August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ulinzi CUF Mtendeni usipime

Spread the love

UONGOZI wa juu wa Chama cha Wananchi (CUF) umeimarisha mfumo wake wa ulinzi kwenye Makao Makuu yake yaliopo mtaa wa Mtendeni, mjini Zanzibar wakati huu wa kuendelea kwa mgogoro wa uongozi, anaandika Jabir Idrissa.

Uimarishaji wa ulinzi unatekelezwa kwa makusudi hasa baada ya kupatikana taarifa ambazo hazijathibitishwa mpaka sasa, kwamba Profesa Ibrahim Lipumba, aliyefukuzwa uanachama wiki mbili zilizopita, amepanga kutinga kwenye ofisi hizo.

Mbali na ushuhuda kwamba ‘askari’ wa chama waitwao Blue Guards wameongezwa, mitaa yote na vichochoro vinavyoingilia mtaa wa Mtendeni, ina walinzi wengi wakiwemo waliowekwa kwa siri.

“Si uongo, mfumo mzima wa ulinzi hapa makao makuu Mtendeni umeimarishwa. Unajua zilienea taarifa za kiitelijensia kuwa Profesa Lipumba anatarajiwa kuja na kutaka kuingia ofisini,” amekaririwa mlinzi mmoja wa CUF.

Mlinzi huyo alipoulizwa kwa alivyosikia Profesa Lipumba aende Mtendeni kufanya nini wakati anajua hatua hiyo huenda ikamsababishia matatizo, mlinzi huyo alisema, “Tunasikia ametangaza kuwa anataka kuja makao makuu eti kukutana na watendaji wa chama waliopo huku Zanzibar.”

Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hili upande wa Zanzibar kwani hata Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alipoulizwa, ghafla simu yake ilikatika na haikupatikana tena.

Katika moja ya vikao vyake na waandishi wa habari akiwa Ofisi Kuu za CUF Buguruni ambako Profesa Lipumba amejichimbia na genge lake la watu wachache, amesikika akisema kuwa anakusudia kwenda Zanzibar kukutana na watendaji.

Profesa Lipumba alitangaza mwishoni mwa wiki kuwa anawataka watendaji wote ndani ya chama kufika ofisini ili kufanya kazi walizoteuliwa kuzifanya na kwamba kwa yule atakayekosa kufika na kukakosekana taarifa ya maandishi ya sababu yake, atahesabiwa kuwa amejiondoa katika nafasi.

“Nitateua wanachama wengine wa kufanya kazi walizopangiwa wale watendaji watakaokuwa wameshindwa kutokea,” alisema. Hata hivyo kwa taarifa zilizopatikana jana, hakuna mtendaji hata mmoja aliyemtii Profesa Lipumba.

Mtendaji mmoja kwenye ofisi hizo ameiambia MwanaHALISIonline kuwa hana moyo wa kufika ofisini kufanya kazi kwa kuwa mgogoro umesababisha kuwepo mazingira ya hofu Ofisi Kuu Buguruni.

“Hivi ukiangalia kwa mtu mwenye akili timamu, unakwenda ofisini pale kufanya kazi gani kama sio kutafuta kusakamwa,” alihoji mtendaji huyo wa ngazi ya juu.

Prof. Lipumba juzi alitangaza kutengua uteuzi wa watendaji uliofanywa wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) wiki iliyopita mjini Zanzibar.

Mvutano unaendelea kugubika CUF ambayo Prof. Lipumba ameshika upande mmoja akiwa na viongozi wawili tu – Mgdalena Sakaya na Abdul Kambaya – ambao walisimamishwa uanachama pamoja naye 28 Agosti.

Sakaya alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama Bara wakati Kambaya alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma. Wote wanaendelea kujitambua kuwa ni viongozi halali.

Prof. Lipumba ambaye anadai kusimamia kutambuliwa na Msajili wa Vyama kama mwenyekiti halali kwa hatua yake ya kutengua kujiuzulu kwake, alifukuzwa uanachama 27 Septemba kufuatia kutotii wito wa kufika mbele ya Baraza Kuu kujitetea kwa tuhuma za kuvamia Ofisi Kuu Buguruni na kuvunja ofisi na kuharibu mali za chama.

Upande mwingine wa mgogoro unaongozwa na Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad anayeungwa mkono na zaidi ya asilimia 90 ya Baraza Kuu la Uongozi.

 

error: Content is protected !!