FRANCIS Mgasa, Katibu Mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria hapa nchini (CHAKUA), ametoa siku saba kwa mamlaka zinazohusika na usafiri kuhakikisha unyanyasaji wa wanafunzi katika vyombo vya usafiri kote nchini unakoma, anaandika Charles William.
Mgasa amesema kuwa makubaliano kati yao na madereva pamoja na makondakta ni kuhakikisha wanatoa huduma kwa usawa bila kuangalia makundi ya watu na hivyo wanafunzi wanapokalia viti katika daladala hawatakiwi kusumbuliwa.
“Madereva na makondakta wamekuwa wanyanyasaji wa wanafunzi, kwanini wanawasimamisha? tumekubaliana bei ya nauli kwa wanafunzi iwe 200/= sasa naagiza wasisumbuliwe kwani hatujakubaliana wasikalie viti kwasababu nauli yao ni ndogo,” amesema.
Katika hatua nyingine Mgasa amewalaumu Wakala wa Usafiri wa Haraka (UDART) kwa usimamizi mbovu ikiwemo matatizo mengi katika vituo vya mabasi ya mwendo kasi hasa katika malipo kwani baadhi ya abiria wanapolipia kupitia kadi za ki-elektroniki, fedha zao hupotea na kulazimika kulipa tena.
“Abiria wanapoteza fedha zao kutokana na matatizo ya mara kwa mara katika ulipiaji wa mabasi ya mwendokasi na hata wanapolipa bila kadi za kielektroniki wanaweza kuambiwa kuwa chenji hakuna,” amesisitiza.
Ameshauri kuwa ni vyema kampeni ya nenda kwa usalama isifanyike kwa siku moja kwa mwaka badala yake lazima iwe ya kila siku ili madereva na makondakta wapate elimu ya kila siku kuondokana na unyanyasaji wa wanafunzi pamoja na abiria wengine.
More Stories
Askofu Kilaini alaani Klabu ya Simba kutumia msalaba kwa dhihaka
NMB kunufaisha sekta ya kilimo Tanzania
Dk. Mwinyi: Utafiti ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa