July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ulingo kuwafunda wanawake 2000

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Ave-Maria Semakafu

Spread the love

ULINGO- Taasisi inayofanya kazi ya kuwajengea uwezo wanawake katika siasa, inatarajia kufanya mafunzo kwa wanasiasa wanawake 2000 nchini nzima. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kauli ya Ulingo inakuja ambapo tayari wanasiasa kadhaa wemetangaza nia au wanatajwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Hawa ni Lazaro Nyarandu – Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangalla – Mbunge wa Jimbo la Nzega, Edward Lowassa –Mbunge wa Jimbo la Monduli, Stephen Wassira-Waziri wa Kilimo, Bernard Membe-Waziri wa Mambo ya Nje, Mizengo Pinda-Waziri Mkuu, January Makamba-Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wengineo

Hata hivyo, wengi wa wanaotajwa au kujitokeza wenyewe ni wanaume. Hii ndiyo ikawa sababu ya MwanaHALISIOnline kuwatafuta Ulingo ili kujua mikakati yao ya kuwahamasisha wanawake wajitokeze.

Dk. Eva Maria Semakavu – Mratibu wa Ulingo amesema, “mafunzo haya yatafanyika ndani ya mwezi huu wa nne, katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar”.

“Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, tuliviomba vyama vyote vya siasa kutupatia majina ya wanawake ambao wana nia ya kuingia kwenye uongozi wa kiasa. Mwaka jana tumepata majina 2000. Tutawagawa katika makundi na kuwapa mafunzo kwa muda wa wiki moja,” amesema.

Semakafu amesema, baada ya mafunzo hayo, wanawake watakuwa na uwezo kushiriki katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa ili kushiriki uchaguzi mkuu.

“Kwa kuwa mgombea anatapaswa kuteuliwa ndani ya chama cha siasa ili aweze kushiriki katika kutafuta uongozi, baada ya mchakato wa vyama kumalizika, tutawajengea tena uwezo.

“Awamu ya pili tutawajengea uwezo kuhusu mbinu mkakati zitakazowasaidia wakati wa kampeni na tutawashawishi kujitokeza hadharani kutangaza nia,” amefafanua Dk. Semakavu.

Amesema, wanasiasa waliojitokeza na kutangaza nia ni wale wenye majina makubwa (maarufu) na nguvu ya rasilimali fedha. Tofauti na wanawake wengi ambao hawana uwezo huo.

“Wanawake wanasiasa wanakabiliwa na vikwazo vingi ukilinganisha na wanaume. Hasa rushwa ya ngono. Wanaume waliojitokeza ni wenye nguvu ya pesa na majina, huku wengine wakifuatwa na vikundi vya kijamii tofauti na wanawake hasa wa ngazi ya chini ambao uchumi wao ni mdogo,”amesema.

error: Content is protected !!