July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ummy awachongea Ma-DED kwa Rais Samia

Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu

Spread the love

 

WAZIRI Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, awachukulie hatua Wakurugenzi wa Halmashauri (DED), wanaoshindwa kupeleka asilimia 40 ya mapato ya ndani ya halmashauri zao, kwenye miradi ya maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Ummy ametoa ombi hilo leo Jumatatu, tarehe 21 Juni 2021, akizungumza katika hafla ya uapisho wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Batilda Salha Burian na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Zuwena Omari Jiri, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Waziri huyo wa Tamisemi amemshauri Rais Samia, awaondoe wakurugenzi wanaoshindwa kupeleka fedha hizo, kama anavyowaondoa wakurugenzi wanaopata hati chafu, katika ripoti za ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Sisi tutakuletea mapendekezo, badala ya kuwahukumu wakurugenzi kwa kupata hati chafu na kuwaondoa, nadhani hili la kutopeleka fedha wachukuliwe hatua,”

“ Sababu wanazikusanya kutoka kwa wananchi, wanatakiwa kuzirudisha kwa wananchi halafu hawapeleki. Wanakusanya hela wanatumia kwa matumizi ya kawaida,” amesema Ummy.

Ummy alitoa ombi hilo, wakati akizungumzia mwenendo wa ukusanyaji mapato na matumizi ya halmashauri za Mkoa wa Tabora.

Ambapo amesema halmashauri hizo hazitekelezi agizo la kupeleka asilimia 40 ya mapato, katika miradi ya maendeleo.

Waziri huyo amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, imepeleka asilimia 18 ya fedha hizo, huku Sikonge ikipeleka 16% na Igunga 21%.

“Maelekezo ya rais ni kila shilingi inayokusanywa, asilimia 40 ilipelekwe kwenye miradi ya maendeleo mfano elimu, afya, barabara na miundombinu, lakini halmashauri nyingi hazitekelezi,” amesema Ummy.

Ummy amesema Mkoa wa Tabora unasua sua katika ukusanyaji mapato na kumuagiza Balozi Batilda, akasimamie suala hilo.

“Sasa hivi Tabora, Dk. Batilda tuna changamoto ya ukusanyaji mapato ya halmashauri. Ambapo rais alinielekeza nisimamie kikamilifu ukusanyaji mapato. Hadi Mei 2021, makusanyo ni asilimia 69, wakati kitaifa ni asilimia 94, unayo kazi kuhakikisha halmashauri zinafanya vizuri,” amesema Ummy.

error: Content is protected !!