Spread the love

NI unyama ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya mtoto Ian Macha mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi nane kudaiwa kutendewa ukatili wa kingono, kimwili pamoja na kutopatiwa matunzo kiasi cha kusababisha kifo chake. Anaripoti Gabriel Mushi … (endelea).

Bibi wa marehemu

Mtoto huyo ambaye alikuwa akilelewa na shangazi yake anayefahamika kwa jina la Janeth Macha mkazi wa Madale jijini Dar es Salaam, amepoteza maisha tarehe 24 Februari mwaka huu katika hospitali ya Mwananyamala Dar es Salaam na kuzikwa katika makaburi ya Mwananyamala tarehe 26 Februari mwaka huu.

TUKIO LILIVYOKUWA

Akizungumza na RAIA MWEMA lililotinga katika maziko ya mtoto huyo, Baba mzazi wa Ian Macha, Jackson Macha ambaye ni mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro alisema baada ya kutokea mgogoro kati yake na mkewe, alitelekezewa mtoto huyo na mkewe na kuanza kumlea mwenyewe kwa kushirikiana na ndugu wa karibu.

Alisema mwaka jana mwezi wa nane dada yake Janeth Macha ambaye Shangazi wa marehemu alienda Moshi kushiriki msiba wa ndugu yake ndipo alipomuomba amkabidhi mwanaye huyo ili arejee naye Dar es Salaam na kumsaidia kumlea.

Alisema licha ya kusita kwa muda na kupata ushauri wa ndugu zake akiwamo baba yake mzazi, alikubali kuwa dada yake huyo ambaye ni Mwalimu wa shule moja ya msingi mkoani Dar es Salaam amchukue mwanaye.

Baba wa marehemu

Alisema baada ya kurejea Dar es Salaam na mwanaye huyo aliendelea kuwasiliana na dada yake yaani shangazi wa marehemu ikiwamo kutoa fedha za matunzo na kumtafuta na kumlipa dada ambaye ni msaidizi wa kazi za nyumbani maarufu kama house girl.

“Nilikuja Dar Disemba mwaka jana na kumtembelea mtoto nikaona anaendelea vizuri. Nilirejea kwenye kazi zangu mikoani lakini ilipofika mwezi Januari nilielezwa kuwa mtoto anaumwa Malaria, nikatuma fedha za matibabu akatibiwa akapona… ilipofika mwezi Februari mwaka huu, Shangazi yake akanieleza tena kuwa mtoto anaumwa sana hivyo nije Dar.

“Wakati najiandaa kuja pamoja na kutafuta nauli, bahati mbaya nikapewa taarifa kuwa amefariki dunia,” alisema.

NDUGU WAMKAGUA MOCHWARI

Aidha, baadhi ya ndugu wa marehemu akiwamo aliyekuwa akimuuguza baada ya Shangazi aliyekuwa akimlea kumtelekezea mtoto hospitali kwa madai ya kukosa muda wa kwenda kumhudumia hospitali, walisema mtoto huyo alipoanza kuumwa alipelekwa katika Hospitali ya Kitengule ambao baadaye walimpa rufaa na kuletwa Mwananyamala.

Akielezea safari hiyo Zamoyoni Omary ambaye aliombwa na shangazi kumhudumia huko hospitali Mwananyamala alisema alimkuta mtoto akiwa amedhoofu, huku hali yake kiafya ikizidi kuwa mbaya kadiri muda ulivyokuwa ukisonga.

Alisema alibaini kuwa yamkini mtoto alikuwa anatendwa ukatili kwa kupigwa na kufinywa na vitu vyenye ncha kali kwa kuwa alikuwa na majeraha mwili mzima.

Pia alidai yamkini alikuwa anaingiliwa kinyume na maumbile baada ya kumbadilisha nguo pindi alipokuwa amejisaidia haja kubwa na kukuta amechanika sehemu hizo za siri kiasi cha kuonesha kuwa alikuwa akifanyiwa mchezo mchafu.

Alisema alipomuita Daktari ili kumkagua alishtushwa na muonekano huo na kudai kuwa hakuelezwa na shangazi aliyekuwa anamlea kuhusu hali hiyo.

“Kwa hiyo wakati wanaendelea kumhudumia na kupigania uhai wake ndipo akafariki,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Bibi wa marehemu, Caroline Mrema ambaye alisema walithibitisha madai ya Zamoyoni baada ya kwenda kuuandaa mwili wa mtoto kwa ajili ya maziko.

“Awali uongozi wa hospitali ulitushauri asizikwe kwanza mpaka afanyiwe hivyo vipimo kupata uhakika wa kuingiliwa kinyume, hata mama yake aligoma asizikwe kwanza lakini Shangazi huyu aliyekuwa akiishi naye alilazimisha basi mtoto akazikwa.

SHANGAZI AKIMBIA MAKABURINI, AMTIMUA HOUSE GIRL, BOY

Bibi huyo aliendelea kueleza kuwa baada ya maziko, Shangazi wa mtoto alikataa kikao cha kuvunja Tanga kufanyika nyumbani kwake Madale.

“Kwanza aligoma sisi ndugu kwenda kuvunja tanga nyumbani kwake, lakini cha ajabu licha ya kwamba yeye ndiye aliyekuwa akiishi na mtoto, hakuna hata jirani wala mumewe ambaye alijitokeza kushiriki mazishi ya mtoto.

“Cha ajabu tulipata taarifa kuwa baada ya mtoto kufariki aliwafukuza kazi wale wasaidizi wake pale nyumbani yaani house girl na house boy ambaye ndiye tunamhisi alikuwa akimfanyia mchezo mchafu mtoto wetu,” alisema.

WAIANGUKIA SERIKALI

Kutokana na madai hayo, ndugu hao wakiongozwa na Baba wa marehemu Jackson Macha waliiomba Serikali kuingilia kati suala hilo na kuwasaidia ili mwili ufukuliwe na Shangazi wa marehemu achukuliwe hatua kutokana na ukatili aliokuwa akimfanyia mtoto huyo.

WAANZISHA VARANGATI

Aidha, baada ya maziko, ndugu hao wa marehemu waliekea nyumbani kwa shangazi wa mtoto Madale ambapo walienda kuripoti kituo cha polisi Madale ambako askari walielekea nyumbani kwake na kumkamata mtuhumiwa huyo Janeth Macha.

Awali ndugu hao kwa kushirikiana na wananchi usiku wa saa tatu, nusura wavunje mlango wa mtuhumiwa huyo ili wamtoe nje lakini uongozi wa mtaa uliwasihi kupunguza munkari.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa wa Kasanga- Madale, Mwajuma Mussa Mrisho alisema hakufahamu kama kulikuwa na msiba katika nyumba ya Janeth.

Alisema pia hafahamu kama mtoto huyo alikuwa kitendewa ukatili lakini baada ya kuzungumza na majirani walimweleza kuwa mtoto huyo tayari alikuwa akitendewa ukatili na mara kwa mara house girl alikuwa akiwaeleza majirani hao.

SHANGAZI AJITETEA, ATIWA PINGU

Aidha, wakati anakamatwa na askari na kupelekwa kituoni Madale kwa mahojiano, shangazi huyo alisikika akiwa anajitetea kuwa licha ya msaada aliokuwa akiutoa kwa mtoto huyo sasa anatuhumiwa kwa mauaji.

“Yaaani nimetoa msaada kwa masikini lakini sasa mnasema nimeua!,” alisikika shangazi huyo ambaye hadi gazeti linakwenda mitamboni bado alikuwa anashikiliwa katika kituo hicho.

HOSPITALI MWANANYAMALA WAJIBU

Aidha, akizungumzia tukio hilo Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala Dk. Zavery Benela alisema baada ya kufuatilia ripoti ya daktari aliyekuwa akimtibu mtoto huyo, amebaini alifariki kutokana na utapiamlo mkali.

Alisema suala la kunajisiwa hana uhakika nalo labda kama hatua zaidi zitachukuliwa na ndugu ili kufahamu ukweli.

Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema bado taarifa za tukio hilo hazijamfikia hivyo anaomba apewe muda ili aweze kuzifuatilia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *