May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Umoja wa Falme za Kiarabu wapata rais mpya

Mtawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan

Spread the love

 

MTAWALA wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan amechaguliwa rasmi kuwa rais leo tarehe 14 Mei, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya kifo cha Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan aliyekuwa Rais wa umoja huo.

Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan alikuwa akiiongoza UAE tangu mwaka 2014 hii ikiwa ni baada ya Rais Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan ambaye ni kaka yake wa kambo kupatwa na maradhi ya kiharusi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Kwa mujibu wa shirika la habari la Umoja huo WAM, Sheikh Mohamed amechaguliwa na Baraza Kuu la Shirikisho la UAE ikiwa ni baada ya miaka mingi ya kuingoza UAE nyuma ya kaka yake.

Watawala wa shehe saba za UAE walifanya uamuzi huo katika mkutano huo ambao umefanyika leo baada ya Sheikh Khalifa kufariki jana akiwa na umri wa miaka 73.

WAM imeelezea kura hiyo imepigwa kwa kauli moja kati ya watawala wa shehe za nchi hiyo, ambayo pia inajumuisha jiji la Dubai.

“Tunampongeza na tunaahidi utii kwake, na watu wetu wanaahidi utii kwake,” mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, alisema kwenye Twitter baada ya kura kupigwa.

Sheikh Mohamed ni mmoja wa viongozi wenye nguvu zaidi katika ukanda wa nchi za Kiarabu.

Ni mhitimu wa Chuo cha Kijeshi cha Uingereza cha Sandhurst, ameongoza mojawapo ya majeshi yenye vifaa bora zaidi katika eneo la Ghuba.

Akifanya kazi nyuma ya pazia kwa miaka kama kiongozi mkuu, Sheikh Mohamed (61), alibadilisha jeshi la UAE kuwa kikosi kinachotumia teknolojia ya juu, ambacho pamoja na utajiri wake wa mafuta na kitovu cha biashara, kilipanua ushawishi katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Sheikh Mohamed alianza kutawala katika kipindi ambacho kaka yake wa kambo Sheikh Khalifa alikumbwa na magonjwa, ikiwa ni pamoja na kiharusi mwaka wa 2014.

Chini ya uongozi wake ameiwezesha UEA kupeleka wanasayansi kufanya uchunguzi katika sayari ya Mars na kuzindua kinu cha kwanza cha nyuklia.

UAE inaomboleza kwa muda wa siku tatu kifo cha Sheik Khalifa ambapo biashara zitafungwa kote nchini na maonyesho kusitishwa kwa heshima ya Sheikh Khalifa.

error: Content is protected !!