August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ukuta bado moto, Lissu ashinda Kisutu

Spread the love

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imempandisha kizimbani, Denis Temu, Mkazi wa Tabata Bima, jijini Dar es Salaam kwa madai ya kushabikia Ukuta, anaandika Faki Sosi.

Wakati Jamhuri ikiendelea kuwapandisha kizimbani watuhumiwa mbalimbali, Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameendelea kushinda mahakamani kutetea watuhumiwa wa Ukuta.

Ukuta ni Umoja wa Kupinga Udikteta nchini, operesheni hiyo ilitangazwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa Julai mwaka huu kwa niaba ya Kamati Kuu ya chama hicho.

Operesheni hiyo ilipangwa kuanza kufanyika Septemba Mosi mwaka huu lakini viongozi wa dini, taasisi za kiraia na serikali ziliutaka uongozi wa Chadema kutofanya mikutano na maandamano chini ya Ukuta ili kuweka mazingira sawa ya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Temu amepandishwa kizimbani leo kwa tuhuma za kuandika maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi kwenye ukurasa wake wa kijamii wa ‘Facebook’ kuhusu Ukuta.

“Nipo tayari kwa Ukuta, naomba mnikabidhi askari 10, nikiwashindwa Mungu anihukumu.”

Kwenye kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi ya kulidhalilisha Jeshi la Polisi.

Akisoma shitaka hilo Salumu Mohammed, Wakili wa Serikali mbele ya Amillius Mchauru, Hakimu Mkazi Mkuu amedai kuwa, mtuhumiwa huyo aliandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mohammed amedai kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 30 Agosti mwaka huu.

Kwenye kesi hiyo, Mohammed anawakilishwa na Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Hata hivyo, Mohammed amekana shitaka hilo ambapo amedhaminiwa na wadhamini wawili kwa wadhamini kusaini hati ya Sh. 500,000 kila mmoja.

Upande wa Jamhuri umedai kwamba, upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 12 Oktoba mwaka huu.

Mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi kabla ya  Septemba Mosi.

Jeshi la Polisi na serikali walipinga kuwepo kwa operesheni Ukuta kwa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa hali nzuri ya usalama nchini.

Wakati akiahirisha maandamano na mkutano ya Ukuta Mbowe alisema, “tunajua uamuzi huu utawaumiza sana wafuasi wetu, na uamuzi huu umeniumiza sana hata mimi mwenyewe.

“… lakini ni nani miongoni mwa viongozi wetu na wanachama wetu ambaye anaweza kuombwa kuahirisha jambo na viongozi wa madhebu na dini zote hapa nchini na akawakatalia.

“Polisi na Serikali wajue kuwa, hatuahirishi maandamano na mikutano yetu kwa sababu ya mazoezi, risasi au mabomu ya polisi. Hatuahirishi kwasababu ya usafi wao, wanaofanya kesho na wala hatuahirishi kwasababu ya ndege za kijeshi zinazoruka, ila tumeamua kuwaheshimu viongozi wetu dini.

Tunawaomba wanachama wetu, wapenzi wetu na wapenda demokrasia kote nchini watusamehe na wakubali kuwapa viongozi wa dini hizi wiki tatu, watafute suluhu kwa kuonana na Rais na ikishindikana, hatutarudi nyuma. Tutaingia barabarani.”

Siku chache baada ya kauli hiyo, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ulikosoa hatua ya viongozi wa dini kuwasihi Chadema kuendesha maandamano na mikutano ili kutafuta suluhu kutokana na mvutano uliokuwepo kati ya chama hicho na vyombo vya dola nchini.

error: Content is protected !!