August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ulinzi wa kutisha, Lissu bado rumande

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imezungukwa na askari wa Jeshi la Polisi waliojihami kwa silaha za moto wakati Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu akisubiriwa mahakamani hapo, anaandika Faki Sosi.

Lissu alikamatwa juzi na Jeshi la Polisi mkoani Singida na kusafirishwa usiku wa manane, akilazwa Chamwino, Dodoma kabla ya kufikishwa Dar es Salaam mchana wa jana na kuhojiwa kwa tuhuma za uchochezi huku akinyimwa dhamana na kulazwa rumande.

Katika mlango mkuu wa kuingilia mahakama ya Kisutu anapotarajia kupandishwa kizimbani leo, ukaguzi mkali unaendeshwa kwa kila anayeingia huku waandishi wa habari wakikumbana na adha ya kuzuiliwa kwa muda na wananchi wanaofika kwa lengo la kusikiliza kesi hiyo wakizuiliwa.

Licha ya kukaguliwa na kuonyesha kitambulisho chake cha kazi lakini mwandishi wa mtandao huu alizuiliwa kuingia mahakamani hapo kwa sababu zisizoeleweka mpaka baadaye mmoja kati ya askari wa doria alipothibitisha kuwa anafahamiana naye.

Mpaka kufikia mchana huu (13:00) wabunge kadhaa wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wamewasili katika katika viunga vya mahakama hii akiwemo Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe.

Wabunge wengine waliofika mahakamani hapo mpaka sasa ni Riziki Ngwali Mbunge Viti Maalum CUF, Saed Kubenea Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Joseph Haule Mbunge wa Mikumi, James Mbatia Mbunge wa Vunjo, na wengineo.

Mtandao huu utaendelea kukujuza kila kinachoendelea katika mahakama ya Kisutu ambapo mpaka sasa bado Tundu Lissu hajafikishwa mahakamani hapo na jeshi la Polisi, akiendelea kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

error: Content is protected !!