July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

UN: Assange wa WikiLeaks alipwe

Spread the love

MMILIKI wa mtandao wa habari za kiuchunguzi wa WikiLeaks, Julian Assange amekuwa akizuiwa, kinyume cha sheria za kimataifa, kutumia uhuru wake na analazimika kulipwa fidia, ndivyo usemavyo uamuzi wa Jopo la Wanasheria walio chini ya Umoja wa Mataifa wanaoshughulikia malalamiko yanayohusu kuwekwa kizuizini. Anaandika Jabir Idrissa.

Katika uamuzi wake wa Februari 5, 2016 walioutolea taarifa ya ufafanuzi Jumamosi, jopo hilo limesema raia huyo wa Australia mwenye umri wa miaka 44, amekuwa akizuiwa uhuru wake isivyo halali na si kweli kwamba uamuzi wake wa kujificha Ubalozi wa Ecuador nchini Uingereza ulilenga kukwepa mkono wa sheria.

Jopo limesema amezuiwa kwa miaka mitano mfululizo: muda aliokaa jela, muda alipozuiwa kutotoka nje na pale alipolazimika kukimbilia ubalozini jijini London kutafuta hifadhi ya kisiasa.

Wanasheria wa jopo hilo wamegundua staili hiyo ya kumfunga mtu imekosa msingi wa uhalali kwani hapakuwa na utaratibu wa kumpatia haki zake kama vile kutibiwa anapougua.

Ripoti ya uamuzi wa jopo hilo imesema mazingira hayo yamezorotesha hali ya afya ya Assange na kuihatarisha.

“Assange hakuamua kwa hiari yake kuishi katika mazingira haya. Februari 2012 timu ya wachunguzi kuhusu tuhuma za utesaji, ilibaini kuwa Chelsea Manning alidhalilishwa alipochukuliwa na kuhojiwa nchini Marekani kuhusiana na ukaribu wake na Assange na mtandao wake,” imesema ripoti ya jopo hilo.

Pia palipatikana ushahidi imara kuwa Marekani ilikuwa ikimchunguza Assange na wakifanya mashauriano na serikali ya Sweden kuhusu uwezekano wa kumkamata na kumsafirisha kwenda Marekani hapo baadaye.

Assange alifungua malalamiko mbele ya jopo hilo Septemba 2014, akidai Sweden na Uingereza zimekuwa zikimfuatilia kutaka kumkamata ili kumkabidhi kwa mamlaka ya Marekani kwa ajili ya kushitakiwa kwa tuhuma za kufanya ujasusi.

Uamuzi wa jopo hilo sio tu ni ushindi kwake binafsi, bali kwa jumla ni kwa haki ya watoa taarifa popote pale duniani kulindwa dhidi ya mashitaka ya jinai na pia kwa wale wanaonufaika kutokana na kazi yao.

Aliomba Ecuador imkinge na hatari ya kukabiliwa na mashaka ya kiusalama yaliyotarajiwa iwapo angekabidhiwa kwa serikali ya Marekani. Alipatiwa hifadhi aliyoomba.

Sweden na Uingereza ziliridhia mkataba wa 1951 wa masharti ya hifadhi ya kisiasa lakini zilikataa kutambua hadhi hiyo na wala haikumhakikishia kutompeleka Marekani.Ikawa na maana kuwa Assange akiendelea kukaa Ubalozini, atakuwa amejihatarishia kuwepo hapo kwa muda usiojulikana, bali akiondoka mtu wa kwanza kubanwa katika vita vipya vya Marekani dhidi ya watoa taarifa za siri kwa vyombo vya habari.

Kwa namna Sweden zilivyojipanga, imeonekana walimkatalia Assange utayari wa kushirikiana katika uchunguzi uliokuwa unafanywa.

Kwa muda wote wa miaka mitano, Mwendesha Mashitaka wao alikataa kumhoji Assange nchini Sweden, London au Ubalozini, na akanyimwa jalada la tuhuma.

Hapo Assange akawa amekataliwa kujitetea na kufuta uvumi ulioenea kutokana na tuhuma nzito alizotajwa kuhusika. Hiyo ikavuruga haki ya asili ya mtuhumiwa kutokuwa na kosa mpaka ahukumiwe na haki yake ya tuhuma zinazomkabili kuchunguzwa kwanza kwa haki.

Jopo kwa kuzingatia hayo, likaridhika kuwa Assange hakutendewa haki, na kwa hakika hakupaswa kusalimisha haki zake za msingi ili tu aepuke mateso.

Sweden na Uingereza zimetakiwa kumlipa fidia japo hakuna kinachotosha kumfariji kwa hasara aliyoipata pamoja na familia yake. Hata hivyo itakuwa kibano kwa mamlaka hizo kutekeleza agizo hilo haraka kwa kuwa kiasi kitaongezeka.

Mfumo wa utoaji haki wa Umoja wa Mataifa uliwekwa kwa lengo la kulinda haki za watu wote, wenye na wasio uwezo duniani kote.

error: Content is protected !!