bali muda mwingi anapoteza muda wake kwa kufanya kazi kwenye kompyuta.

Dk. Sergio Canavero ni nani

Canavero kutoka Italia, ni daktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa fahamu na amefanya ugunduzi wa tiba mbalimbali za mfumo wa fahamu na moja ya weledi wake ni ugunduzi wa jinsi ambavyo maumivu yanayosababishwa na mfumo wa fahamu yanavyotokea (genesis of central pain syndrome), ugunduzi huu ulimpatia tuzo inayoitwa “benefactor of mankind” kwa kujali na kuwa na huruma kwa wagonjwa wanaoteseka kutokana na maumivu.

Canavero ni bingwa mwandamizi anayeongoza kwenye taaluma ya mfumo wa umeme na kemikali zinazosafirisha taarifa kwenye mfumo wa fahamu (electrical & chemical neuromodulation).

Mwaka 2007 aliwahi kutambuliwa kama mtu mwenye akili za hali ya juu kabisa, mbunifu na mwenye uwezo zaidi ya uwezo wa binaadamu wa kawaida kwa nchi ya Italia “Italian genius of the first order”. Licha ya ugunduzi, ameandika vitabu kadhaa katika taaluma yake.

Ndoto ya upandikizaji aliipata wakati ana umri wa miaka 15, aliposoma gazeti lililoandika kuhusu Dk. Robert White , bingwa wa upasuaji wa Marekani, ambaye mwaka 1970 alipandikiza kichwa cha Tumbili kwenye mwili wa Tumbili mwingine.

error: Content is protected !!