January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Unafki wa Prof. Kitila huu hapa

Prof. Kitila Mkumbo

Spread the love

NIMESOMA makala ya Dk. Kitila Mkumbo, iliyobandikwa kwenye mitandao ya kijamii inayosema, “CCM kinaimarika, Chadema kinasinyaa na CUF kinakufa.”

Kwa maoni ya Dk. Kitila, pamoja na Chadema kukubalika mbele ya wananchi na kubeba mashabiki wengi, lakini hakipati kura za kutosha katika uchaguzi. Anatoa sababu kadhaa:

Kwa mfano, mhadhiri huyo mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, Chadema kinaonekana siyo mbadala sahihi wa chama tawala.

Licha ya kufanikiwa kuweka wazi mabaya ya chama chake cha zamani, lakini bado kimeshindwa kushawishi wananchi kuwa chenyewe ndiyo mbadala wa CCM, anasema na kuongeza kuwa mbadala wa CCM hajafika na hivyo anawataka wananchi waendelee kusubiri.

Aidha, Dk. Kitila anasema, viongozi wakuu wa Chadema wametumia muda mwingi kufanya kampeni za kumchafua Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini, badala ya kunadi wagombea wake.

Anadai kuwa kitendo cha viongozi wakuu wa Chadema kumtangaza Zitto kama mhaini kwa chama, ili hali wananchi wanajua mchango wake katika mafanikio ya chama hicho, kimesababisha watu wengi kupoteza kabisa imani na Chadema na wengine hawakitaki tena.

Anasema, Chadema hakitaki kukosolewa na kujirekebisha. Ukikikosoa hata kama unachokisema ni kweli, hawachelewi kukuita wewe ni msaliti; pandikizi la CCM, umetumwa na mambo mengine ya kichonganishi kwa lengo la kukuchafua kisiasa.

Dk. Kitila anahitimisha kwa kusema, “Ni heri kutawaliwa na wakoloni weusi (CCM), kuliko wakoloni wekundu (Chadema). Maana hawa ni zaidi ya kudandia meli ya Kigiriki.”

“Ni bora tuendelee kutawaliwa na CCM ambao wanang’ata na kupuliza, kuliko hawa viongozi wa Chadema ambao wanaweza kuiba mpaka tukaingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe,” anaeleza.

Siyo kawaida yangu kujibizana kwenye vyombo vya habari. Nimejifunza kusikiliza na kujibu hoja hizo kupitia mikutano ya hadhara na vikao vya ndani. Lakini katika hili, nimeamua kuvunja mwiko huo ili kujibu upotoshaji huu wa anayejiita msomi – Dk. Kitila Mkumbo.

Kwanza, Dk. Kitila anayeporomosha matusi, kejeli na maapizo; alikuwa kiongozi mwandamizi ndani ya Chadema. Ameondoka katika chama hiki miezi michache iliyopita, baada ya wenzake kumfukuza.

Msomi huyu anayekiombea Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiendelee kutawala, alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC). Alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi – kamati ambayo ilifanya kazi ya uteuzi wa wabunge wa Viti Maalum.  

Mwaka 2010, Dk. Kitila alikuwa mjumbe katika timu ya kampeni. Alifanya kazi hiyo, chini ya uenyekiti wa Prof. Mwesiga Baregu.

Alifukuzwa ndani ya Chadema, baada ya kubainika na kukiri kushirikiana na vikundi vyenye kupandikiza mbegu za ukabila, udini na ukanda. Alikiri kutokuwa mkweli; kuchonganisha viongozi wakuu wa chama; kujihusisha na upinzani dhidi ya chama na kugombanisha baadhi ya viongozi na wanachama.

Hivyo basi, siyo sahihi kwa Dk. Kitila kudai Chadema siyo mbadala sahihi wa CCM. Siyo sahihi kusema, “Ni heri kutawaliwa na wakoloni weusi (CCM), kuliko wakoloni wekundu (Chadema).

Hii ni kwa sababu, kabla ya kufukuzwa uanachama, Dk. Kitila alikuwa mtetezi mkuu wa Chadema dhidi ya poropaganda za aina hii. Aliamini na kuaminisha umma, kwamba Chadema ni chama bora na kinachostahili kukabidhiwa dola.

Kwa mfano, wakati chama tawala kikisambaza vijineno, kuhusu uteuzi wa wabunge wa Viti Maalum, kwamba ulifanyika kwa njia ya upendeleo, rushwa na ghiliba, Dk. Kitila alisimama kidete kutetea Chadema.

Alisema, ndani ya Chadema mambo yote yanatendeka kwa uwazi. Yanafanyika kwa kufuata katiba, kanuni na miongozo. Ni shirikishi. Anachokisema sasa, ni tofauti na kile alichokuwa akikieleza wakati huo.

Pili, kuhusu madai kuwa wakati wote wa kampeni, Chadema kiliacha kunadi wagombea wake, badala yake kikajielekeza katika kumshambulia Zitto, ukweli ni huu. Hakuna mahali popote ambako viongozi wakuu wa Chadema – Freeman Mbowe na Dk. Willibroad Slaa – wamefanya hivyo.

Bali, Dk. Kitila akiwa mkweli atakiri kuwa Mbowe na Dk. Slaa wamemvumilia sana Zitto. Atakiri kuwa mwezi mmoja baada ya anayedai kumtetea, kukabidhiwa wadhifa wa naibu kiongozi wa upinzani bungeni, wabunge wenzake wa Chadema walimpigia kura ya kutokuwa na imani naye.

Hii ni baada ya kutuhumiwa kwa usaliti dhidi ya chama. Kukiri kutenda kinyume na maelekezo ya kamati ya wabunge wa chama hicho, waliopitisha kwa kauli moja, maamuzi ya kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa ufunguzi wa bunge.

Alikiri kushawishi baadhi ya wabunge kutotii maamuzi hayo. Mkutano uliomvua Zitto wadhifa wa kiongozi wa upinzani bungeni, ulifanyika Bagamoyo mkoani Pwani.

Hata hivyo, pamoja na maamuzi hayo kutolewa, Zitto aliendelea kuhudumu katika nafasi yake. Ni kutokana na viongozi wakuu wa Chadema – Mbowe na Dk. Slaa – kuamua kumpa fursa zaidi ya kujipima na kujitafakari.

Dk. Kitila akiwa mkweli atakiri kuwa cheo cha naibu katibu mkuu ndani ya Chadema, hakigombewi. Nafasi hii inapatikana kwa uteuzi unaofanywa na mwenyekiti.

Mbowe aliweka jina la Zitto na kulipeleka kwenye Baraza Kuu (NEC), ili kuidhinishwa. Akampa uwaziri kivuli – waziri wa fedha na uchumi. Hakulazimishwa. Angeweza kuliondoa. Bali alisimama kama kiongozi na kuvumilia yote yaliyokuwa yakisemwa na kutendwa na Kitila na kundi lake.

Aidha, Dk. Kitila akiwa mkweli atakiri kuwa Zitto hakuwahi kukanyaga makao makuu ya Chadema kwa zaidi ya miezi sita, wakati akiwa naibu katibu mkuu. Atakiri kuwa pamoja na kutofanya kazi zake za naibu katibu mkuu, bado aliachwa katika nafasi hiyo kwa madhumuni ya kijirekebisha.

Tatu, Dk. Kitila anasema, licha ya Chadema kushabikiwa mitaani, lakini hakipati kura za kutosha katika uchaguzi kwa sababu wananchi wameona hakiwezi kuwa mbadala wa CCM.

Kinachosikitisha ni pale anayejiita msomi, kutofahamu kuwa baada ya uchaguzi jimboni Igunga ambako Chadema waliporwa ushindi wao, na CCM kushindwa katika uchaguzi mdogo jimboni Arumeru Mashariki, hakukuwa tena na uchaguzi nchini.

Zinazoitwa chaguzi ndogo mbili – uchaguzi mdogo wa Kalenga na ule wa Chalinze, kwa vyovyote vile hauwezi kuitwa uchaguzi. Ule ulikuwa uporaji wa haki za wananchi.

Ni jambo la kushangaza kuona msomi huyu ameshindwa kubaini kuwapo kwa vitendo vya kinyama vilivyofanyika jimboni Kalenga. Ameshindwa kubaini uwapo wa ripoti za kitafiti na zile vyombo vya habari, vilivyoripoti jinsi makada na wabunge wa Chadema walivyotendewa kinyama – kutekwa, kuteswa, kulawitiwa na kubakwa.

Hakika, ukisoma andishi la Dk. Kitila utaweza kuelewa kwa nini Zitto ameingia katika matatizo ndani ya chama chake. Utaelewa kwa nini Dk. Kitila alishiriki kuandaa andishi chafu lililopewa jina la “Mabadiliko.” Utaelewa kwa nini Chadema inasakamwa na chama tawala na vyombo vya dola.

Ni kwa sababu, Dk. Kitila hakuwa na dhamira njema na chama hicho; hivyo akaamua kumtumia Zitto kutaka kukivuruga. Ni muhimu Zitto akasoma andishi la swahiba wake na kulipima.

error: Content is protected !!