September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Ulissu’ wamponza Michael Wambura

Richard Wambura (mwenye shati jeupe) akielekea kupanda gari la Magaereza kwenda rumande

Spread the love

MICHAEL Richard Wambura, aliyepata kuwa Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), amepandishwa kizimbani jijini Dar es Salaam. Ameshitakiwa kwa makossa kumi na saba (17), yakiwamo ya kutakatisha fedha. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Pamoja shitaka hilo ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sharia za Tanzania, Wambura ameshitakiwa kwa makosa ya kughushi, kutoa nyaraka za uwongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, mwendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), George Barasa alisema, mshtakiwa alitenda makosa hayo, tarehe 6 Julai 2004 jiji la Dar es Salaam.

Katika shauri hilo, linalosikilizwa na Kelvin Mhina, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Barasa anasadiwa na wenzake wawili, Moza Kasubi na Imani Mitumezizi.

Wambura anatetewa katika shauri hilo lililovuta hisia za wengi na wakili wa kujitegemea, Majura Magafu.

Haya yanatokea wiki moja kabla, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, kutaka Wambura ashughulikiwe kwa kile alichokiita, “anaaibisha TFF na taifa.”

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa TFF jijini Arusha, Karia alimfananisha Wambura na wanasiasa wa upinzani, Tundu Lissu, jambo ambalo lilizusha tafrani kubwa kwa wapenda soka na baadhi ya wafuasi wa Lissu.

Alisema, “…nimesema kama kuna ‘ma -Tundu Lissu’ kwenye mpira, nadhani mnaelewa Lissu anahangaika kwenye vyombo vya habari kuikashifu serikali, na Wambura anazungumza kwenye vyombo vya habari kuikashifu TFF na uongozi wa TFF.”

Alisema, “watu kama hawa wanatakiwa kushughulikiwa kwa nguvu zote, ili kulinda heshima ya TFF na taifa.”

Lissu ni mbunge wa Chadema, ambaye ameshambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.” Kwa sasa, yuko kwenye ziara ya Ulaya na Marekani, akieleza kilichompata na kuituhumu serikali ya Rais John Magufuli, kukandamiza demokrasia nchini.

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio, Wambura kwa nia ya kutapeli  alitengeneza barua ya  kughushi; akionyesha imeandikwa na E. Maganga akidai kurejeshewa kiasi cha USD 30,000 (Sh. 95 milioni) pamoja na riba.

Maganga ambaye ni mtendaji mkuu wa kampuni ya Jeck system, anadaiwa kuwa aliwahi kuikopesha TFF kiasi hicho cha fedha ambacho kimechukuliwa na Wambura.

Katika shtaka la kutoa Nyaraka ya uongo, Mahakama imeelezwa kuwa mshtakiwa alitoa barua ya tarehe 6 Julai 2004, akidai imeandikwa na Maganga huku akijua kuwa siyo kweli.

Aidha, Wambura anadaiwa kujipatia kiasi jumla ya zaidi ya Sh. 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa Jek huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika moja ya mashtaka hayo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, imedaiwa kuwa 17 Juni 2015, katika ofisi za TFF, Wambura alijipa Sh. 10 milioni kutoka shirikisho hilo kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ya Jeck.

Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kuwa kati ya 15 Agosti  na Oktoba 21 mwaka 2015, huko katika ofisi za TFF mshtakiwa alijipatia Sh. 25,050,000 milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Amedaiwa pia kati ya 16 Machi na 21 Oktoba 2015, Wambura alijipatia Sh. 75,947,924 milioni kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali.

Mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi hiyo imefunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi ambapo mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza.

Nao upande wa mashitaka umedai mahakamani hapo kuwa upelelezi katika kesi hiyo, bado haujakamilika.

Kwa upande wake, Magafu aliomba mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo kwa sababu mashitaka yote 17 yaliyopo mahakamani, hakuna shitaka hata moja lilolofunguliwa chini ya sheria ya  uhujumu uchumi.

Alisema, mashitaka ambayo mteja wake ameshitakiwa nayo, yamefunguliwa chini ya kesi za kawaida za jinai ambayo yanamruhusu mshtakiwa kuyajibu.

Kufuatia hoja hiyo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi 14 Februari 2019, ambapo kesi hiyo itakakuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Michael Wambura, anakuwa kiongozi watano wa soka hapa nchini kufikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa makossa ya utakatishaji fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Wengine walioshitakiwa, ni Jamal Malinzi, aliyekuwa rais wa TFF; Celstine Mwesiga, aliyekuwa katibu mkuu, Godfely Nyange (Kaburu), makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba na Evas Aveva, rais wa klabu hiyo.

Hata hivyo, historia ya Wambura katika mapambano ya kugombea madaraka kwenye klabu za Simba na TFF, ilianzia tokea alipokuwa katibu mkuu wa chama cha Mpira wa Miguu nchini, wakati huo kikijulikana kama FAT.

Aling’olewa kwenye chama hicho kwa “sululu” lililoandaliwa na kusimamiwa na wadau wa soka, kupitia Leodigar Tenga, ambaye ameliongoza shirikisho hilo kwa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minane (8) ya uongozi wake.

Katika siku za karibuni, Wambura alianza kukwaruzana na rais wa TFF, Karia, kutokana na hatua yake ya kutetea nafasi yake ya makamu wa rais wa shirikisho hilo.

Ni kupitia sakata hilo, ndipo Wambura alishitakiwa na TFF kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ambako lilimfungiwa maisha kujihusisha na mchezo wa mpira wa miguu kwa madai kuwa amepeleka suala la michezo kwenye mahakama ya kawaida.

error: Content is protected !!