August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ubunifu unalipa- Kinshaga

Spread the love

UBUNIFU unalipa. Ndivyo anavyosema Elia Wiston Kinshaga (27) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KiNshaga Foods and Products inayotumia tunda la Nanasi kuzalisha bidhaa mbalimbali, anaandika Charles William.

Kinshaga akizungumza na mtandao huu amesema, vijana wanapaswa kutumia fursa zilizopo badala ya kusubiri kuajiriwa.

Kinshaga ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilichopo mkoani Morogoro (SUA) akisomea shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara amesema, elimu aliyopata imemsaidia kubuni bidhaa mbalimbali zinazotumia tunda aina ya Nanasi.

“Kwa kutumia elimu niliyoipata wakati nikisoma shahada yangu ya kwanza, nimeweza kuanzisha mradi wa utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kwa kutumia tunda la Nanasi ikiwa ni pamoja na biskuti za nanasi, majani ya chai ya nanasi na zinginezo,” amesema.

Kinshaga amesema, bidhaa zinazozalishwa na kampuni yake kwa sasa, zinasambazwa katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.

Amesema, ujasiriamali unalipa na unasaidia vijana kulikabili tatizo la ajira na hata kuwa sehemu ya suluhu ya tatizo hilo kwa kuwapa ajira wengine.

“Kupitia mananasi ambayo nimekuwa nikiyanunua Morogoro na Geita, kampuni yangu imekuwa ikiyasindika na kutengeneza bidhaa ninazosambaza katika maduka mbalimbali hapa nchini.

“Bidhaa hizo ni bidhaa asilia na hakuna kemikali zinazoweka kama ilivyo kwa wazalishaji wengine, mimi natumia jua tu kukausha nanasi na kutengeneza bidhaa husika,” amefafanua Kinshaga.

Kinaeleza kuwa, alianza kujifunza ujasiriamali mwaka 2012 alipokuwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza SUA ambapo hapo awali, alianza kwa kujishughulisha na biashara ya kupika chakula na kuuza kwa wanafunzi wenzake kabla ya kuanza kuuza kwa watu wengine.

“Nilianza kwa kuwauzia chakula nilichokuwa napika wanafunzi wenzangu watatu, baadaye nikawa maarufu kwa kupika vizuri na nikashawishika kufungua mghahawa wa chakula na kuanza kuuza mpaka sahani 50 za chakula kwa siku.

“Matarajio yangu ni kuwa mfanyabiashara mkubwa zaidi ndani na nje ya nchi katika miaka michache ijayo,” amesema Kinshaga.

Kinshaga kwa sasa anashiriki  katika shindano la mradi bora wa mwaka linaloendeshwa na  mashirika mbalimbali yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF.

 

 

error: Content is protected !!