July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Unyonyeshaji duni tishio kwa vifo vya watoto wachanga

Mama akimnyonyesha mwanaye

Spread the love

DUNIA ikiwa inaadhimisha wiki ya unyonyeshaji, nchini Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa vifo vya watoto wachanga bado vinashika kasi sababu ikitajwa ni kuchelewa kunyonyeshwa na wakati mwingine kutonyonyeshwa inavyostahili. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea). 

Hayo yamebainishwa na Afisa lishe mwandamizi wa Taasisi ya chakula na lishe Tanzania (Wizara ya afya), Neema Joshua wakati akitoa mada katika semina ya wanahabari kuhusu maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama Duniani. 

Akifafanua zaidi Afisa huyo mwandamizi wa Lishe, alisema kuwa nchini Tanzania hutokea vifo 25 kwa kila watoto wachanga 1,000 waliozaliwa wakiwa hai.

“Bado kuna changamoto ya kutofikia malengo ya kuokoa vifo vya watoto. Vifo vya watoto bado vipo juu sana ambapo takwimu zinaonyesha kuwa hutokea vifo 25 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai,” alisema na kuongeza kuwa;

“Tunaweza kuinusuru hali hii na kuokoa uhai wa watoto hawa kwa kuwanyonyesha maziwa ya mama kwa wakati na kufuata kanuni za afya.”

Pamoja na hayo Neema alisema taratibu zisizofaa za unyonyeshaji huathiri afya na maendeleo ya uhai wa watoto.

“Takribani nusu ya magonjwa ya kuhara na theruthi moja ya magonjwa ya njia ya hewa yanaweza kuzuilika kwa kunyonyesha watoto maziwa ya mama,” alisema.

Kwa upande wake Mratibu wa Lishe ya mama, mtoto na vijana balehe (Wizara ya afya), Tufingene Malambugi alisema kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama hupunguza utapiamlo kwa watoto.

Hata hivyo aliongeza kuwa ikiwa jamii itaelewa manufaa ya unyonyeshaji hakutakuwa na watoto wenye udumavu wa akili wala kimwili.

Akitoa takwimu za unyonyeshaji Tufingene alisema kwa sasa asilimia 31 ya watoto  walio chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa ukilinganisha na asilimia 34 ya mwaka 2015.

“Lazima tukubaliane kuwa mtoto anapaswa kunyonya kwa miezi sita mfululizo bila nyongeza ya chakula chochote ili kumpa vitutubisho anavyostahili mtoto,” alisistiza Tufingene.

Hata hivyo Mratibu huyo wa lishe alitanabaisha kuwa wazazi wote yaani baba na mama wana umuhimu mkubwa katika kufanikisha unyonyeshaji sahihi wa maziwa ya mama.

“Wazazi kwa pamoja wanapaswa kiweka mazingira ratiki yanayowezesha kufanikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama,” alisema.

error: Content is protected !!