ONGEZEKO la vifo vya wajawazito hapa nchini linachangiwa na umbali wa vituo vya afya katika halmashauri zilizopo vijijini pamoja na ubovu wa miundombinu, anaandika Esther Macha.
Stephen Africa, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la HIMSO amesema kuwa wanawake wajawazito wanaoishi vijijini wataendelea kuwa katika hatari ya kupoteza maisha iwapo hawatasogezewa huduma za kiafya pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu.
Alikuwa akizungumza katika mkutano mkuu wa shirika hilo mkoani Mbeya.
“Tafiti zilizofanywa na shirika la PATH mwaka 2012 lilibaini asimilia 61 ya wanawake nchini hawakuweza kujifungua kwenye vituo vya afya kutokana na umbali mrefu, asilimia 44 walikosa usafiri wa kuwafikisha kwenye vituo vya afya.
“Tafiti zingine zilifanywa mwaka 2010 juu ya ubora wa mfumo wa rufaa wa afya ya uzazi vijijini Tanzania ulionyesha kuwa mfumo huo ni muhimu katika kusaidia huduma za afya ya uzazi,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza kuwa wanawake wengi hawazingatii ushauri wa rufaa kutokana na changamoto ya ufinyu wa rasilimali fedha na miundombinu duni ya usafiri iliyopo vijijini.
Shirika la HIMSO linatoa huduma za kiafya katika halmashauri za Kyela, Rungwe na Busokelo zilizopo mkoani Mbeya, na kwa upande wa mkoa wa Songwe shirika hilo linatoa huduma zake katika wilaya ya Mbozi.
Kwa upande wake William Ntinika, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya amepongeza jitihada kubwa ambazo zinafanywa na shirika hilo katika kushughulikia afya ya uzazi kwa wanawake.
“Serikali inatambua na kuunga mkono jitihada za shirika hili katika kusaidia makundi ya wenye vipato duni na makundi maalum kama waishio na virusi vya Ukimwi, wajawazito, na watoto waishio kwenye mazingira hatarishi,” amesema.
Leave a comment