June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UNFPA, UNICEF wasisitiza ukeketaji kukomeshwa

Spread the love

SHIRIKA la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) yametoa wito kujipanga vyema kumaliza tatizo la ukeketaji (FGM) ifikapo mwaka 2030. Anaandika Aisha Amran.

Taarifa iliyotolewa na Dk. Babatunde Osotimehin ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA na Anthony Lake, Mkurugenzi Mtendaji wa UNCEF imeeleza kuwepo kwa haja ya dunia kuadhimisha siku hiyo kwa kulenga kukomesha kitendo cha ukeketaji.

Mashirika hayo yamesema ukeketaji ni kitendo cha kikatili kinachowanyima wanawake haki yao ya msingi na kuwanyima uhuru kama wanawake.

Viongozi hao wamesema, ukeketaji umesambaa duniani kote ikiwemo Mashariki ya Kati, Asia, Australia, Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Kusini ambako imekuwa kawaida na kuathiri familia.

Wameonya kuwa kama hatua zaidi hazitachukuliwa kutokomeza ukeketaji, idadi ya mabinti na wanawake wanaoweza kuingizwa katika vitendo hivyo inaweza kuongezeka.

Septemba mwaka jana katika mkutano wa kutengeneza mpango wa kimataifa wa maendeleo endelevu, nchi 193 zilikubaliana kuhakikisha kwamba ukeketaji unatokomezwa ifikapo mwaka 2030.

Wamesema wanahitaji kufanya kazi na wataalamu wa tiba za asili pamoja na wataalamu wa kisasa ili kutoa elimu juu ya ukeketaji.

Aidha wamewataka wanawake waliofanyiwa ukeketaji kusaidiwa kupatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za kisaikolojia na nyingine zinazostahili ili kuwapunguzia maumivu waliyoyapata na wanayoendelea kuyapata kutokana na kukeketwa.

Ili kufanikiwa kutokomeza kitendo cha ukeketaji, jamii kwa ujumla inatakiwa kushawishi familia zao kuachana na ukeketaji.

error: Content is protected !!