Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ulinzi, mambo ya nje waelezea mafanikio mwaka mmoja wa Samia madarakani
Habari za Siasa

Ulinzi, mambo ya nje waelezea mafanikio mwaka mmoja wa Samia madarakani

Dk. Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Spread the love

 

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, zimeeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja, wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wizara hizo zimetaja mafanikio hayo jana tarehe 16 Machi 2022, kwa nyakati tofauti jijini Dodoma na Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, amesema wizara yake kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), imefanikiwa kulinda mipaka ya Tanzania pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Amesema, wizara hiyo kupitia makubaliano ya kikanda imeshirikiana na Msumbiji, kudhibiti ugaidi uliyoibuka katika mipaka ya nchi hizo mbili.

“Tumekuwa na changamoto katika mpaka wetu na Msumbiji, ambapo kikubwa kumekuwa na ugaidi, ni upande zaidi wa wenzetu lakini kwa pamoja tumeweza kushirikiana kudhibiti changamoto hii,” amesema Dk. Tax.

Amesema mafanikio hayo yametokana na Serikali hiyo, chini ya Rais Samia, kuiwezesha wizara katika utekelezaji majukumu yake, kwa kuipatia fedha zaidi ya asilimia 80, ilizotengewa kwenye bajeti, ambazo zimetumika kununua vifaa na dhana.

“Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa, nchi yetu iko salama na amani inalindwa, kwa kuimarisha umoja, mshikamano na utulivu nchini. Kuhakikisha kiasi cha fedha kilichotengwa kwa matumizi ya wizara kwa zaidi ya asilimia 80, kinatolewa.

“Ina maana tumepokea kiasi kikubwa na tumebakiza asilimia 20, ambayo tunaamini itamaliziwa kwani imebaki miezi mitatu,” amesema Dk. Tax.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula

Dk. Tax amesema, “tukiangalia mwenendo wa huko nyuma na wa sasa, inaonyesha wazi wizara imepewa uzito mkubwa kwenye Serikali ya Awamu ya Sita na tunaweza kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi.”

Akielezea zaidi mafanikio hayo, Dk. Tax amesema wizara yake imewezeshwa kulipa madeni ya wazabuni yenye thamani ya Sh. 175 bilioni.

Aidha, Dk. Tax amesema, wizara imefanikiwa kushughulikia migogoro sugu ya ardhi 74, katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Lindi, Mara, Morogoro, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga na Singira, ambapo Sh. 8.15 zimetumika kulipa fidia wananchi kwenye baadhi ya maeneo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, akizungumza jijini Dar es Salaam, amesema wizara yake imefanikiwa kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na mataifa ya nje, pamoja na maslahi ya nchi kupitia utekelezaji wa miongozi na sera ya mambo ya nje ya 2001.

Akitaja mafanikio mengine, Balozi Mulamula amesema Tanzania ilichaguliwa na nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), kuwa makamu wa rais wa mkutano wa 76 wa Baraza la umoja huo. Pia, ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Uchumi na Jamii la UN, kwa kipindi cha miaka mitatu (Januari 2022 hadi Desemba 2024).

Balozi Mulamula amesema, wizara yake imefanikisha uwekaji saini mikataba sita yenye thamani ya Sh. 1.77 trilioni, na upatikanaji wa Euro 425 milioni, kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesena nafanikio hayo yametokana na ziara ya Rais Samia katika mataifa mbalimbali, alizofanya muda mfupi baada ya kuingia madarakani.

Aidha, Balozi Mulamula amesema ziara iliyofanywa na Rais Samia, Februari mwaka huu katika Umoja wa Falme za Kiarabu, wizara yake ilifanikisha kusainiwa kwa hati za makubaliano 36 baina ya Tanzania na umoja huo.

Balozi Mulamula ameongeza, katika kipindi hicho, Tanzania imefungua balozi mpya mbili katika nchi za Austria na Indonesia, na kupeleka balozi zake kufikia 45. Huku mabalozi 25 wakiteuliwa.

Zaidi ya hayo amesema, kutokana na mahusiano ya Tanzania na mataifa ya nje kuimarika, Serikali ilipata msaada kiasi cha Yuani 100 (Sh. 35.37 bilioni), kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo, ikiwemo kupanua miundombinu ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na mradi wa uhifadhi miamba katika eneo la Ngorongoro.

Pia, amesema Serikali ya India ilitoa mkopo nafuu wa Dola za Marekani 503 milioni, kwa ajili ya usambazaji maji kwenye miji 24 ya Tanzania Bara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!