July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ulingo- Uchaguzi haukuwa wa huru na haki

Spread the love

ULINGO – Taasisi inayofanya kazi ya kuwajengea uwezo wanawake katika siasa, imesema uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 “haukuwa wa huru na haki kwa upande wa wagombea na wapiga kura wanawake.” Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kauli hiyo ya Ulingo imetolewa na Eva Maria Semakafu- Mratibu wa Ulingo, leo jijini Dar es Salaam kwa waandishi wa habari, wakati taasisi hiyo ilipokutana na waangalizi wa ndani kutoka mikoa 18, ambao walijikita kuangalia masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kabla na wakati wa uchaguzi.

Semakafu amesema “mara nyingi waangalizi wa uchaguzi hawatoi matokeo yanayohusu wanawake katika uchaguzi…mwaka huu tumeamua kutuma waangalizi 56 wa ndani katika mikoa 18. Hivyo tumebaini uchaguzi haukuwa wa huru na haki kwa sababu ya vitisho na unyanyasaji waliofanyiwa wagombea na wapiga kura wanawake.”

“Sisi kwetu wanaharakati tunasema, uchaguzi utakuwa wa huru na haki endapo wagombea na wapiga kura wanawake watawekewa mazingira ya demokrsia bila ubaguzi hasa kwenye vyama vya siasa,” amesema Semakafu.

Aidha, Shakira Mayamawa- mtafiti kutoka Ulingo ameutaja unyanyasaji wa kijinsia uliojitokeza kabla na wakati wa uchaguzi kuwa ni; wanawake kukataliwa na waume zao kuhudhuria katika kampeni, matumizi ya lugha chafu dhidi ya wagombea wanawake na wanawake walioonekana kuunga mkono chama fulani cha siasa kutoka kwa wanaume hasa vijana.

“Katika mchakato huu wa uchaguzi, nafasi ya ushiriki wa wanawake imekuwa finyu. Katika kampeni za vyama vyote vya siasa, kwa kiasi kikubwa wanawake walionekana ni wahamasishaji majukwaani. Hawakupewa nafasi ya kuwa waongeaji kama ambavyo walipewa wanasiasa wanaume,” amesema Mayamawa.

Mayamawa amesema elimu inapaswa kutolewa ili kuondoa unyanyasaji katika michakato ya uchaguzi. Vinginevyo changamoto hizo zinaweza kuzuia ushiriki wa wanawake katika siasa.

error: Content is protected !!