WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ameiagiza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kufanya tathmini ya kina kuhusu matumizi ya shisha, ugoro na sigara za kielektorniki ili kuona namna ya kupunguza au kusitisha matumizi ya bidhaa hizo kwa lengo la kulinda afya ya jamii. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo tarehe 31 Mei, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya kutotumia tumbaku duniani.
Amesema licha ya sheria ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku, sura ya 121 kuzuia matumizi ya baadhi ya bidhaa za tumbaku, kama vile shisha, ugoro na sigara za kieletroniki, bado utekelezaji wa sheria hiyo nchini unasuasua hasa ikizingatiwa zinatumiwa katika mahoteli makubwa hususani yaliyopo jijini Dar es Salaam.
“Sheria haijafutwa, inasema ni marufuku kutumia bidhaa hizo lakini nafahamu bidhaa hizi zimekuwa zikitumika kwa miaka mingi hususani kwa vijana na wazee, hizi bidhaa zipo katika mahoteli makubwa hususani Dar es Salaam,” amesema.
Pia ametoa tahadhari kwa Watanzania kuhusu matumizi ya bidhaa za tumbaki na kuongeza kuwa bidhaa hizo ikiwamo sigara zinasababisha madhara kwa nusu ya watumiaji wake, huku watu zaidi ya milioni nane wakipoteza maisha duniani kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku.
Amesema kati ya vifo hivyo milioni nane, vifo milioni saba hutokana na matumizi ya moja kwa moja wakati milioni 1.2 hutokana na utumiaji wa bidhaa za tumbaku usio wa moja kwa moja.

Pamoja na mambo mengine amesema taarifa alizonazo ni kwamba baadhi ya wafanyabiashara wa shisha huchanganya bidhaa hizo na dawa za kulevya wakati wa uvutaji.
Amesema hali hiyo imekuwa ikileta changamoto kwenye sekta ya afya na kusababisha rasilimali ndogo iliyopo kutokidhi mahitaji ya huduma kwa wagonjwa kwa kushindwa kuwahudumia ipasavyo na hivyo kusababisha vifo ambavyo vingeepukika.
“Mbali na madhara ya kiafya yatokanayo moja kwa moja na matumizi ya tumbaku, pia kuna uchafuzi wa mazingira, tuchukulie mfano sigara takribani 65 ya wavutaji sigara hutupa vishungi vyake barabarani, kwenye fukwe za bahari na maziwa,” amesema.
Amesema takribani tani milioni 25 za taka zitokanazo na tumbaku huzalishwa kila mwaka kutokana na mzunguko wa maisha ya tumbaku na kwamba kuna zaidi ya kemikali 7,000 zinatolewa kwenye mazingira kutokana na matumizi ya sigara huku 70 kati ya hizo zimethibitika kuwa na uwezo wa kusababisha saratani.
“Tanzania inawajibika kuandaa mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupunguza matumizi ya bidhaa za tumbaku ili kuziepusha jamii dhidi ya madhara ya bidhaa hizo ambapo TMDA imeanza kazi ya udhibiti wa bidhaa kwa kusajili bidhaa za tumbaku, kufanya ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara na kuelimisha umma,” amesema.
Ameitaja mikakati mingine kuwa ni kuhakikisha majengo yote ya umma yanatenga maeneo maalum ya uvutaji ili kulinda afya ya jamii, kuchangia kulinda mazingira kwa kupunguza uchafuzi na kusimamia uteketezaji wa bidhaa za tumbaku zisizofaa kwa matumizi.
Waziri huyo pia amesema ili kufikia lengo la kutokomeza athari zote za kiafya zinzosababishwa na tumbaku, Tanzania itaendelea kushiriki katika jitihada za kitaifa na kimataifa za kudhibiti matumizi ya baadhi ya bidhaa za tumbaku kama vile shisha, ugoro na sigara za kielekroniki.
Kila mwaka ifikapo tarehe 31 Mei, 2022 nchi zote duniani kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani huadhimisha siku hii Kka lengo la kuelimisha jamii madhara ya kiafya na athari za mazingira yatokanayo na bidhaa za tumbaku na hatimaye kupunguza na kutokomeza matumizi ya tumbaku ili kulinda afya ya jamii na mazingira.
Leave a comment