August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukuta wamtia kiwewe waziri wa JPM

Spread the love

MSIMAMO wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuendesha Operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta), umemtisha waziri wa Rais John Magufuli, anaandika Christina Haule.

Chadema wameendelea kusisitiza kwamba, Septemba Mosi mwaka huu watafanya maandamano na mikutano licha ya Rais Magufuli na Jeshi la Polisi nchini kuzuia.

George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) bila kutaja chama, ameagiza Wakuu wa Mikoa na Wialaya kuzuia kile alichoita ‘uvunjifu wa amani’ unaotaka kufanywa na wanasiasa.

Simbachawene amesema hayo jana kwenye Kikao Kazi cha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na viongozi wa TAMISEMI kilichofanyika mkoani Morogoro.

Amesema kuwa, Watanzania hawapaswi kuthubutu kufuata maelekezo ya mtu yeyote yanayosimama kwenye kuvunja amani ya nchi na kwamba, amani iliyopo ikiharibiwa, kuirejesha itakuwa kazi.

Aidha, Simbachawene amewataka wananchi kutambua kuwa, suluhisho lolote linalohusu masuala ya kiserikali linapaswa kuzungumzwa au kuchukuliwa hatua ndani ya Bunge na kwamba, kutoka nje na kuanzisha maandamo ni sehemu ya kuleta uvunjifu wa amani.

“Wabunge kutoka ndani ya bunge ni sawa, kwasababu wanataka serikali na jamii ijue kuwa wamepinga kitu fulani.

“Lakini baadaye wanapaswa kurejea na kuendelea na kitu kingine na sio kwenda nje kushawishi maandamano ambayo hayanatija,” amesema Simbachawene.

Amesema, kufanya maandamano au mikutano si sehemu ya kupata majibu bali ni kurudisha nyumba suala zima la maendeleo kwa wananchi ambao watatumia muda wao mwingi kwenye masuala hayo na kuachakufanya shughuli za maendeleo.

“Kutuingilia wakati tunatekeleza ahadi zetu mnatuonea kwasababu, suala la kampeni za uchaguzi lilishakwisha na sasa ni kutekeleza ahadi kwa chama kilichoshinda, kampeni tusubiriane kwenye uchaguzi mwingine jamani,” amesema.

Steven Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema, hatosita kutoa amri ya kumkamata mtu au watu watakaohisiwa kufanya vikao vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

Kebwe amesema, suala la uvunjifu wa amani ya mkoa na hatimaye nchi halitavumilika na kwamba, atahakikisha anawashughulikia wavunjifu wote wa amani kwa kushirikiana na kamati yake ya ulinzi na usalama mkoa hasa pale watakapobainika watu kujaribu kutekeleza suala lao la maandamano hapo Septemba Mosi mwaka huu yanayotarajiwa kufanywa na Chadema.

Akizungumzia mazoezi ya Jeshi la Polisi mkoani humo yaliyofanyika kuanzia tarehe 19 Agosti mwaka huu na yakidaiwa kuhusishwa na kutisha wananchi amesema, mazoezi hayo hayahusiani na suala lolote bali ni sehemu ya kawaida kwa kuwa hakuna jeshi linalokaa bila kufanya mazoezi.

error: Content is protected !!